Friday, October 26, 2007

Kwa nini tuzungushane, Kikwete naye si safi?

M. M. Mwanakijiji
HIVI kwa nini anayechezea uchafu na yeye asichafuke? Itakuwaje mtu anayelinda uchafu aitwe msafi? Hivi kanuni ya kwanza ya uchafu haijulikani kwa watu wengi kuwa mwenye kukumbatia uchafu, na yeye huchafuka?
Ni wazi kuwa kuna tofauti ya aliyesababisha uchafu na yule ambaye ameuona uchafu lakini akauvumilia na kuitia marashi ili unukie!
Aliyesababisha uchafu ndiye aliyechafua hasa, lakini aliyenyunyizia marashi kuficha uchafu huyo naye ni mchafuzi wa hali ya juu, kwani uchafu unaponuka husababisha watu watake kusafisha lakini anayefukizia ubani uchafu anahatarisha maisha kwani watu hawatajua kuna kitu kichafu karibu!
Katika madai ya watu 11 waliotajwa katika orodha ile ya uchafu, jina mojawapo linaonekana kuwagawa wanaharakati. Kuna wale wanaosema kuwa kumjumuisha Rais Kikwete (kwa mambo aliyoyafanya akiwa waziri) ni kumbana mikono, kwani kama na yeye yumo kwenye orodha hiyo ataweza vipi kuwachukulia hatua wengine?
Na wapo wale wanaosema chepeo huitwa chepeo na si kijiko japo vyafanana. Kama Rais Kikwete asingevumilia uchafu huko nyuma (na sehemu nyingine kusababisha uchafu huo), basi asingejumuishwa katika orodha hiyo.
Binafsi naamini kabisa kuwa hakuna mtu yeyote katika Tanzania ambaye yuko katika utumishi wa umma ambaye akichafua hastahili kuambiwa kachafua na akiboronga basi asiambiwe kaboronga.
Yale mambo ya kuwa mzee “akichafua hewa” basi alaumiwe mtoto yamepitwa na wakati, hasa kwenye masuala yanayohusu maslahi na mustakabali wa taifa letu. Mkubwa akichafua hewa vidole vitaelekezwa kwake, na awe muungwana kukiri na kuomba radhi! Tusiwatwishe wafanyakazi wa chini mizigo iliyotengenezwa na wakubwa!
Nidhamu ya woga ya kutowaambia wakubwa ukweli na badala yake kuwapigia makofi na kuwaimbia nyimbo za shangwe wakati tunajua wamevurunda ni unafiki wa hali ya juu, usiostahili nchi yetu.
Kama Karamagi kaboronga tutamwambia, kama Lowassa kaboronga tutamwambia, na kama Rais kaboronga na yeye ataambiwa, kwani haogopwi mtu, hapendwi mtu na hapendelewi mtu, kinachopendwa ni Tanzania na Tanzania peke yake.
Swali kubwa linalotukabili ni kuwa je, Kikwete ni msafi wa kutosha kuweza kusafisha uchafu wa watu wengine katika serikali yetu? Je, Kikwete anaposema kuwa atashughulikia wala rushwa mbona hazungumzii ufisadi mwingine?
Kwa nini msisitizo uko kwenye kutoa na kupokea rushwa tu wakati kuna mambo mengine ambayo viongozi wetu kadhaa wamejihusisha nayo; mambo kama matumizi mabaya ya ofisi, ubadhirifu, unyanyasaji, kutumia vibaya mali za serikali n.k Ni kwa nini Rais Kikwete anataka kushughulikia rushwa tu? Je, yawezekana kuwa kutoa na kupokea rushwa ni dalili tu ya matatizo makubwa zaidi katika jamii yetu na katika vyombo vyetu vya serikali?
Nilichoamua kufanya leo ni kusema kuwa Rais Kikwete hawezi kupigana na ufisadi nchini hata kama angetaka na hata kama watu wanaombea atake. Anaweza kupigana na vitendo vya rushwa kwa kiasi Fulani, lakini matumizi mabaya ya madaraka, vyeo au vitu vya namna hiyo hawezi kuthubutu kugusa maeneo hayo kwani kile kinachomla ‘ki nguoni mwake’ mwenyewe na atakuwa ni mtu jasiri atakayeweza kuwanyoshea vidole wengine bila yeye mwenye kujinyooshea kidole.
Mkataba wa IPTL ulisainiwa na yeye akiwa Waziri wa Nishati na Madini. Hakuna mkataba mbovu kama huo. Kushindwa kwake kutetea maslahi ya nchi akiwa waziri na kulisababishia taifa hasara kubwa ilikuwa ni kilele cha kutokuwajibika na kushindwa kuongoza.
Akiwa waziri mwenye dhamana ya nishati, Kikwete alitakiwa kuhakikisha kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano inaingia kwenye mikataba inayoweza kujitoa pasipo kupata adhabu kubwa. Alishindwa hivyo na hivyo kuoneshe kutokuweza kusimamia maslahi ya nchi.
Wakati rada ya bilioni 50 inanunuliwa, Kikwete alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa, na wakati sakata lenyewe linaanza alikuwa ni Waziri wa Fedha. Akiwa waziri mwenye dhamana hiyo alishindwa kabisa kufuatilia ukweli kuwa kampuni ya BAE si mali ya serikali ya Uingereza na ya kuwa rada yenyewe ilikuwa imeongezwa kwa asilimia 24.
Kiasi hicho kinakaribiana kabisa na wastani wa asilimia 20 za fedha za umma zinazopotea katika manunuzi ya serikali (public procurement).
Alishindwa kuhakikisha kuwa maslahi ya taifa letu yanalindwa na alipopata nafasi ya kuonyesha busara aling’aka na kusema “kwa nini sisi ni idara ya Benki ya Dunia? Ni kututukana kudai kuwa tusubiri Benki ya Dunia kutuamulia nini kinatufaa”.
Ndio maana leo hii anapokuja na kuzungumza kuwa hawezi kuamini kuwa nchi kama Uingereza inaweza kuacha kampuni ‘yake’ kurusha rada hiyo kwa bei hiyo, wengine tunamshangaa kwani alikuwa na nafasi zaidi ya 20 ya kuweza kupinga ununuzi huo lakini alikuwa ni kinara wa kutetea tenda hiyo ya rushwa!
Ni kuelewa hilo ndio utaona ni kwa nini hakutaka watu wamuulize Rais Mkapa juu ya suala la rada, kwani miongoni mwa wahusika wakubwa ni yeye mwenyewe Kikwete.
Kama nilivyoonyesha hapo juu kuwa Rais Kikwete aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini. Kwa hivyo nina uhakika kabisa alikuwa anajua kabisa jinsi mikataba inavyoingiwa na alikuwa na kila sababu ya kuhakikisha kuwa mikataba inalinda maslahi ya nchi na kunufaisha nchi wakati inawapatia wawekezaji faida ya kibiashara.
Kwa kitendo chake yeye mwenyewe kuwa ukaribu na wafanyabiashara hao hasa swahiba wake ambaye ni mmiliki mkubwa wa ardhi yenye vito na madini, James Sinclair, Rais Kikwete tangu akiwa Waziri wa Nishati na Madini na baadaye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje amekuwa mtu aliyetiwa upofu na ‘dhahabu’.
Wakati Rais Mkapa na Yona wanajipatia tenda ya Kiwira, Rais Kikwete na Msabaha walikuwa wanajisogeza karibu na Kampuni ya Tanzania Royalty Exploration.
Kampuni hiyo ya TRE iliingia mkataba na Barrick Gold wakati wa kuanzishwa kwake na sehemu ya mkataba huo inaipa upendeleo wa aina fulani Barrick katika ugunduzi unaofanywa na TRE.
Ni wao TRE walioiuza Buzwagi kwa Barrick na maeneo mengine kadhaa ya uchimbaji kwa makampuni mengine. TRE inaponufaika kwa mikataba mibovu ambayo serikali inaingia na makampuni ya uchimbaji kuna Watanzania nao wanaonufaika (miongoni mwao vigogo wa serikali) na ‘dili’ hizo.
Hivi kweli mnafikiri kati ya mawaziri wote 60 hakuna walio na hisa katika makampuni ya madini au makampuni ambayo majukumu yao yanawalazimisha kuyatolea maamuzi? Kama Daniel Yona aliweza kuwa na hisa katika kampuni ya Kiwira ni kitu gani kinawazuia mawaziri na watendaji wengine wasiwe nazo?
Kama Rais Mkapa aliweza kufungua ‘kiosk’ chake cha ujasiriamali akitumia anuani ya Ikulu kama ofisi yake, ni kitu gani kitakachowazuia mawaziri, makatibu, wakuu wa mikoa n.k kutumia ofisi zao kufanya biashara zao? Jibu ni hakuna, tofauti ni kuwa hawa wengine wakibambwa wanaweza kuishia ‘Keko’ ila Mkapa akifanya hivyo tunaambiwa analindwa na katiba na ‘ameachana na siasa’.
Ndio maana hadi leo hii si kweli kuwa kupitia vipengele na kuzungumza na ‘wakubwa’ hao kuhusu mikataba kumekoma kama alivyodai mjasiriamali mwingine, Nazir Karamagi, alipokuwa akijaribu kupangua bungeni hoja za Kabwe Zitto.
Ukweli ni kwamba kamba ya kujinyongea waliitundika wenyewe serikali na ni wenyewe walioziweka shingo zao humo! wawekezaji wanatishia kuondoa kigoda tu! Serikali inabembeleza!!
Anapozungumzia matatizo ya mikataba, Rais Kikwete anazungumzia kana kwamba tatizo ni kipengele kimoja tu! Hajachukua muda kufuatilia uzito wa hoja hizo kwani kwake ni kelele!
Tatizo la mikataba si kipengele cha kodi tu, akitaka kujua zaidi amuite Lissu atamsaidia kuelewa maana wasaidizi wake hawamwambii ukweli kwani ‘ukila na kipofu usimguse mkono’.
Kikwete si safi. Amewalinda watu wachafu! Waswahili walisema ukiwa na urafiki na wezi, usishangae watu wakakuhisi na wewe kuwa mwizi! Rais Kikwete anapomlinda mjasiriamali Mkapa kwamba asihojiwe kuhusu rada na biashara zake za ‘Ikulu’ na aliposhindwa kumsimamisha kazi mara moja Ditopile mara tuhuma za mauaji zilipojulikana na kuamua kumwacha ajiuzulu ili aendelee kupata mafao yake kana kwamba asingejiuzulu angeendelea kuwa mkuu wa mkoa alionyesha udhaifu mkubwa wa uongozi!
Hicho ndicho kilichomfanya Ka’Dito kwenda kututukania wake zetu jukwaani na hakuna kiongozi wa CCM aliyenyoosha kidole kuonyesha kukerwa na kitendo hicho! Labda hiyo ndiyo zawadi ya kuwa ‘Best Man wa Mkuu’!
Rais Kikwete amekuwa mpigwa mkwara mkuu wa nchi! Amekuwa akikesha kutoa vitisho hewa akijaribu kutetemesha mabua na kuangusha vichuguu huku milima ikiendelea kuganda theluji!
Ukimya wake kama ule wa Mkapa ni ishara wazi kuwa walifeli darasa la Mwalimu! Mwalimu hakuwahi kupuuzia hoja ambazo zinaweza kugawa nchi, na wazo kuwa hoja nzito “ni kelele tu” sidhani kama limewahi kutamkwa hadharani na Mwalimu.
Leo hii mawaziri na watendaji wengine na wenyewe hawachoki kupiga mikwara kwenye ofisi zao, kwani wanajua “kama alivyo baba, ndivyo alivyo mwana”.
Leo hii, tena ugenini, anadiriki kukiri kuwa madai ya ubadhirifu Benki Kuu, matumizi mabaya ya madaraka ya kina Mkapa, na Yona, ubadhirifu, rushwa n.k kuwa ni ‘kelele za upinzani’ na kuwa ‘ndiyo demokrasia ya vyama vingi’ anaonyesha udhaifu mkubwa usiomstahili kiongozi wa nchi.
Haiwezekani upotevu wa mabilioni ya fedha na matumizi mabaya ya madaraka kuwa viwe ni ‘kelele’ tu! Rais lazima awe wa kwanza kutokuvumilia uzembe, wa mwisho kuzawadia ufisadi, na asiwepo kabisa miongoni mwa wanaochukulia kero za wananchi kuwa ni kelele!
Rais ni lazima awe mtu ambaye hapuuzii masuala mazito ya kitaifa na hayafanyi kuwa ni ya kijinga. Kwa mtu kuwa mpinzani hakuifanyi hoja yake kuwa ‘kelele’ na haimfanyi yeye mwenyewe Mtanzania-Nusu. Leo hii wana-CCM wenzake wanazungumza wazi kuhusu tuhuma hizi na kudai kuwa wanaotuhumiwa (akiwamo yeye mwenyewe) wajibu si suala la kupuuzia! Butiku na Bilali siyo wapinzani hao!
Rais Kikwete ameonyesha na anaendelea kuonyesha udhaifu mkubwa wa maamuzi hasa kwa kuwa mtu wa kusitasita na ambaye yuko tayari kutumia uwezo wake wote kutofanya lolote.
Hivi hadi nini kitokee ndipo Rais Kikwete ajue kuwa mambo haya si ya kupuuzia? Wakati Lowassa amekwenda kukutana na Karamagi kule London na mkataba wa Buzwagi ukasainiwa, je, Rais Kikwete alifahamu ujio wa waziri wake mkuu? Je, walikutana?
Kama Rais hakujulishwa kutiwa saini kwa mkataba mkubwa namna hiyo na waziri mkuu anakutana na waziri mwingine pasipo Rais kujua katika mji walioko wote watatu, je, haoni ni ukosefu mkubwa wa kiutawala!?
Leo hii watu wakihoji mazingira ya kusainiwa mkataba huo kwa nini hiyo iitwe kelele!
Sitaki kuamini kabisa japo kwa sekunde chache kuwa Watanzania walifanya kosa kubwa kumchagua Kikwete. Sitaki ijekuwa kuwa kosa hilo vizazi vijavyo vitasimulia kama hadithi, kuwa “hapo zamani za kale kulikuwa na mwana CCM mmoja ambaye aliwapa watu matumaini sana kabla ya uchaguzi”.
Watu wengi waliamini kuwa mwanaCCM huyo ndiye atakayekuwa mkombozi na kiongozi wa kuwaonyesha njia ya kufikia nchi ile ya ahadi. Walipomchagua kwa asilimia 80 ya wapiga kura, Watanzania walijaa matumaini kwani waliamini ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana…Miaka miwili baadaye Watanzania wanashika vichwa vyao kujuta, kwani waliyemdhania ndiye kumbe siye!..” Inawezekana kuwa Rais Kikwete ni msafi kwa kiasi fulani yaani hakuchafuka hadi soksi kama wengine. Na inawezekana wapinzani kulijumuisha jina lake kwenye kundi la “mafisadi” walivuka mpaka.
Hata hivyo, naamini kabisa kuwa kila mtu anastahili nafasi ya kusahihisha alipoharibu na kupewa na nafasi moja nyingine. Rais Kikwete anayo nafasi ya pekee ya kusahihisha alipoharibu akiwa waziri, si tu anayo nafasi sasa ya kufanya hivyo bali pia anao uwezo wa kufanya hivyo. Kitendo cha kuruhusu uchunguzi ufanyike kwenye Benki Kuu (japo kwa mazingaombwe kidogo) ni hatua ya kwanza.
Watanzania wengi (nikiwamo mimi) tuliompigia debe Kikwete tunaamini anaweza kutengeneza palipoharibika. Kwa hiyo tunasubiri na tunatulia huku tumepinga vidole vyetu kuwa “atafanya kweli”.
Kinyume cha hapo akimaliza kipindi chake msishangae mkijaambiwa Rais aliyeahidi maisha bora kwa “kila Mtanzania” na yeye alianzisha “kioski” akiwa Ikulu cha kunufaisha “kila shabiki wake”.
Rais atakayefuata atatwambia “msimbughudhi Rais mstaafu” na utawala wa CCM utaendelea kutuburuza! Isipokuwa wakati huo Bunge litakuwa si la CCM tena, na hapo watajibu kwa wananchi.
Niandikie: mwanakijiji@jamboforums.comNisikilize: http://www.mwanakijiji.podomatic.com

No comments: