Monday, October 22, 2007

Mkapa amtesa Rais Kikwete

na Charles Mullinda
DHAMBI ya ubaguzi na kuchafuana majina iliyoibuka wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa imeanza kumwandama Rais Jakaya Kikwete.
Rais Kikwete, sasa analazimika kubeba mzigo wa tuhuma zinazodaiwa kufanywa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, wakati akiwa madarakani kwa muda wa miaka kumi.
Sasa anaonekana kuwekwa katika mtego wa kumlazimisha kuwatosa baadhi ya washirika wake wa karibu waliofanikisha ushindi wake katika uchaguzi wa 2005.
Angali bado na mzigo wa tuhuma za ufisadi zinazowaandama wasaidizi wake, Kikwete sasa ameanza kugeuziwa kibao na wana CCM wenzake kwa kumkosoa na kumtuhumu waziwazi mtangulizi wake, ‘mzee’ Mkapa, anayedaiwa alibadili kanuni za kumpata mshindi katika uchaguzi huo ili kuwezesha ushindi kwa Kikwete.
Aidha, Rais Kikwete ambaye ni mmoja wa vigogo 11 waliotajwa katika orodha ya mafisadi iliyotangazwa hivi karibuni na viongozi wa kambi ya upinzani, yuko katika hatari ya umaarufu wake kuendelea kuporomoka iwapo ataendelea na uamuzi wake wa kumkingia kifua Mkapa asijibu tuhuma zinazoelekezwa kwake.
Hatua ya hivi karibuni ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku kumshambulia Mkapa kuwa alipageuza Ikulu kuwa pango la walanguzi, inamgusa pia Rais Kikwete ambaye alikuwa mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tatu.
Butiku katika kauli yake hivi karibuni kwa waandishi wa habari alikaririwa akidai kwamba, Mkapa aliruhusu Ikulu kuwa mahali ya walanguzi na wanyang’anyi na alimtaka ajitokeze kueleza namna yeye mwenyewe alivyogeuza eneo hilo takatifu kuwa mahali pa walanguzi.
Wachambuzi wa mambo wameeleza kuwa hatua ya Butiku kuibuka na kumshambulia Mkapa hadharani huku akimtaka ajitokeza kujibu mashambulizi yake ni majibu ya kambi ya upinzani ndani ya CCM kwa tabaka la wana CCM walio madarakani ambao ushindi wao ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na siasa za ubaguzi na kuchafuana majina.
Shutuma zilizotolewa na Butiku ambaye wakati wa kampeni za kumpata mgombea urais kupitia CCM mwaka 2005 hakuwa katika kambi ya Kikwete, anasema kwamba Mkapa akiwa Mwenyekiti wa CCM, aliamua kumuengua mapema makamu wake, John Malecela, asisonge mbele katika mchakato wa kugombea kuteuliwa kuwa mgombea kupitia chama hicho.
Kwamba Mkapa alibadili kanuni kwa shinikizo na bila sababu yoyote ya msingi, ambayo awali ilijadiliwa kuwa isibadilishwe, ya mjumbe mmoja kura tatu.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai zaidi kwamba, Mkapa alibadili kanuni hiyo kwa shinikizo ili kuhakikisha Rais Kikwete anashinda na kuwa mgombea wa CCM, na kwamba, anachokifanya Kikwete kwa sasa ni kulipa fadhila kutokana na ujasiri unaodaiwa kuonyeshwa na Mkapa wa kuhakikisha kijana wake anashinda katika mchakato huo.
Butiku anayetajwa na wafuatiliaji wa masuala ya siasa kuwa anatumiwa kama chambo na wapinzani wa wanamtandao ndani ya CCM, anamtaja Mkapa kama mtu msahaulifu, ambaye wakati akiwa Ikulu, alisahau yote aliyofundishwa na Mwalimu Nyerere, akashindwa kutofautisha uongozi na kutafuta mali na kwamba wakati anatoka katika uongozi alitafuta mtu wa kumbeba na kumpeleka Ikulu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sayansi ya Jamii (FASS) aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa, ameitafsiri kauli ya Butiku kuwa moja ya matamshi mazito yanayolenga kuichafua kabisa serikali ya Kikwete kuwa iliwekwa madarakani na Mkapa kwa ajili ya kumlinda yeye na baadhi ya wenzake.
“Hii ni kauli nzito sana, inamaanisha kuwa Kikwete aliwekwa pale kwa dhumuni maalumu la kumlinda Mkapa dhidi ya madhambi aliyoyafanya wakati akiwa madarakani, kauli hizi zitamtesa sana Rais Kikwete kwa sababu zinaichafua kabisa serikali yake, hivi ndivyo ninavyoweza kuitafasiri kauli hii,” alisema mhadhiri huyo.
Kauli nyingine ya Butiku inayoonyesha kuwepo walakini katika mchakato huo inaeleza kuwa, wakiwa Dodoma kwenye uchaguzi wa kumpata mgombea wa urais kupitia CCM kulikuwa na mgombea mmoja anayedaiwa alikuwa akigawa fedha hadharani na kwamba alikuwa akiwajaza wajumbe wa mkutano huo kiasi kikubwa cha fedha.
Kwamba baada ya kusikia maneno hayo ndipo alipoondoka kwenda kumwandikia Mkapa barua ambayo hata hivyo mpaka anaondoka madarakani hakuwahi kuifanyia kazi.
Hili nalo linaelezwa kuwa ni hatua ya Mkapa kuhakikisha kuwa Kikwete anashinda katika uchaguzi huo licha ya baadhi ya wapambe wake kudaiwa kutoa fedha.
Kikwete ambaye amekwisha kutangaza kuwa kamwe hatamchunguza Mkapa dhidi ya tuhuma zinazomwandama, sasa analazimika kujiandaa kutoa ufafanuzi kwa wapiga kura dhidi ya kashfa mbali zinazoindamana Serikali ya Awamu ya Tatu, ikiwemo ile ya rada na madai ya Mkapa kufanya biashara akiwa Ikulu.
Kikwete pia anapaswa kuanza kujipanga upya kupambana na makundi ndani ya chama chake ambapo baadhi ya vigogo aliowaangusha katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005, akiwemo Malecela wanaonekana kutofautiana na msimamo wake katika kupambana na ufisadi ndani ya serikali yake.
Kauli za kumbana Kikwete zimeibuka baada ya viongozi wa kambi ya upinzani kutaja orodha ya majina ya viongozi wanaodai kuwa wanahusika na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Kundi la wana CCM walio nje ya mtandao wanaonekana kunufaika zaidi na madai haya ya wapinzani ambayo kwa kiasi kikubwa yameiweka serikali njia panda kwa kushindwa kutoa majibu ya moja kwa moja ya tuhuma hizo.
Aidha, maadhimisho ya miaka minane ya kifo cha Mwalimu Nyerere anayechukuliwa kuwa ni kielelezo cha uadilifu yametumiwa na wapinzani wa kundi la wanamtandao kuibua madai ya shutuma hizi huku wengine wakithubutu kueleza kuwa tuhuma za ufisadi zinazoiandama serikali ni mzimu wa Mwalimu Nyerere, ambaye wakati wa uhai wake aliwakataa katakata baadhi ya viongozi waliopo madarakani, akidai si waadilifu.

No comments: