Friday, October 26, 2007

Taifa lamlilia Mbatia

na Happiness Katabazi na Godfrey God
VIONGOZI wakuu wa kitaifa serikalini, wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vya siasa na wananchi wa kawaida wameshikamana kuomboleza kifo cha Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Joseph Mbatia, aliyefariki dunia juzi wilayani Njombe kwa ajali ya gari.
Vilio vya kwikwi na hali ya simanzi jana vilianikiza nyumbani kwa marehemu jijini Dar es Salaam na eneo zima la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (Terminal One), kabla, wakati na baada ya mapokezi ya mwili wa aliyekuwa naibu waziri huyo.
Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyewaongoza viongozi wakuu wote watatu wa kitaifa na mamia ya waombolezaji wengine wakiwamo makada wanawake wa Chama Cha Mapinduzi waliokuwa wamevalia mavazi rasmi ya chama hicho katika kuupokea mwili wa Mbatia.
Mwili wa kiongozi huyo aliyepata kuwa Mweka Hazina wa Taifa wa CCM, ulifikishwa uwanjani hapo majira ya saa 7:59 kwa ndege ya serikali aina ya Fokker 50, yenye namba za usajili 5H-TGH ambayo pia ilibeba mwili wa dereva wa naibu waziri huyo, Anakleti Mogella, ambaye naye alipoteza maisha katika ajali hiyo hiyo.
Ilipotua na kusimama, wahudumu walifungua mlango na aliyetangulia kushuka alikuwa ni mume wa marehemu, Dk. Joseph Mbatia, aliyekuwa ameongozana na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani, ambao waliondoka Dar es Salaam jana asubuhi na ndege hiyo kuufuata mwili huo.
Baadaye Naibu Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, alikabidhiwa bendera ya taifa, ambayo aliingia nayo ndani ya ndege na kuitumia kufunika sanduku lililokuwa na mwili wa Mbatia kabla halijateremshwa.
Sanduku hilo lilipitishwa mbele ya Rais Kikwete, Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, John Samwel Malecela na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao waliweka mikono yao juu ya jeneza hilo kama ishara ya kumwomboleza.
Aidha, baada ya kumalizika kwa tukio hilo mwili wa Mbatia uliingizwa kwenye gari maalumu la kubebea wagonjwa aina ya Land Rover Defender, lenye namba za usajili 1776 JW04, na maiti ya dereva nayo ilipakiwa kwenye gari la kubebea wagonjwa aina ya Land Rover Defender lenye namba 1744 JW04, mali ya Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, ambapo zilipelekwa kuhifadhiwa kwenye hospitali hiyo.
Muda mfupi baada ya msafara wa magari ya maiti kuondoka uwanjani hapo, viongozi wote wakuu wa kitaifa walikwenda kuwapa pole watoto wa marehemu; Philip, Yolanda, Junior na Charles, ambao walikuwa wanalia kwa uchungu kwa kuondokewa na mama yao.
Viongozi wengine waliojitokeza kuupokea mwili wa marehemu ni mawaziri na naibu mawaziri, Mnadhimu Mkuu wa (JWTZ) Meja Jenerali Abdulaman Shimbo, makatibu wakuu wa wizara mbalimbali, viongozi wa vyama, wabunge na wananchi wa kawaida.
Mara baada ya mwili kuwasili uwanjani hapo, Rais Kikwete aliwaongoza viongozi mbalimbali katika kuwashika mikono na kuwakumbatia watoto, mume na ndugu wengine wa marehemu ambao walikuwa na huzuni kubwa.
Muda wote akiwa uwanjani hapo, Yolanda, mtoto pekee wa kike wa marehemu, alikuwa akilia kwa kwikwi, huku akiwa amekumbatiwa na mtu mmoja aliyetajwa kuwa ndugu wa karibu wa familia ya Mbatia.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mwili wa marehemu kuwasili, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, alisema kuwa mwili wa marehemu ungehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo na jana jioni maombolezo yangeendelea nyumbani kwa marehemu, Oysterbay, Mtaa wa Uganda, nyumba namba 120.
Waziri Chenge alisema mwili wa marehemu utatolewa Lugalo leo saa moja asubuhi na kupelekwa nyumbani. Hata hivyo, alisema bado haijafahamika iwapo ibada ya kumwombea marehemu itafanyika kanisani au nyumbani kwa marehemu na kuongeza kuwa baada ya ibada, saa nane mchana mwili huo utapelekwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro ambako mazishi yatafanyika.
Naye Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye jana asubuhi alikwenda nyumbani kwa marehemu kabla ya kwenda kuulaki mwili wa mbunge huyo wa Viti Maalumu, alisema Ofisi ya Bunge imepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, kwa kuwa marehemu alikuwa ni kiongozi mchapakazi na hivyo kifo hicho ni pigo.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustine Mrema, ambaye naye alifika nyumbani kwa marehemu kutoa pole, alisema marehemu ni mmoja wa viongozi wanawake waadilifu na kutoa pole kwa familia kwa niaba ya chama chake.
Wakati huo huo, Mweyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amemtumia Rais Kikwete salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho.
Katika salamu hizo, Profesa Lipumba alisema alipokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbatia.
“Nilimfahamu marehemu tangu tulipokuwa wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1973-76. Toka akiwa mwanafunzi, marehemu alikuwa mchapakazi, mwenye bidii na nia ya kujiendeleza na kushirikiana na wenzake. Kama kiongozi mwanamke, alikuwa mfano mzuri kwa wanawake wengine katika nchi yetu. Na kwa kweli Watanzania tulikuwa bado hatujautumia kikamilifu uwezo wa Mbatia,” alisema.
Nao wanawake wa CHADEMA, katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Ofisa Mwandamizi Taifa Kurugenzi yya Wanawake wa chama hicho, Mary Jumbe, wamesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbatia.
Wamesema taifa limepoteza mmoja wa viongozi katika harakati za maendeleo ya jamii, jinsia na watoto na kuwa wanatoa pole kwa familia ya Mbatia na marehemu wote waliofariki kwenye ajali hiyo.
Aidha, wanawake hao wa CHADEMA wamesema wanafadhaishwa na wimbi la ajali za barabarani zinzoendelea kutokea hapa nchini.
“Wakati umefika kwa serikali kutangaza hali hii kama sehemu ya majanga yanayolikabili taifa ili mikakati madhubuti iwekwe kuzuia ongezeko la ajali ambazo zinachangia katika kuacha wanawake wengi kuwa wajane na watoto kuwa yatima,” ilisema taarifa hiyo ya CHADEMA.
Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, kwa niaba ya chama hicho, naye alituma salamu za rambirambi kwa Rais Kikwete na kuwataka watu kufahamu kuwa kuondokewa na Mbatia ni mapenzi ya Mungu.
Katibu Mkuu huyo wa CCM amekielezea kifo hicho kuwa kimeacha pengo kubwa kwa serikali, CCM na jamii kwa ujumla. Alisema marehemu atakumbukwa kwa ucheshi, uhodari wa kazi na upendo wake kwa watu.
“Mbatia alikuwa amana ya Mwenyezi Mungu, kwa chama na serikali yetu. Mungu ameichukua amana yake kutoka kwetu ili akaitumie kwa kazi nyingine. Hatuna uwezo wa kumzuia zaidi ya kumshukuru,” alisema Makamba.
Kutoka Iringa, inaripotiwa kuwa maelfu ya wananchi mkoani humo jana walijitokeza kuuaga mwili wa Mbatia, kabla ya kusafirishwa kwa ndege hadi Dar es Salaam.
Hata hivyo, wananchi hao hawakupata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kwa naibu waziri huyo na akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Said, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Bernard Nzungu, aliwaambia wananchi waliokuwa nje ya chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kuwa jambo hilo haliwezi kufanyika kutokana na ufinyu wa muda.
Mwili wa Mbatia pamoja na wa dereva wake, Anakleti Mogella, ambaye naye alifariki katika ajali hiyo, ilisafirishwa kwa ndege iliyoondoka kuelekea Dar es Salaam jana majira ya saa 6:30 mchana.
Baadhi ya viongozi waliokuwa katika msafara huo ukiongozwa na Naibu Waziri wa Tamisemi, Celina Kombanya ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Lawrance Masha na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Wengine waliokuwa katika msafara huo ni mume wa marehemu, Dk. Mbatia, mtoto wa kiume wa marehemu na baadhi ya wanafamilia. Mwakilishi wa Jeshi la Polisi Tanzania, aliyemuwakilisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema, Kamishna wa Polisi Paul Chagonja, alisema ajali zinazoendelea kutokea sehemu mbalimbali nchini zinaendelea kuwakumbusha watumia barabara kuzingatia sheria za barabarani.
Katika ajali hiyo, gari la waziri huyo aina ya Nissan Safari lenye namba za usajili T 724 AGZ, liligongana uso kwa uso na gari lenye namba T 299 AFJ aina ya Mitsubishi Fuso mali ya Jackson Kilagwa wa Rujewa, Mbeya.
Kamishna Chagonja alisema pamoja na Naibu Waziri na dereva wake kufariki papohapo, msaidizi wa dereva wa roli hilo, Castory Kilangwa, naye alifariki papo hapo.
Dereva wa lori hilo, Peter Mangula, mkazi wa Makambako, wilayani Njombe, aliyenusurika katika ajali hiyo, alitoroka baada ya ajali hiyo na Jeshi la Polisi limeahidi kumsaka mpaka apatikane.
Nicholaus Lubava na Dastun Gonze, waliokuwemo kwenye lori hilo lililokuwa limebea mbao, walijeruhiwa vibaya kwa kuvunjika miguu na mikono ambapo walipelekwa katika Hospitali ya Kibena, Njombe.

No comments: