Friday, October 26, 2007

CCM; hayo yote yana mwisho

Samson Mwigamba
KWA wasomaji wangu wapendwa, leo naanza kwa kuwashukuru sana kwa kunisoma, na nawashukuru sana wale ambao wamekuwa wakinitumia salamu za pongezi kwa e-mail, ujumbe mfupi na hata wengine kwa kunipigia simu.
Mwanzoni nilijiwekea utaratibu wa kumjibu kila aliyewasiliana nami na kumpa shukrani zangu kwa njia ile ile aliyoitumia. Nimekuja kugundua kwamba inaniwia vigumu kuwasiliana nanyi nyote kwa jinsi mlivyo wengi na pia nitakuwa sijawatendea haki wasomaji wanaoshindwa kuwasiliana nami kwa sababu mbalimbali.
Hivyo naomba sasa niwe nawashukuru kwa pamoja kwa njia hii.
Kwa wasomaji wa vitabu, watakumbuka maneno haya yanayobeba kichwa cha makala hii.
Ni maneno yaliyobeba ujumbe mzito ulio kwenye kitabu cha Kuli kilichoandikwa na Ndugu Haji. Katika kitabu hicho, tunamwona Kuli (mbeba mizigo bandarini) akichoshwa na manyanyaso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa wakoloni kiasi cha kufikia kutamka kwamba “yana mwisho haya”.
Baada ya miaka kadhaa, ukoloni ulikoma. Nchi ikapata uhuru na wananchi wote bila kujali rangi, kabila, hali ya uchumi, n.k, wakawa huru ndani ya nchi yao. Manyanyaso yakawa yamefikia mwisho kama alivyotamka Kuli.
Imekuwa kawaida sasa kwa Rais Kikwete kutoa kauli za ajabu akiwa nje ya nchi. Kauli zinazozidi kumfunua na kumwonyesha jinsi alivyo.
Baada ya wiki kadhaa kukiri akiwa Ufaransa kwamba hajui umaskini wa Watanzania unatokana na nini hasa, wiki iliyopita ameibuka na kauli nyingine akiwa Italia na kudai kwamba, “Kelele za wapinzani hazimsumbui, hazimnyimi usingizi.” Vyombo vya habari pia vilimkariri akisema atakapoona wanaleta uchochezi, atachukua hatua.
Hii ni kauli ya jeuri, dharau na kejeli kwa Watanzania. Nitafafanua.
Kwanza, tujiulize, anaowaita “wapinzani” Rais Kikwete ni kina nani? Ni Dk. Slaa na mwanasheria Tundu Lissu? Ni Mrema, Mbowe, Lipumba na Mbatia? Ni Zitto Kabwe, Polisya Mwaiseje, na Wilfred Rwakatare?
Ni viongozi wote wa vyama vinavyojulikana kama vya upinzani na wanachama wao wote? Ni Joseph Butiku, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Makamu wake John Samwel Malecela na sasa Dk. Mohamed Gharib Bilal?
Ni baadhi ya wajumbe wa NEC ya CCM kama Makongoro Nyerere ambaye imeandikwa kwenye Mwanahalisi ya Oktoba 17, 2007, kwamba aliuliza kwenye kikao alichokuwa akikiongoza Kikwete mwenyewe kwa nini watuhumiwa wa ufisadi wasiachie ngazi na nafasi zao kuchukuliwa na watu wengine waadilifu ambao wako wengi tu (kama alivyopata kusema baba yake, Mwalimu Nyerere)?
Je, ni wanachama wa kawaida wa CCM ambao nao wanalalamikia hali ya mambo ndani ya serikali yao na ndani ya chama chao? Au ni Watanzania wote wanaolalamika kwa jinsi wanavyoona nchi ikiuzwa kwa bei ya reja reja? Au ni wote niliowataja hapo juu?
Upinzani ni hali ya kutokukubaliana. Ni kuwa katika upande wa pili ukitofautiana na upande mwingine katika jambo lolote. Ni kutoa maoni tofauti na ya mwenzako katika jambo lolote.
Hivyo wapinzani wa Kikwete ni Watanzania na wasio Watanzania wote wasiokubaliana na namna anavyoendesha nchi hii ambayo tayari amekiri kwamba hana uwezo wa kuiongoza kama rais maana hajui umaskini wake unasababishwa na nini.
Kazi kubwa tuliyomkabidhi wakati anachaguliwa kuwa rais wa nchi yetu ilikuwa ni kutuongoza katika kuachana na umaskini na kuyafikia maisha bora kwa kila Mtanzania.
Ikiwa hajui umaskini wetu unasababishwa na nini, basi hawezi kuuondoa na kutuletea maisha bora na hivyo hastahili kuendelea kuwa rais wa nchi hii.
Miongoni mwa wapinzani wa Kikwete ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye ametaka tuhuma za rushwa zilizotangazwa na Dk. Slaa zisipuuzwe.
Kwa Kikwete kuziita tuhuma hizo kelele za wapinzani, tayari amezipuuza na kupingana na Mzee Mwinyi.
Wapo pia viongozi wa muda mrefu ndani ya CCM walioshika nafasi kubwa kwenye CCM na Serikali kama Joseph Butiku, John Malecela na Dk. Mohamed Gharib Bilal ambao wote wanataka walioshutumiwa wajiuzulu ama wasimamishwe uongozi hadi hapo uchunguzi huru utakapokamilika.
Lakini Kikwete anasema hizo ni kelele za wapinzani. Pia wamo wananchi wengi wa taifa hili ambao wananung’unika kila kona kwa jinsi CCM na Serikali yake ilivyouza rasilimali za nchi yao na kujineemesha wao na familia zao pamoja na wageni waliokula nao. Wote hao ni wapinzani wa Kikwete.
Na naomba nimweleze Mheshimiwa Rais kwa uwazi wote bila kuficha wala kuzunguka, akiniita mchochezi sawa, kwamba nimekutana na wananchi wengi tu ambao wanajuta kwa nini walimpigia Kikwete kura.
Mpinzani mwingine mkubwa wa Kikwete ni marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Huyu amekufa lakini hotuba na maandishi yake yote yanapingana na jinsi Kikwete anavyoendesha nchi sasa hivi na hivyo anampinga. Naamini Nyerere angekuwa hai mojawapo ya mambo yafuatayo yangetokea:
Aidha, angesimama kidete na kuyapinga mambo haya ndani ya vikao vya Chama Cha Mapinduzi na hivyo yasingefanyika. Au angefanya kila liwezekanalo kuhakikisha viongozi waliokuwa wanawania kwenda Ikulu wakati hawajui kile kinachowapeleka huko watakitekeleza vipi, hawaupati huo uongozi. Au angekihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na CHADEMA.
Siku Chama Cha Mapinduzi kilipokuwa kinamuaga mzee Kawawa (alipostaafu rasmi siasa za majukwaani), katika hotuba ya shukrani alisema, pamoja na mambo mengine: ‘Naahidi nitakufa nikiwa mwanachama mwaminifu wa CCM.’
Ilipofika zamu ya Mwalimu Nyerere kuzungumza, akasema: ‘Rashid una roho ngumu. Utakufa mwanachama mwaminifu wa CCM? Mimi siwezi kuyasema haya. CCM inaweza kubadilika. Siku ikiacha misingi, nami naachana nayo, kwa sababu CCM si mama yangu. Ninaye mama mmoja na siwezi kupata mwingine...’
Na wakati tunaelekea kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, Mwalimu aliandika kitabu kilichoitwa “Uongozi wetu na hatima ya Tanzania”
Ndani ya kitabu kile kuna mahali Mwalimu anasema alitamani kuwepo chama kingine cha upinzani chenye nguvu ili kichukue nafasi ya CCM na kuing’oa madarakani.
Alipoulizwa na waandishi wa habari siku moja kwamba ni chama gani mbadala ambacho aliona kingefaa kuja kuongoza taifa hili baadaye aliitaja CHADEMA.
Sina uhakika kama Rais Kikwete aliwatambua wapinzani wake wote wakati akisema kelele zao hazimsumbui.
Nadhani hakujua kama anawakejeli Watanzania wengi sana wanaopingana na hali ya mambo katika nchi hii na jinsi serikali inavyoendeshwa kinamna.
Na kama alijua, basi ilitokana na jeuri, dharau na kejeli kwa Watanzania. Jeuri hii, kiburi hiki na dharau hii inatoka wapi?
Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge alinukuliwa na gazeti la Mwananchi toleo la Oktoba 04, 2007 akisema huko Musoma kwamba wananchi wasubiri tu ikifika mwaka 2010 wataona jinsi barabara zitakavyojengwa.
Kauli hii kwa maoni yangu, kwa jinsi alivyonukuliwa, aliitoa kwa hasira baada ya kuwa yeye na mwenzake, Deodalus Kamara wamezomewa na wananchi kwa kushindwa kujibu tuhuma za wananchi kwa serikali yao.
Katika kukasirika waziri alijikuta akitoboa siri yao ya ushindi. Kwa maoni yangu ni kama alikuwa akiwaambia wananchi: “Hata mtuzomee, uchaguzi mkuu ujao tutashinda tu. Subirini 2010 tutakavyojenga barabara na kuwaonyesha, mtatupatia tu kura”.
Hii ndiyo dharau ya CCM, Watanzania wenzangu. Kwamba wanatunyanyasa wananchi, maisha magumu, wao wananeemeka.
Tukikaribia uchaguzi mkuu, wanafanya kitu kimoja au viwili vizuri, wanatuonyesha “angalieni mafanikio ya CCM, tupeni kura tuendelee kuwaletea maendeleo. Tunawapa ushindi wa “kishindo”, “kimbunga” au “tsunami”.
Wanatudharau na ndiyo maana malalamiko yetu ya msingi juu ya ufisadi unaoendelea ndani ya serilkali na mikataba mibovu inayotuumiza wananchi wanaiita kelele za wapinzani.
Sasa wakati umefika. Wakati wa kuwaonyesha kwamba Watanzania si mbumbumbu tena.
Tunajua tunachokifanya. Tulikuamini Kikwete lakini ukatuona malofa tusiojua kitu. Ukadhani unaweza ukafanya maajabu Ikulu halafu uchaguzi unaofuata tunakupatia kura. Umekosea.
Natoa wito kwa Watanzania wa kada zote. Tukatae utawala wa kiaina. Tumwambie Rais Kikwete, “Yana mwisho haya” na 2010 tuachane naye.
Tukatae kudanganywa kama watoto. Miaka yote tunapatishwa taabu halafu karibu na uchaguzi ndiyo tunapewa “pipi” kama watoto.
Walifanya hivyo kwa kufuta kodi ya maendeleao wakati tunakaribia uchaguzi. Wakaleta mikopo ya elimu ya juu kwa kila mwanafunzi tena kwa asilimia mia moja wakati tunakaribia uchaguzi wa 2005. Baadhi ya wanafunzi wakajichotea mara mbili mbili bila kuulizwa.
Walipochaguliwa tu, wakapunguza mikopo hadi asilimia 60, tena kwa waliopata madaraja maalumu tu. Leo wanafunzi wanakopeshwa kwa viwango ambavyo hakuna duniani pote.
Tulipokaribia uchaguzi wa 2005 walitudanganya kwamba kufikia 2006 Mtanzania atasafiri kwa teksi kutoka Mtukula (mpaka wa Tanzania na Uganda) - Mwanza - Dar es Salaam – Mtwara, maana itakuwa ni lami tupu. Leo wanasema tusubiri 2010!
Mwaka wa uchaguzi. Watudanganye tena tuwape kura. Tuwaambie hapana. Tuwanyime kura 2010.
smwigamba@yahoo.com0784 815499 au 0712 012514

No comments: