Monday, March 3, 2008

Mkapa hali mbaya


Wakiongea na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, jijini Dar es Salaam, wikiendi iliyopita, wachambuzi hao walifafanua kwamba ‘ishu’ ambazo zinaelekea kumkaanga Mkapa ni ile ya Akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) na mikataba yote ambayo ilisainiwa wakati wa utawala wake.

Katika mikataba, kipimo cha kwanza walikielezea kuwa ni kauli ya wafanyakazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) ambao walimshushia lawama nzito Mkapa kuwa utawala wake ndiyo umeifanya taasisi hiyo iwe hohe hahe.

“Waswahi wanasema mwehu mtoto akikuvua nguo usimkimbize, ni kweli Mzee Mkapa hataki kukimbizana na watoto, lakini ukimya wake unafanya hali yake izidi kuwa mbaya kisiasa,” alisema Dk. Zaid Kamsa wa Dar es Salaam.

Dk. Kamsa ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu, Chuo Kikuu cha Arizona Marekani katika masomo ya Sayansi ya Siasa (Political Science), aliongeza: “Kikwete ameshatangaza Mzee Mkapa asibughudhiwe, lakini ni jambo gumu kwa sasa.

“Ni jambo gumu kwakuwa kuna uwezekano watu wakaendelea kumrushia madongo na kwasababu hali ya sasa ni mbaya, itakuwa ngumu kumsafisha kutokana na hili wimbi la ufisadi.”

Ijumaa iliyopita, wafanyakazi wa TANESCO walifanya kikao kujadili mikataba mibovu ya shirika hilo ambapo moja kwa moja walimrushia lawama Rais Mkapa enzi ya utawala wake kwa kuingia mikataba mibovu kama ule wa IPTL na Songas.
Wakati akiwashiwa moto TANESCO, tayari kumekuwa na msukumo kutoka kwa watu wengi, wakitaka rais huyo mstaafu awajibishwe kwenye sakata la EPA ambalo lililomfukuzisha kazi, aliyekuwa gavana wa Benki Kuu, Daud Ballali.

Pointi iliyo nyuma ya shinikizo hilo ni kuwa Mkapa awajibishwe kwakuwa upotevu wa shilingi bilioni 133 katika mfuko wa EPA, ulifanyika enzi ya utawala wake.

No comments: