Friday, October 26, 2007

Mkapa umevuna ulichopanda

KWA heshima na mapenzi makubwa naomba niwasiliane nawe kwa njia hii, baada ya kusema kuwa huna mpango wa kuzungumza na waandishi wa habari.
Ni kwa nia safi kama mwananchi na pia kama mwathirika wa baadhi ya mambo yanayosemwa juu yako.
Pole sana kwa kukosa tuzo ya mabilioni na heshima. Nilisoma baruapepe nyingi kwenye mtandao, watu wengi wakiomba Mungu uikose tuzo hiyo kutokana ulivyowatibua kwa kukataa kujibu tuhuma zinazokukabili.
Wakosoaji watakuwa na furaha si ya kawaida, kugundua kuwa kumbe tuhuma zako zimevuka mipaka kiasi cha wawekezaji uliokuwa ukisema wangekusifia, kuanza kuzipata na kushtuka.
Sasa hivi ungekuwa unafaidi pongezi kama Joaquim Roberto Chissano, ambaye hata akiamua kufanya biashara baada ya kutoka Ikulu, mtaji na heshima anavyo na hatalaumiwa na mtu bali kupongezwa na kuonekana kama alama ya taifa na si aibu ya taifa.
Wapo wanaokutania kuwa kama hutajitokeza uhesabiwe watapendekeza upewe tuzo ya kufanyia biashara Ikulu wewe na mkeo. .
Pia wanasema kuwa ulinzi unaopewa na Rais Jakaya Kikwete ambaye naye ni mwajiriwa wao usiuamini. Maana watu wamegeuka…wanaweza kufanya kama Zambia wakabadili katiba na kukushitaki. Je, hapa kweli utaweza kufaidi ustaafu kama unavyosema?
Mimi nikiwa mmoja wa waliokupigia kura vipindi vyote ulivyogombea na kukuweka madarakani, sikutarajia kama Rais ungeweza kutupa mgongo, hasa wakati huu ambako kuna tuhuma nyingi zinazokuhusu wewe, mkeo, mwanao na vivyele vyako ambako majibu yako ni muhimu kuliko wakati wowote.
Wewe si wa kwanza kutuhumiwa. Mwalimu alituhumiwa akajibu tena bila kusukumwasukumwa au kusemwasemwa.
Nafanya hivi ili kwanza licha ya kuepuka heshima yako kuporomoka, kuepusha aibu kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekufichua ulikokuwa na kukunadi nchi nzima huku akisengenywa kuwa anataka kuweka ‘kinyago chake cha mpapure’ ndani ya Ikulu.
Pia nakufahamu kama mtu mwenye kujaaliwa kipawa cha kujenga na kujibu hoja - Wazungu huita ‘gift of gab’. Kwa kujua hili, wengi wanashangaa inakuwaje unaamua kuwadharau kwanza, wananchi waliokuchagua, wakakulipa mshahara na marupurupu kwa kodi zao, na pili Mwalimu Nyerere na tatu kuruhusu jina lako liingie kwenye jinai na mambo machafu wakati uliingia madarakani ukiwa Mr. Clean?
Sikuamini kuwa ungefikia kiwango hicho. Maana nakumbuka kwenye kumbukumbu ya Mwalimu sikukusikia hata ukitoa salamu kwa taifa au chama kwa msiba huu ambao kila mwaka tulikubaliana uwe unaadhimishwa.
Nakumbuka uliahidi tena mbele ya kaburi lake ungemuenzi Mwalimu hadi watu wakasema ulizungumza na maiti!
Pia nilishangaa kusikia kuwa ulipokea barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku, aliyekuwa katibu wa Mwalimu kwa miaka arobaini na anayekujua vilivyo. Anasema hukumjibu. Na hilo nadhani unalijua fika.
Mheshimiwa hivi njia uliyotumia ya kutoa kisingizio cha kustaafu hivyo huwezi kujibu hoja unajua ubaya na madhara yake? Kwanza watu wameshaanza kusema eti unastaafu vibaya. Kwani wanasema unatumia pesa za wananchi kwa kukulipa pesa ya ustaafu wakati ukweli ni kwamba unalipwa kwa kufanya biashara zako na familia na marafiki zako ukiwa Ikulu. Huu waweza kuwa umbea.
Lakini utaishia kuwa ukweli kama utashikilia msimamo huo wa kusema hutaki kuingizwa kwenye siasa. Kujibu si siasa bali ni wajibu. Utaingiaje kwenye siasa wakati hugombei cheo chochote. Utaingiaje kwenye siasa wakati wanaokutaka ufanye hivyo si wapinzani bali ni wana-CCM wenzako safi?
Kama washauri wako wanakuhadaa kuwa hiyo ndiyo njia salama, watimue. Maana wanaodai maelezo ni wananchi ambao Ikulu wanayosema ulitumia kufanya biashara na kuibuka na makampuni kama ANBEN, TanPower, Fosnik na mengine ambayo hayajaanikwa ni wao, ni mali yao na Rais ni mpangaji wa muda tu.
Pia ningeshauri ufikirie upya. Leo wewe unaweza kuwakomalia na kuwadharau kiasi cha kuwapandisha hasira wakaamua kumshitaki mke, mtoto wako, vivyele vyako na marafiki zako tunaoambiwa ni wabia katika TanPower.
Wewe unaweza kuhadaliwa na kinga (immunity). Je, hao nao wana kinga gani? Kwa vile si Rais tena, huwezi kuwakingia kifua. Hata Rais anaweza asifanikiwe kama wananchi wataamua. Maana Walatini husema ‘vox populi vox Dei’.
Pia nikushauri tena. Madai ya kuwa uliifanya Ikulu sehemu ya biashara ukipingana na maneno yako na ya Mwalimu aliyesema ni patakatifu yalikuwa yanaonekana kutokuwa na nguvu yalipokuwa yameshupaliwa na wapinzani mliozoea kuwageuza kama bata anyapo kuku…
Sasa mambo yamebadilika. Wanaosema hivyo ni watu na heshima na usafi kuliko mtu yeyote katika nchi yetu.
Wale wanaokudanganya kuwa usijibu wanakudanganya sana.
Maana umma kwanza umebadilika unaweza kuamua kuchukua hatua hata tukaumbuana na kuishia kwenye vurugu. Nasisitiza usimtegemee sana Rais. Huoni naye wanavyozidi kumsakama sakama. Hawa si wa mwaka 47. Kumbuka Zambia walivyobadili katiba na kuondoa kinga na Frederick Chiluba na sasa yuko matatani.
Pia ufahamu kuwa umma kwa ulivyoamka unaweza kupata nguvu na sababu kutokana na uzito wanaokutaka ujitokeze uhesabiwe.
Haya yaliwahi kutokea Romania, Iran, Indonesia, Peru, Ufilipino nchi jirani ya DRC na dikteta Joseph Desire Mobutu jinsi kondoo walivyomgeuka na kuwa fisi walipopata kiongozi wa kumpinga.
Nani aliyekuwa anaogopewa kama Ferdinand Marcos, Mobutu au Albert Fujimori kule Peru? Leo Rais wa zamani wa Ufilipini, Joseph Estrada, anatumikia kifungo cha maisha kwa tuhuma kama hizi hizi zinazokukabili. Na alikuwa akidhani kinga ya urais ingemsadia lakini wananchi walivyoamua waliiondoa kinga.
Ni vizuri kuwa kinga ya urais inatokana na wananchi si ujanja wala utashi wa mtawala. Wanaweza kuandamana na kushinikiza itolewe kama ilivyofanyika Zambia na mambo yakawa mabaya.
Kitu kingine unachopaswa kufahamu ni kuwa Mwalimu bado ana nguvu sana hata kama ameshakufa ingawa ‘the dead tell no story’ ila si kwa Mwalimu. Hili unalifahamu sana.
Pia inabidi ufahamu kuwa kwa wanasheria kukaa kimya si kukiri. Lakini kwa umma inatosha kupitisha hukumu.
Mimi ningeshauri ujitokeze ukiri na kuomba msamaha yaishe. Maana Watanzania wanajulikana kwa ukarimu na huruma yao.
Leo unaweza kushupaa usijue kitakachotokea kesho. Hebu angalia mawaziri wazima wanavyozomewa mikoani kutokana na kwenda kutetea haya haya! Wengine wamefikia hata kuchoma majumba na kuwatimua wataalamu wanaoona ni longo longo.
Ukiondoa wazee wetu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki ambao unajua jinsi mlivyowazungusha, wazee wanaostaafu mara nyingi wanapaswa kufaidi matunda ya kazi zao.
Lakini inakuwa vigumu kufaidi matunda yatokanayo na tuhuma za wizi kama hutajibu. Kama utaendelea na msimamo huu hatari usishangae ukaja kunyooshewa kidole mbele ya umma kwa dharau bila kujali uliwahi kuwa rais tena kwa miaka kumi.
Sababu au jibu ulilotoa kama litakuwa ndiyo msimamo wako ni jepesi na linaonyesha kuwa unawadharau wananchi au kujiona mjanja kwa sababu umeishajipatia mradi wako. Ukiendelea kupuuza na kudharau nao watakudharau lakini hawatapuuza patilizi.
Je, uhitaji kuheshimika kama mzee msataafu na kiongozi wa nchi? Wanauliza huruma kwa wenye ukimwi inatoka wapi iwapo umaskini na ujinga vitokanavyo na ubinafsishaji wa wizi ni mama wa maafa ya ukimwi? Wanasema watendee haki kwanza si ujifiche kwenye ukimwi. Wameshachoka na miradi kama hii ambayo mara nyingi ni ulaji wa wajanja.
Pia ukiendelea kukataa kutoa maelezo umbea kuwa wewe ni mbishi, kiburi hata haambiliki utaota mizizi. Wewe kwa umri wako unaweza usione madhara ya hali hii. Lakini watoto wako na wajukuu wanaweza kuonja ‘joto ya jiwe’ kama ilivyotokea huko Ethiopia kwa jamaa wa mfalme Haile Selassie ilipobainika kuwa kumbe wakati akionekana kung’ara juu alikuwa katili kiasi cha kufuga simba wakila vinono huku waethiopia wakiteketea kwa njaa.
Pia ilimkumba Mangistu Hale Mariam naye aliyeonekana kupenda kutumia kodi za wananchi kutanua huku wananchi wakiteketea. Sasa ndugu zake wanalipa.
Wananchi wanawafahamu ndugu zako hata wa mkeo. Hivyo kama utawaacha watu wajitafutie majibu ujue mengine huko tuendako si mazuri.
Watu wanashangaa ulivyoweza kutaja mali zako bila kulazimishwa au kuzuga kama waliopo sasa lakini ukashindwa kuwatajia unaondoka na kiasi gani ili walinganishe na kutathmini uadilifu na utajiri wako? Wapo wanaosema usingefanya hivyo kwa sababu wakati ukitaja mali zako ANBEN, TanPower na Fosnik hukuwa umevitaja wala hukuwa navyo.
Je, hii ni kweli mheshimiwa? Na kama ni kweli unatarajia yafanye biashara na nani iwapo walaji ni hao hao wananchi au taasisi zao kama vile nilivyosikia TanPower itakuwa ikiiuzia umeme Tanesco hii ya wananchi wale wale ambao pia ndiyo walaji wa umeme huo. Wanaweza kuisusa nchi ikaingia majaribuni.
Chonde chonde tusiifikishe nchi huko. Yaliyopo yanatosha.
Pia ungeamua kujibu maana huishi kisiwani peke yako. Na hata kama unaamini kuwa wapinzani ndio wanaokuchokonoa lakini ujue kuwa wananchi ‘walivyopigika’ wakizidi kusikia una mabilioni ya pesa wewe, mkeo, ndugu na marafiki zako watazidi kukuchukia hata kuthubutu kutaka wakuadhibu kwa wanavyojua.
Tumalizie kwa kukusisitizia kuwa wazee wenye heshima kama Ali Hassan Mwinyi, Joseph Butiku na sasa Makamu Mwenyekiti wa CCM, John Malecela, si wa kupuuzia. Pia hatujui ni wangapi watajitokeza kuongezea mapigo. Na hujui watazidi kupata kuungwa mkono kiasi gani.
Na kumbuka kuna kipindi watu walisema wewe ni mbabe. Uzushi huu utakamilika ukiendelea kushikilia msimamo huo unaoonekana kama visingizio, utawaudhi wengi kiasi cha watu niliokutajia wenye heshima nao kuamua kulinda heshima zao na nchi yao kwa kuwahimiza wananchi wakukabili.
Nimalizie kwa kukushauri ujikumbushe yaliyowakuta watu kama Chiluba yalipoanza kama haya akapuuza hata kutukana. Wako wapi na katika hali gani sasa. Mwisho nishauri kuwa kukwepa tatizo si kulitatua bali kuliahirisha na kuliacha lizaliane.
Si njia ya busara wala salama hakika.
Nisikuchoshe. Ulitufundisha uwazi na ukweli. Tunatarajia wewe uwe mwalimu pia katika kuutekeleza badala ya kuuimba. Mdharau mwimba…Mimi simo.
Wako mtiifu - Al Maarufu.
nkwazigatsha@yahoo.com

No comments: