Wednesday, October 17, 2007

Viongozi wa dini mmewaangusha Watanzania

NINAPOKAA chini kuwaandikia waraka huu wapendwa watumishi wa Mungu, ninajihisi kutostahili na kutofaa kusema nitakayosema. Mikono yangu yanitetema na vidole vyangu kama vina ganzi kwa hofu lakini moyo wangu unadunda kwa shauku.
Kwenu nyote msimamao katika nyumba zetu za ibada na kuwaongoza watu wetu katika safari ya kiroho, ninyi mnaojua mmeitwa kumtumikia Mungu Mwenyezi katika makundi ya imani zenu mbalimbali, ninyi ambao watu huwaita “wahudumu wa Bwana” na Watendaji kazi katika shamba la Mungu, kwenu nyote Salam!
Ninapozungumzia “wachungaji” simaanishi wale tu wa Wachungaji wa Kilutheri au makanisa ya Kiprotestanti au wale wanaoongoza parokia na sharika mbalimbali; na sina maana ya wale tu ambao ni viongozi wa dini ya Kikristo. “Wachungaji” ninaowazungumzia hapa ni wale ambao kwa maana ya msingi kabisa ya neno hilo, wanajukumu la kuchunga na kutoa mafunzo ya kiroho kwa waamini wao.
Hapa najumlisha viongozi wote wa kidini wa dini zote na madhehebu yote, wale ambao jukumu lao la kwanza ni katika kuwaongoza watu katika mafundisho na maadili ya kidini. Wale wenye kukiri imani ya mitume na wale wenye kukiri shahda, wale wenye kusimama makanisani na wale wenye kusimama misikitini. Nina maana ya wale wote ambao kimsingi wanachunga maisha ya kiroho ya watu kwa kutoa maongozo, maelekezo na mausia ya kiroho ili waamini wao waweze siku moja kufika mbinguni. Hawa ndiyo wachungaji ambao ninakusudia waraka huu.
Kwenu nyote mashehe, mapadre, maimamu, wachungaji n.k bila ya shaka mnafahamu wajibu wenu mkubwa katika maisha ya kiroho ya waamini wenu na bila ya shaka mmekuwa mkijitahidi kila kukicha kuwapatia waamini wenu mafundisho na maelekezo ambayo mna uhakika yatawasaidia kiroho. Hata hivyo ni kwa masikitiko makubwa niseme wazi kuwa kwa kiasi kikubwa mmewaangusha Watanzania. Sauti yenu haisikiki kama inavypaswa katika kuongoza “kondoo” wenu, na matokeo yake badala ya nyinyi kuwa katika kundi la wanaoongoza, sasa hivi mnajikuta mnafuata.
Ninayasema haya hasa baada ya kusoma Tamko la Baraza Maaskofu Katoliki, lililotolewa hivi karibuni. Niliposoma tamko hilo nilijikuta natikisa kichwa kwa shaka, kwani walichotaka kukisema hawakukisema na wasichotakiwa kukisema walijaribu kukisema. Matokeo yake walitumia herufi na maneno mengi waliyoyapanga vizuri kwa lugha “endelevu” lakini bila kusema kitu! Ni ubutu huu ambao ninawaandikia ili muunoe na viongozi wengine wa madhehebu mengine ya dini watakapotoa tena matamko wafikirie vizuri.
Viongozi wetu wa dini mmekuwa butu! Mnameremeta kama kisu kwenye ala, na mnang’aa kama sime iliyoinuliwa. Mnapendeza kwa kanzu na majoho yenu na kwa hakika mnavutia mnapozungumza kwa maneno yaliyopangwa. Hata hivyo hamna tena makali ya kukata kwani mmekuwa butu kwa muda mrefu na sasa mmbakia kama ishara ya “kile kilichowahi kuwapo”.
Mlikuwa wapi wakati Watanzania 900 walipokufa kwenye ajali ya mv Bukoba? Mlikuwa wapi wakati wa ajali ya mv Kilombero, ajali ya treni Dodoma, na ajali ya basi kule Singida? Leo hii Rais Joseph Kabila amemtimua Waziri wake wa Usafiri baada ya ajali nyingine ya ndege iliyoua watu zaidi ya thelathini. Hivi hapa Tanzania ni hadi watu wangapi wafe kwenye ajali zisizo za lazima ndipo wachungaji wetu mtaungana na wanaharakati kutaka viongozi goigoi wawajibishwe?
Zilipotokea vurugu Mwembechai na baadaye mauaji ya kisiasa kule Pemba, mbona hatukuwaona mkiikemea serikali, vyama vya kisiasa na wananchi kwa ujumla na mkaliacha jambo hilo kwa watu wachache? Wakati serikali inanunua ndege ya bilioni 50, rada ya bilioni 50, magari mawili ya milioni mia mbili, na kuingia mkataba wa Richmond, wachungaji wetu mlikuwa wapi? Hata hili suala la sasa linaloendelea la Buzwagi na Karamagi, mbona mmechelewa kuamka na mnafumbua macho kama mliolazimishwa au kukatishwa usingizi?
Ninyi mnaojitambua kuwa ni watumishi wa Mungu, mbona mmekuwa kimya na mnagwaya mbele ya watawala wetu? Mbona hivi karibuni kiongozi mmoja wa ngazi za juu alitamka mbele ya viongozi wa dini kuwa taasisi za dini zinapojenga mahospitali n.k zinashiriki katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, mbona hamkukosoa, au zile hisia kuwa kanisa ni sehemu ya CCM zina ukweli? Kuna wakati lazima muwe mashahidi wa ukweli!
Wako wapi kina Sheikh Khalifa Khamis watetezi wa “mali” za Waislamu? Je, na wao wamekuwa kama CCM kuwa mali za Watanzania wote zikipotea kama zilivyopotea Benki Kuu haziwaumi, ila zile za Waislamu na za CCM ndizo zinazowauma? Iko wapi ile Shura ya Maimam ambao kila baada ya muda wanatishia maandamano ili kuishinikiza serikali kufanya hili au lile? Mbona hadi leo hawajatishia maandamano kutaka kujua ukweli wa Benki Kuu, Buzwagi, Richmond, n.k ? Au ndio huo uongozi wa kidini mamboleo ambao wapendwa watumishi wa Mungu mnauendeleza? Bakwata wako wapi wakati nchi yetu iko katika wakati mgumu?
Wako wapi wale wahubiri wa Injili, wahubirio miujiza? Yuko wapi Mchungaji Kakobe ambaye yuko tayari kukemea “mapepo” wakati watu wanatoana upepo? Ni lini ataacha kwa dakika chache kuhubiri miujiza na badala yake aje kuwajuza watu, kuhusu udhambi wa maisha ya kujikuza, na ya kutweza wengine?
Haitoshi kuimba mapambio, haitoshi kusikiliza kasida, na haitoshi kushika vitabu vya dini mikononi, huku nchi na wananchi wanakosa mwelekeo katika maisha yao ya kawaida. Sala nyingine za miujiza zinaweza kuwa si za lazima endapo watu watakua na matumaini wanapoenda mahospitalini, wanapata huduma nzuri serikalini n.k
Wapendwa wachungaji wetu, nina hofu kuwa inawezekana hamkemei na kupiga vita uovu wazi wazi na pasipo utata kwa sababu ninyi nanyi mnanufaika kwa namna moja au nyingine na uongozi mbovu na tabia za kifisadi. Je, yawezekana ni kwa sababu baadhi yenu wamelala kitanda kimoja na ufisadi, wakijifunika mablanketi ya unafiki, huku wanajipepea upepo wa uzandiki? Inawezekana ni kwa sababu baadhi ya miradi yenu (binafsi na vinginevyo) isingewezekana isipokuwa kwa baraka za “walio katika viti vya enzi vivunjikavyo?”
Ni wazi mara nyingi mna hofu ya kutotaka kuichukiza serikali. Tunatambua kuwa mkipiga kelele sana viongozi watawanyooshea vidole na kuwaonya, na watawaambia “fanyeni kazi zenu za dini, msiingilie serikali” Tunajua hilo linaweza kuwafanya mgwaye, kwani wanaweza wakaanzisha uchunguzi dhidi yenu au kujaribu kuwaumbua kutokana na madhaifu yenu mbalimbali kama ilivyomkuta Askofu Ncube wa Zimbabwe. Je, ni hilo ndilo mnaloogopa, kiasi cha kwamba mikataba mibovu inasainiwa na hakuna mwenye ujasiri wa kuitisha Waziri Karamagi ajiuzulu au awajibishwe?
Tunafahamu pia kuwa wakati mwingine hamna ujanja isipokuwa kula sahani moja na watawala wetu ilimradi mkiwaalika kwenye harambee zenu watokee, vinginevyo mna hofu kuwa michango yenu na makusanyiko yenu hayatafanikiwa. Lakini kama kilichotokea Burma hivi karibuni ni fundisho, basi kuna wakati viongozi wa dini ni lazima wafanye uchaguzi aidha kufumba macho na kuendelea kufurahia hisani ya watawala, au kuwa majasiri na kuongoza mapambano ya kifikra ili kuamsha dhamira za wananchi wetu ili tuweze kujenga taifa lile la kimaadil mnalolihubiri kila siku.
Ni kiongozi gani kati yenu atakayekuwa tayari kusimama juani, kuandamana, na kushika mabango na sisi wanakijiji kuihoji na kuikemea serikali? Ni nani kati yenu ambaye atakuwa tayari hata kwenda kifungoni katika harakati za kutetea haki za raia na wananchi? Itakuwa ni siku ya uamsho mkubwa tukimuona Kardinali Pengo mtaani, Mufti Simba mtaani, kina Kakobe, Mwakasege, Mwaipopo na wengine mtaani wakiongoza kelele za kutaka serikali iwajibike.
Katika Tanzania ambayo viongozi wa dini na serikali hawawezi kufanya kazi pamoja isipokuwa hadi wakubaliane, na wasiweza kupingana bila kuvunjiana mahusiano, ni vigumu kwa viongozi wetu wa dini kwenda kinyume na serikali na hicho ndicho kiini cha ubutu wenu.
Niwakumbushe kuhusu kiongozi mwingine wa dini ambaye alionyesha kilele cha “Uchungaji Bora” siyo tu kwa kwenda jela na kufungwa, bali kutoa uhai wake mbele ya risasi muuaji. Dr. Martin Luther King Jr, alipokuwa amefungwa kwenye jela ya Birmingham Alabama, Marekani, baadhi ya viongozi wa dini walimshangaa kwa nini amekuwa anapiga kelele sana. Walimshauri apunguze makali yake kwani yeye ni kiongozi wa dini.
Akiwa kifungoni, Dk. King aliandika barua yake maarufu ijulikanayo kama “Barua kutoka Jela ya Birmingham” (Letter from Birmingham Jail) ambayo ndani yake alieleza ni kwa nini yeye kama kiongozi wa kidini hakuweza kukaa kimya. Na hata alipouawa kule Memphis, alikuwa tayari moyoni amejua kuwa ameshafika “kilele cha mlima”!
Alisema jambo moja ambalo natumani litawasha moto ya uzalendo na kusababisha mlipuko wa utumishi wa umma ndani yenu. Alisema “ukandamizaji mahali popote, ni tishio la haki mahali pote.” Haiwezekani viongozi wa dini wakakaa katika kisiwa cha mahekalu yao, huku watu wanataabika, wananyimwa haki au kwa namna moja au nyingine kufanywa duni.
Ndiyo maana ninawauliza, mlikuwa wapi wakati vijana zaidi ya ishirini wa Kitanzania wamekwama Ukraine na kupigwa na ubaridi nje ya ubalozi wa Uingereza, kisa serikali imejifanya mbabe? Mbona hamjauliza hatima yao ikoje? Na kwa nini hamkuibana serikali kutoa majibu ya kina badala ya majibu ya kibabe iliyoyatoa?
Leo hii mnaposimama na kutuhubiria maadili, hivi mnaweza kweli kusimama mbele ya Mungu mnayemtumkia na kusema ninyi ni mawakili wazuri wa maadili mnayotwambia tuyafuate? Wapendwa viongozi wa dini, wakati uko mbioni na sasa umefika ambapo mnatakiwa mfanye uchaguzi, tena uchaguzi wa haraka na wa makusudi. Nina mapendekezo machache kwenu kufikia uchaguzi huo.
Kwanza kabisa mtakapotoa matamko mengine huko mbeleni na hasa yale yaliyokusudiwa kutuma ujumbe kwa watawala wetu, acheni kuzunguka mbuyu, semeni mnachotaka kusema badala ya kutumia maneno mengi kutosema kitu! Kuweni kama Yohana Mbatizaji (Nabii Yahya A.S) na watangazieni watawala wetu kwamba wakati wa toba umefika na ya kuwa shoka limekwishainuliwa juu ya shina!
Pili, vunjeni hii ndoa haramu mliyojifungisha na watawala wetu na muwe huru kweli kweli. Leo hii mnashindwa kukemea maovu moja kwa moja kwa sababu mnaowakemea ni watu ambao wanawanufaisha!
Ndiyo maana leo mmekuwa bubu kukemea tabia ya Rais kufanya biashara Ikulu, na mmekuwa bubu mabilioni ya fedha kupotea Benki Kuu, na kwenye taasisi mbalimbali na halmashauri mbalimbali nchini. Mnashindwa kunyoosha kidole kwani mkinyosha kimoja mnaogopa vitatu vinawaelekea nyinyi wenyewe na gumba linashuhudia mbinguni! Mnatetemeka mbele ya saluti na mnagwaya mbele ya vimulimuli!
Na mwisho, muwe tayari kusimama upande wa haki si kwa matamko yasiyokwisha na mausia yasiyokoma bali kwa hatua dhahiri na za makusudi. Muwe tayari kufanya kile Yesu wa Nazareti (Nabii Issa Bin Maryam A.S) alichokisema kuhusu Mchungaji Mwema kuwa “Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake”.
Kuna siku (Mungu aiepushie mbali) wakati taifa letu litapitia ile “Saa ya Mjaribu” na mtatakiwa wakati huo kuchagua uhai wenu au hatima ya kondoo, natumaini mtafuata mifano ya wale waliokwenda mbele yenu, mifano ya kina Oscar Romero, Martin Luther King, Malcom X, na watawa wa Kibuddha kule Burma ambao wiki chache zilizopita baadhi yao wamekwenda kwenye vifo vyao wakitetea haki za wananchi wenzao. Siku taifa lenu litakapowaita kutoa sadaka kubwa mtakuwa tayari au mtaandika barua nyingine ya kichungaji au kuitisha vyombo vya habari?
Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu mnayemtumikia mpate ujasiri wa kusimama kama manabii na kunyosha mikono ya haki mbele zake, na kuwaongoza watu wetu siyo tu katika “malisho ya majani mabishi” ya mbinguni, bali katika kupata mana itokayo mbinguni hapa hapa duniani kwanza.
Ni matumaini yangu hatamjaribu kujenga ufalme au paradiso mpya mbinguni bali mtaanza kushiriki katika kujenga paradiso ya Bongo hapa hapa duniani! Msipofanya hivyo, kama kile kinachowakuta CCM leo na nyinyi mjiandae kitawakuta, nacho ni kuwa mkianza ‘kutuyeyusha’ na kutupiga soga za kizamani, Watanzania watawahesabu kuwa na ninyi hamna mpango (you’ll become irrelevant). Natumaini, hilo halitatokea. Myakumbuke maneno ya Nabii Yeremia kuwa “Ole wenu Wachungaji, wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu” Yer. 23.1Ni mimi msafiri mwenzenu katika safari ya Kiroho,
M. MwanakijijiNisikilize: http://mwanakijiji.podomatic.com
Niandikie: mwanakijiji@jamboforums.com

No comments: