Friday, October 26, 2007

VIVA Chissano, Mkapa umevuna ulichopanda

WASWAHILI wana dhana kwamba kila mtu ana siku yake na kwamba siku hazifanani. Kama ni katika jambo baya watakwambia za mwizi 40, na katika mafanikio watakwambia kila mtu na nyota yake au Mungu si Athumani, ilimradi watataka kuonyesha kuwa kila mtu ana siku ambayo neema humuangukia.
Naweza kusema kuwa hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano.
Kwa Chissano siku hiyo ilikuwa juzi Jumatatu, Oktoba 22, mjini London, England, alipoibuka mshindi wa tuzo ya uongozi bora ya Mo Ibrahim na kuwabwaga wenzake 12.
Tuzo hiyo ya thamani ya dola za Kimarekani milioni tano (sawa na sh. bilioni sita) katika kipindi cha miaka 10 na baadaye kufuatiwa na malipo ya dola 200,000 (sh. milioni 200) kila mwaka, katika kipindi chote cha maisha ya mshindi, iliasisiwa mwaka jana na Taasisi ya Mo Ibrahim, raia na bilionea wa Sudan anayejishughulisha na biashara ya huduma za simu za mkononi. Ni mwanzilishi pia wa kampuni ya Celtel.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Rais mstaafu wa Msumbiji, mambo yalikuwa kinyume kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alipojikuta akibwagwa katika kinyang’anyiro hicho cha kwanza cha moja ya tuzo zenye hadhi ya juu ya Mo Ibrahim, ambayo ingemwezesha kuvuna kitita cha dola za Kimarekani milioni tano (karibu sh bilioni sita).
Huenda hali hiyo ikawa imemshtua Mkapa ambaye katika kipindi chake cha utawala wa miaka kumi (1995-2005), alikuwa kipenzi cha mataifa makubwa na taasisi zao za fedha na uchumi.
Ushindi ulivyokwenda Msumbiji
Muda mfupi baada ya Chissano kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya uongozi bora ya Mo Ibrahim, watu katika mitaa ya jiji la Maputo na miji mingine walilipuka kwa hoi hoi na nderemo.
“Watu wana furaha isiyo kifani,” alisema mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Peter Biles.
Aliongeza kuwa wengi walieleza kuwa hawashangazwi na hilo kwani kiongozi wao alistahili kushinda tuzo hiyo ya Mo Ibrahim kwa ungozi bora barani Afrika.
Kwa nini Chissano alistahili
Jopo la majaji pamoja na wananchi wa Msumbiji na pengine wale wote wanaoifahamu Msumbiji na Chissano kwa ujumla, watashabihiana katika sababu hizi zilizomfanya Chissano kuibuka mshindi.
Kumaliza vita na kurejesha amani Msumbiji
Chissano alichukua madaraka mwaka 1986 baada ya kifo cha Rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Moses Machel, wakati huo nchi ikiwa katika vita kali ya wenyewe kwa wenyewe iliyoanza tangu mwaka 1975, mara tu baada ya Msumbiji kupata Uhuru kutoka kwa Wareno walioitawala nchi hiyo kwa miaka 500.
Chissano alikabiliana na hali hiyo na akafanikiwa kumaliza vita hiyo na kulishawishi kundi la waasi la Renamo chini ya kiongozi wake Afonso Dhlakama kuwa chama cha kisiasa.
“Hii ni kutokana na mchango wake katika kuiongoza Msumbiji kutoka katika vita na kuingia katika amani na demokrasia. Kwa kweli ametoa mchango mkubwa,” alisema Kofi Annan, wakti akikabidhi tuzo hiyo mjini London.
“Maridhiano ya kuigwa baina ya pande mbili hasimu (Frelimo na Renamo) yanatoa mfano wenye kung’aa kwa dunia na ni ushuhuda wa uimara wa tabia na uongozi wake,” aliongeza Chissano anaelezewa kuwa bado ni sauti ya amani popote pale barani Afrika kutokana na wajibu wake katika Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
“Anastahili tuzo hiyo kwa kazi yake nzuri tangu alipochukua madaraka baada ya kifo cha Machel,” alisema Telma Cumbe, mwanafunzi wa chuo kikuu mjini Maputo.
Kukuza uchumi
Chissano anasifiwa kuwa kutokana na uongozi wake mzuri Msumbiji imeweza kuwa na ukuaji mzuri wa uchumi hasa ikitokea katika uchumi ulioharibika kutokana na vita. Na huenda hii ndiyo ikawa sababu ya kushinda tuzo ambayo maudhui yake hasa yanataka kiongozi mwenye uongozi bora usio na rushwa, wenye kuheshimu sheria na kukuza demokrasia.
“Kwa kweli alisaidia kuinua uchumi wa nchi baada ya usumbufu au madhara ya vita,” alisema Sam Gudo, mwandishi nchini Msumbiji
Kuheshimu sheria na kuacha haki itendeke
Ni aghalab kwa kwa viongozi wa Afrika kuruhusu ama ndugu au marafiki kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kukumbana na mkondo wa sheria, lakini hilo liliwezekana kwa Chissano.
Kijana wake anakabiliwa na tuhuma za kuhusika katika mauaji ya Carlos cardoso, mwandishi wa habari nchini Msumbiji. Chissano alikaa pembeni na kuacha sheria ifanye kazi.
Mwandishi wa habari wa BBC, Martin Plaut, alimuuliza Annan, mjini London, iwapo suala la mtoto wa Chissano kutuhumiwa kuhusika katika mauaji ya mwandishi halikuwasumbua majaji na kuwa kikwazo kwa yeye kupata tuzo hiyo ya juu kabisa.
“Tulilizungumzia hilo. Kulikuwa na mchakato wa kisheria na tulimuuliza Chissano na yeye alichotuambia ni kwamba haki ni lazima itendeke. Na tulifanya hivyo na kugundua kuwa hakukuwa na ushahidi wowote wa iwapo alijaribu kuzuia sheria isifanye kazi,” alisema Annan.
“Huwezi kumlaumu Chissano kwa kosa linalotuhumiwa kufanywa na kijana wake…yule ni mtu mzima.” Kustaafu na kukataa kugombea muhula wa tatu
Mafanikio ya Chissano katika tuzo hii yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua yake ya kukataa kugombea urais kwa muhula wa tatu wa uongozi nchini mwake. Jambo hili liliwafurahisha si tu wananchi wake, bali pia jumuiya ya kimataifa ikiwa ni pamoja na jopo la majaji lililokuwa na jukumu la kujadili na hatimaye kupata mshindi wa tuzo hiyo.
Uamuzi huo ulitafsiriwa na makundi mbalimbali ya ndani na nje ya Msumbiji kuwa ni ukomavu wa demokrasia, kwani alifanya hivyo wakati bado alikuwa anaruhusiwa na katiba kugombea muhula mwingine.
Gudo anaongeza kuwa Chissano aliyestaafu urais mwishoni mwa mwaka 2004, anaweza kuwa mfano wa kiongozi bora aliyetawala kwa muda mrefu.
“Viongozi wengine wa Afrika kama Muammar Gaddafi wa Libya na Robert Mugabe wa Zimbabwe wanapaswa kuiga mfano huu wa Chissano aliyeamua kuachia ngazi ingawa alikuwa na nafasi ya kuendelea kuongoza,” anasema Gudo.
Viongozi wengine walioshiriki katika mchuano wa tuzo hiyo iliyotolewa kwa mara ya kwanza London, na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, raia wa Ghana, ni pamoja na Mathieu Kerekou (Benin), Azali Assoumani (Comoros), Domitien Ndayizeye (Burundi) na Henrique Rosa (Guinea Bissau).
Wengine ni Maaouya Ould Sid’Ahmed Taya (Mauritania), Sam Nujoma (Namibia) Benjamin Mkapa (Tanzania), Abass Bonfoh (Togo) Gnassingbe Eyadema (Togo), Bakili Muluzi (Malawi) France-Albert Rene (Shelisheli) na Abdiqassim Salad Hassan (Somalia).
Joaquim Chissano ni nani?
Joaquim Chissano Joaquim Alberto Chissano alizaliwa Oktoba 22, 1939. Aliingia madarakani kama rais wa pili wa Msumbiji na kutawala kwa miaka 19 tangu Novemba 6, 1986 hadi Februari 2, 2005.
Tangu alipoondoka madarakani, Chissano amekuwa akifahamika kama ‘rais mstaafu kiongozi’ na amekuwa akialikwa na kufanya kazi na jumuiya ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa (UN) kama mjumbe maalumu au mpatanishi.
Kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Joaquim Chissano Foundation na pia mwenyekiti wa Forum of Former African Heads of State and Government.
Maisha ya awali
Chissano alizaliwa katika kijiji kilicho mashambani cha Malehice, katika Wilaya ya Chibuto, wakati wa ukoloni wa kireno iliyojulikana kama Jimbo la Gaza.
Alikuwa mwanafunzi wa kwanza mweusi kuhudhuria katika shule ya hadhi ya juu ya Liceu Salazar, alikokuwa mwanachama na baadaye kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa Kiafrika walio sekondari (NESAM). Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alikwenda Ureno kwa ajili ya masomo ya udaktari wa binadamu.
Kutokana na kuwa mwanaharakati mkereketwa mkubwa wa siasa, Chissano aliamua kukatiza masomo ghafla na kuja nchi Tanzania akipitia kwa muda nchini Ufaransa.
Mpigania uhuru
Chissano alikuwa mwakilishi wa chama cha kudai uhuru wa Msumbiji (Frelimo), Paris, Ufaransa, katika miaka ya 1960 alipojulikana kama mwanadiplomasia aliyetumia lugha laini iliyosaidia kuunganisha kundi lenye msimamo mkali na lile la msimamo wa wastani wa Kimarxisti yaliyokuwa yakivutana ndani ya Frelimo.
Aliamua kuingia msituni ili kushiriki katika vita ya ukombozi wa Msumbiji dhidi ya wakoloni wa Kireno.
Hadi Msumbiji inapata uhuru wake mwaka 1975, Chissano alikwishakuwa mwanajeshi wa cheo cha meja jenerali.
Kutokana na mchango wake mkubwa katika kupigania uhuru, Rais wa zamani Msumbiji, Samora Machel, aliamua kumteua kuwa waziri wa mambo ya nje, wizara aliyoiongoza kwa miaka 11.
Kuwa rais wa Msumbiji
Joaquim Chissano alikuwa Rais wa Msumbiji mwaka 1986 baada ya Rais wa kwanza, Machel, kufariki katika ajali ya ndege iliyotokea katika safu ya milima huko Afrika Kusini.
Jambo la kwanza kushughulika nalo ilikuwa kumaliza vita ya wenyewe iliyodumu kwa miaka 20 na kuhakikisha kuwa amani inarejea nchini mwake.
Kumalizika kwa vita hiyo kulilishuhudia kundi la waasi wa Renamo chini ya Dhlakama likiamua kuwa chama cha upinzani, na kushiriki katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1994 uliomshuhudia Chisano akiibuka mshindi, kabla ya kushinda tena katika uchaguzi wa 1999.
Alikuwa mtu aliyechangia kukuza demokrasia nchini mwake. Hilo lilishuhudiwa katika namna ambavyo chaguzi zilikuwa zikiendeshwa kwa njia ya haki, amani na utulivu. Moja ya chaguzi hizo ni ule wa 1999, uliomshuhudia Chissano akimshinda mpinzani wake na kiongozi wa zamani wa waasi, Dhlakama, kwa asilimia 52.3 dhidi ya 47.7
Akiwa madarakani, Chissano alikuwa pia kiongozi wa kimataifa pale alipokuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kati ya Julai 2003 na Julai 2004.
Baada ya kumaliza muhula wake wa pili wa uongozi, Chissano aliamua kutogombea muhula wa tatu katika uchaguzi wa 2004, ingawa katiba ya nchi ingemruhusu kufanya hivyo. Baada ya uamuzi wake huo chama cha Frelimo kiliamua kumteua Armando Guebuza kuwa mgombea wake, ambaye pia alifanikiwa kumuangusha Dhlakama kwa wingi wa kura.
Hatimaye alihitimisha safari yake katika uongozi wa nchi Februari 2005 alipokabidhi rasmi madaraka kwa Rais Guebuza.
Majukumu baada ya kustaafu urais
Mwaka mmoja tu baada ya Chissano kung’atuka madarakani, Desemba 4, 2006, aliteuliwa na katibu mkuu wa UN, Kofi Annan, kuwa mjumbe na mwakilishi wa UN, Uganda ya kaskazini pamoja na Sudan ya kusini, kwa lengo la kuleta suluhisho la kisiasa baina ya mgogoro unaoendelea baina ya serikali na kundi la Lord’s Resistance Army (LRA).
Chissano alikuwa kiungo baina ya ofisi ya UN ya upatanishi wa masuala ya kibinadamu iliyokuwa ikiongozwa na Eliane Duthoit na mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai (ICC), iliyokuwa imetoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa LRA, Joseph Kony, na viongozi wengine wa nne wa kundi hilo.
Tuzo ya Mo Ibrahim
Oktoba 22, 2007 itakuwa siku itakayobaki katika kumbukumbu za Chissano, Waafrika na wapenda maendeleo wote kwa ujumla kote ulimwenguni.
Ni siku ambayo katibu mkuu wa zamani wa UN, Annan, aliongoza sherehe zilizofanyika London, akiizindua na kumkabidhi Chissano (mshindi wa kwanza) tuzo hiyo ya dola za Kimarekani milioni 5 (sawa sh bilioni 6) kutokana uongozi bora.
Tuzo hiyo maalumu kwa uongozi wenye mafanikio hutolewa na taasisi ya Mo Ibrahim kwa kiongozi mstaafu wa Afrika ambaye ameonyesha utawala bora.
Awali tuzo hiyo ilipangwa kutolewa kila mwaka, lakini baadaye taasisi ya Mo Ibrahim iliamua kuitawanya zawadi ya dola milioni tano katika kipindi cha miaka 10 na kutoa nyongeza ya dola 200,000 kwa mwaka katika kipindi cha maisha ya kiongozi mstaafu aliyeshinda tuzo hiyo baada ya miaka kumi hiyo.
Je, atazitumia vipi pesa za tuzo hiyo?
Kulikuwa na mawazo tofauti kuhusiana na jinsi Chissano anavyotakiwa kuzitumia pesa za tuzo yake.
“Ni vyema atumie pesa za mfuko wake katika kuimarisha amani na demokrasia katika Afrika,” anasema Lionel Muchano, mwandishi wa habari nchini Msumbiji.
Naye mwanauchumi, Evaristo Cumbana, anasema kuwa Chissano anapaswa kutumia fedha za tuzo yake kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kijamii katika nchi yake.
“Tuzo ni tunu ya kujivunia kwa Msumbiji na mfano mzuri wa utawala bora,” alisema
Makala hii imeandaliwa na Chachanyakega kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa. Anapatikana kwa anuani ya barua pepe: chachanyakega@yahoo.com au simu 0713 485373

MOCAMBIQUE ESTA NO CORACAO

No comments: