Tuesday, February 26, 2008

Na Erasto Stanslaus

TIMU ya Simba ya Dar es Salaam inaondoka nchini leo kwenda Ethiopia kurudiana na Awassa City ya huko, huku uongozi wa klabu hiyo ukikataa kuambatana na mkuu wa msafara aliyeteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Akizungmza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali alisema timu inatarajia kuondoka leo mchana na shirika la ndege la Ethiopia,ikiwa na msafara wa watu 26, lakini hawatakuwa tayari kuongozana na kiongozi aliyeteuliwa na TFF.

Alisema waliiandikia TFF barua mapema, kuomba kiongozi wa msafara wao awe Muhsin Said ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, lakini shirikisho hilo limewajulisha kuwa wataambatana na Teofrid Sikazwe, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, jambo alilodai hawakubaliani nalo.

"Simba na Yanga tuna itikadi zetu na watu wa kuongozana nao katika mashindano makubwa, ndio maana tukaomba tuongozane na Muhsin Said na kama hawakubali ni bora tusiende na mwakilishi yeyote wa TFF," alisema Dalali.

Dalali alisema Simba itaondoka na kikosi cha wachezaji 19 ambao ni Juma Kaseja, Nassoro Said, Ramadhani Wasso, Kelvin Yondani, Henry Joseph, George Owino, Moses Odhiambo, Mohamed Banka, Emmanuel Gabriel, Athumani Machupa, Ulimboka Mwakingwe na Deogratius Boniventure.

Wengine ni Juma Said Nyoso, Nico Nyagawa, Julius Mrope, Joseph Kaniki, Nurdin Bakari, Ramadhani Chombo na Said Sued, wakati benchi la ufundi litakuwa na Kocha Mkuu Milovan Cirkovic na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo, meneja Innocent Njovu, Idd Pazi na dkt. Lisobire Kisongo.

Viongozi watakaokuwemo ni Katibu Mwenezi wa klabu hiyo Said Rubeya 'Saydou' na kiongozi wa TFF. Simba itarudiana na Awassa mwishoni mwa wiki, ambapo mchezo wa kwanza uliofanyika wiki moja iliyopita Simba ilishinda mabao 3-0.

No comments: