Friday, October 19, 2007

Wapinzani wazushi, Butiku je?

Martin Malera
WAPINZANI wamesema, waandishi na wachambuzi wa makala wameandika juu ya kutamalaki kwa ufisadi na rushwa huku wakitolea mifano ya mikataba yenye utata kama ule wa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, kashfa ya BoT, Tangold, ANBEN, Fosnik, Daveconsult, TanPower na mkataba wa Buzwagi, lakini wote wameishia kuitwa wazushi, waongo na hata wachochezi.
Hawakuishia hapo, kwani walikwenda mbali zaidi kumtaka Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri na ikiwezekana kuvunja na kuunda upya baraza dogo, tena la wachapakazi na wenye uchungu na mali za taifa hili.
Ushauri wa kutaka Rais avunje baraza la mawaziri, aunde lenye watu wenye udhu na uchungu wa maendeleo ya taifa, ameukataa.
Ameshauriwa awawajibishe wote wanaokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu, amekataa na kuishia kuwatetea na hata kuwataka wananchi hususan wapinzani na waandishi kuacha kuwa walalamikaji, mashahidi na mahakimu wa kutoa hukumu.
Rais Kikwete ametakiwa atimize ahadi zake kama kupambana na ufisadi, madawa ya kulevya, kurekebisha mikataba ya madini, kurejesha nyumba za umma alizoahidi, na kurejesha chenji yetu ya ununuzi tuliobambikiwa wa rada, amekataa na wote waliotoa ushauri wa aina hii, wameonekana majuha wa kutupwa.
Lakini leo wazee wameamua kusema. Wazee wenye heshima ndani na nje ya CCM, wameamua kuvunja ukimya, wamepasua jipu, wamesema ukweli bila woga.
Kitu kinachozua maswali mengi kuliko majibu ni kwamba wazee hao si waropokaji kama kina Kingunge tuliowazoea, hivyo kauli zao hasa katika kipindi hiki ambapo mambo katika nchi hayaendi sawa ni nzito na zinapaswa kufanyiwa kazi.
Nawazungumzia Mkurugenzi wa Tasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Butiku na Mwinyi ni watu wenye heshima kubwa na historia katika taifa hili.
Maoni yao na ushauri wao hasilani hayawezi kuchukuliwa kama wazushi, wachochezi na hata waropokaji kama wanavyoambiwa kina Dk. Wilbrod Slaa. Lazima Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikae chini, itafakari na kukubali kwamba kuna tatizo.
Butiku, Mwinyi kama nilivyo mimi na wachambuzi wengine wanaoandika kumkosoa na kumpa ushauri, hawamchukii Rais Kikwete. Wanampenda. Ndiyo maana wamejitoa mhanga kumfikishia ujumbe huu.
Umma unalalamikia mawaziri wake kuwa baadhi ni mafisadi na matajiri wa kutupwa na hawawezi kutoa maelezo jinsi walivyochuma mali hizo. Wengine wanamiliki migodi ya madini kwa siri, na migodi hiyo inajulikana tu wanapoibiwa.
Umma unalalamikia serikali kubwa kuliko uwezo wetu kiuchumi. Wachambuzi kama kina Mpayukaji, Ansbert Ngurumo, kutaja kwa uchache, wameonya kuwa serikali hii ni mzigo kwa mlipa kodi.
Hata hivyo, mbaya zaidi, wahusika wamezidi kushindilia nta kwenye masikio huku macho yao yakipofuka yanapopambana na ukweli huu.
Badala ya kuwa na serikali inayofanana nasi, tumekuwa na serikali inayofanana nao hao wanaoshiba kwa jasho letu.
Butiku, ambaye alikuwa msaidizi wa Rais wa Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, anasema siku zote amekuwa bubu, lakini sasa amelazimika kusema baada ya kuona rushwa nchini imekuwa kama gonjwa la ukimwi na kelele zimezidi kuwa kubwa huku kukiwa na usimamizi mbovu wa maliasili za taifa na kuongezeka kwa umaskini.
Hebu soma nukuu hii ya Butiku: “Taifa zima linapiga kelele rushwa, rushwa, rushwa na labda siyo rushwa tu, ni kuuza nchi kwa fedha zinazoonekana ni nyingi sana lakini zisizojulikana zinatoka wapi.”
“Bubu ameamua kujitokeza wazi kwa sababu kelele hata rais wetu aliyechagulia miaka miwili iliyopita kwa kura nyingi sasa hivi amekuwa akipigiwa kelele, anasimamishwa njiani wananchi wanamuuliza madini, watu wanamsema waziwazi,” alisema Butiku.
Butiku anaendelea: “….Mkapa ameruhusu Ikulu kuwa mahali pa walanguzi na wanyang’anyi, hata yeye alipageuza kuwa eneo la biashara…Ikulu ni mahali patakatifu kila mtu anayeingia pale anakula bure na kulala bure, lakini sasa pamechafuka….. tushirikiane sasa kurejesha heshima, tusiogope kuwaambia viongozi ukweli, wanaoogopa ndio wabaya na Mkapa ajitokeze ajieleze wazi ni namna gani aligeuza Ikulu kuwa mahali pa walanguzi.”
Na bahati nzuri, Mkapa jana kwa mara ya kwanza tangu aanze kuvurumishiwa makombora ya kashfa, ameamua kujibu mapigo na majibu yake yanahitaji makala nzima kuijadili. Heri Butiku ameweza kutoa nyoka pangoni.
Hakuna ubishi kwamba Serikali ya CCM imeshindwa kutofautisha kati ya wema na uovu, kati ya mwenendo unaoweza kuvunja utaifa wetu, na ule unaoweza kudumisha amani na umoja wa taifa na raia zake.
Serikali imeanza kushindwa kutofautisha kati ya rafiki na adui na sasa imeanza kuachana na siri kuu ya uhai wake kuheshimu mijadala ya wazi wazi juu ya jinsi ya kuendesha na kusimamia mambo ya Watanzania.
Serikali ya CCM imeanza kujenga tabaka la viongozi wenye mali au wanaowekwa katika nafasi za uongozi na wenye mali au kwa kutumia mali zao wao wenyewe, ili wapate nafasi za kufanya mambo yao na zaidi ya yote, mali imeanza kuchukua nafasi ya uzalendo na kutumiwa na viongozi wengi wa CCM kama nyenzo ya uongozi bora wa kisasa. CCM imeanza hata kutoona haya, na viongozi wakuu, chini ya uongozi wao sasa wamenyamaza, wanaona haya kukemea uovu.
Rais Kikwete, atake asitake Serikali yake ina kasoro. Na viongozi hawana budi kukubali kuwajibika kwa wananchi kwa madhara yoyote yanayoweza kusababishwa na hali hii ya rushwa sugu.
Rushwa ni mbaya. Rushwa inayodaiwa kuwepo na inayokemewa na watu wenye udhu kama wasio na tabia ya kusema ovyo kama kina Butiku ni balaa kwa CCM na Serikali yake, na isipokuwa makini, wananchi hawatakuwa na sababu ya kusubiri mwaka 2010, kwani haitaweza kuepuka kuvunjika kutokana na dhambi ya kukiuka maadili, ahadi na kiapo chake yenyewe.
Mwinyi katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu alishauri na hapa namnukuu: "Kuna mambo mengine yanazungumzwa katika magazeti, yanakereketa, lakini (mimi) sikasiriki… na baadhi yanayokosoa yana maana na yakifanyiwa kazi yanaweza kuleta maendeleo katika nchi yetu.” Hii ni kauli nzito na uzito wake unatokana na mtu aliyeitoa, kwani Mwinyi wakati serikali yake ilipopigiwa kelele za kuwapo kwa rushwa, alivunja baraza la mawaziri.
Ili kurejesha heshima, Serikali lazima ipambane na ufisadi kwa kuwawajibisha watuhumiwa tulio nao sasa, hata kwa ushahidi wa mazinmgira tu.
Mbona Dk. Juma Ngasongwa, Idd Simba na Simon Mbilinyi waliwahi kuachia ngazi kutokana na tuhuma tu, kwanini Karamagi na wenzake wang’ang’anie? Baraza la mawaziri pia lipunguzwe.
Miiko ya uongozi irejeshwe ili viongozi waache kumiliki mali na hata kufanya biashara Ikulu, na kubwa kuliko yote ahadi ya serikali, hasa ya kutaka kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, iitimizwe, kinyume chake serikali iwajibike au isubiri wananchi wajisemee kwani hawatakuwa tayari kusubiri kuteseka hadi mwaka 2010.
Simu: 0713260071 matintz@yahoo.com

No comments: