Friday, October 19, 2007

Mkapa umekosea, amka useme na taifa

KWA muda sasa kumekuwa na tuhuma dhidi ya rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Kwanza zilianza tuhuma za kutumia vibaya madaraka wakati alipokuwa kiongozi wa juu kabisa nchini.
Inadaiwa kuwa wakati akiwa rais, Mkapa alianzisha kampuni binafsi, kuisajili na kuchukua mkopo benki.
Hizi ni shughuli ambazo watu wengi wanazifanya katika maisha ya kila siku. Lakini anapofanya mtu mwenye dhamana ya kuongoza nchi, inaleta shaka, hasa ukizingatia ukubwa wa mkopo uliochukuliwa, na kasi yake ya kulipwa.
Ni vigumu sana katika mazingira ya kibiashara ya kawaida nchini, kwa mfanyabiashara kukopa sh milioni 500, na kuzirudisha katika kipindi cha miezi kadhaa. Inapokuwa shughuli za kampuni iliyotumika kukopa na kulipa hazieleweki vema miongoni mwa wananchi, shaka inaongezeka zaidi.
Imeshaelezwa kuwa si dhambi wala kosa la jinai kuanzisha kampuni na kuitumia kampuni hiyo kukopa benki.
Ni kitu ambacho kinahimizwa kila mara, kwani ndiyo njia kuu ya kuongeza mtaji. Lakini inapofikia hatua ya rais kufanya hivyo akiwa madarakani, inaleta maswali mengi.
Wengine wanamtetea Mkapa kuwa alikuwa anajiandaa atakapostaafu asiwe katika hali mbaya kiuchumi. Lakini tuna sheria ambazo zinahakikisha kuwa viongozi wakuu wastaafu, wanatunzwa vema na serikali baada ya kustaafu.
Hivi karibuni zimeibuliwa tuhuma nyingine dhidi ya Mkapa, safari hii ni kuhusiana na jinsi alivyokiongoza Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa mwenyekiti wake wa taifa.
Tumeshawahi kusema huko nyuma kuwa kutokana na nafasi yake katika nchi, CCM ina athari kubwa kwa nchi kwa yanayotokea ndani yake. Chenyewe ndicho chama kinachotawala, kinapoharibikiwa, nchi inaharibikiwa, kwa sababu nchi inatawaliwa kutokana na sera za chama hicho.
Tuhuma kuwa uongozi wa Mkapa akiwa mwenyekiti wa CCM ulikuwa na mushkeli kiasi cha kusababisha chama hicho kupoteza dira, ni nzito.
Hili linaweza kuchukuliwa kama siasa, lakini kwa hakika si siasa, kwani kinachozungumzwa kinahusiana na hali ya taifa na mustakabali wake, kwa sababu wengi wa wanaoongoza nchi leo hii, kama si wote, wapo ndani ya CCM.
Kwa maana hiyo, iwapo ni kweli kuwa mfumo ndani ya chama hicho uliachiwa kuzaa viongozi waliopata madaraka kwa kutumia rushwa, hilo ni suala la hatari sana.
Inaweza kuwa suala hilo si sahihi, lakini ukichukulia mjadala unaoendelea sasa hivi kuhusiana na tuhuma za ufisadi, rushwa na ubadhirifu mkubwa wa mali ya taifa, ni vigumu kutoamini kuwa mfumo mbaya wa CCM kupata viongozi ndio umelifikisha taifa hapa lilipo.
Haiyumkiniki basi kwa kiongozi aliyekuwa na dhamana wakati mambo haya yanayodaiwa yakitokea, akae kimya bila kutoa maelezo yatakayowawafanya Watanzania wawe na hakika na kuwa na ufahamu wa uhalisia wa kile kinachozungumzwa hivi sasa.
Wapo baadhi ya watu walioinuka na kumtetea Mkapa, si vibaya, lakini ingekuwa vema zaidi iwapo Mkapa mwenyewe angewaeleza Watanzania, wamsikie kwa kauli yake, akitoa majibu ya tuhuma dhidi yake.
Ni yeye mwenyewe ndiye aliasisi sera ya ukweli na uwazi enzi za uongozi wake. Hatuamini kuwa alianzisha sera hiyo ili aitumie atakapokuwa katika uongozi tu.
Kama mtu aliyewahi kushika madaraka makubwa kabisa nchini, Mkapa ataendelea kuwa kiongozi wa Watanzania hadi mwisho, atake asitake. Hivyo, bado anawajibika kuitekeleza sera yake ya ukweli na uwazi.
Sisi hatutaki kuamini katika tuhuma zinazotolewa dhidi yake, lakini kwa kuangalia mambo yanayotokea na aina ya ushahidi unaotolewa, tunakuwa katika nafasi ngumu sana ya kuamua nini ukweli wa kinachosemwa.
Tunaamini kuwa Watanzania wengi wapo katika kundi hili na mtu pekee atakayewasaidia kuondoka katika hali hiyo ni Mkapa mwenyewe. Tafadhali baba, inuka useme na taifa.

No comments: