Wednesday, October 17, 2007

Hoja ya Zitto, Dk. Slaa, imejibiwa na kufungwa

Richard Tambwe Hiza
NIMEKUWA nikifuatilia kwa karibu sana maendeleo ya siasa na demokrasia yetu ndani na nje ya Bunge.
Nashukuru na kufurahi kuona kwamba demekrasia yetu inakuwa kwa kasi kubwa ingawaje wengine wameanza kuvuka mipaka na taratibu tulizojiwekea na kuishia katika mazingira yanayowaletea matatizo wao wenyewe.
Sakata la Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), na maandamano ya kumpokea Dar es Salaam, ziara za viongozi wa upinzani mikoani na taarifa za kutaka kushitakiwa kwa kuvunja heshima/hadhi ya baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, kumenifanya nami nitoe mchango wangu katika mjadala waliouanzisha ndani na nje ya Bunge letu.
Nimeshuhudia mengi yakisemwa yanayonishawishi kuamini kwamba hoja zao zimejibiwa, lakini wao wanataka kuendeleza vuguvugu hili wakidhani linaweza kuwasaidia kujijenga kisiasa.
Nimejaribu kuainisha mambo yote wanayolalamikia na kukuta kulikuwa na hoja 10 muhimu zilizokuwa za msingi katika sakata hili.
Baada ya kuzipitia na kuamini kwamba zimeshajibiwa, ingekuwa vyema kwa wale wanaoona majibu hayatoshi wangeelekeza nguvu zao katika vyombo vya sheria, vinginevyo wana kila sababu ya kukaa kimya na kutafuta hoja nyingine.
Katika makala hii, nitajaribu kuainisha baadhi ya majibu niliyoyapata kutokana na vyanzo mbalimbali na ningependa mjadala huu tuuelekeze huko.
Je, Zitto na wapinzani wanapinga sera ya uwekezaji?
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mijadala iliyofanyika bungeni na katika mikutano ya hadhara ni hakika wapinzani wote wanaiunga mkono sera ya uwekezaji, bali wanatofautiana na serikali kuhusu viwango vya mrahaba tu.
Jambo hili haliwezi kufikiwa muafaka hata kama viwango vingebadilishwa maana bila kutofautiana hakutakuwa na upinzani.
Je, kinachopingwa ni mkataba kusainiwa London au baadhi ya vipengele vya mkataba?
Wakati Zitto alipokuwa anawasilisha hoja bungeni, alionyesha wasiwasi kwa mkataba kusainiwa London, lakini hakuainisha kifungu chochote kilichomo kwenye mkataba huo kinachoashiria rushwa au ufisadi. Ndiyo maana katika kifungu cha 15 cha hoja yake, alipendekeza iundwe kamati teule kuchunguza mkataba huo na kuona kama kuna vitendo vyovyote vya uvunjaji wa sheria za nchi na kuweza kupoteza mapato ya serikali kwa ufisadi.
Hili lilitokana na ukweli kwamba yeye binafsi alikuwa hajawahi kuuona mkataba aliokuwa akiulalamikia, jambo linalowafanya watetezi wa serikali kushangaa mtu atalalamikiaje kitu asichokijua.
Je, mkataba kusainiwa London ni kosa?
Watetezi wa hoja hii wanasema taratibu zote za kisheria na kitaalamu zilikamilishwa na vyombo husika hapa hapa nchini, Waziri Nazir Karamagi angeweza kuweka saini mahali popote. Hawaishii hapo wanatoa mifano ya mikataba mbalimbali iliyosainiwa nje ya nchi ukiwamo mkataba wa Uhuru uliosainiwa Lancaster House, Uingereza, na ule wa Reli ya Tazara uliosainiwa China.
Wanahitimisha kwa kusema watu wenye mawazo mabaya wanaoona nafasi kama hiyo ingewatokea wao wangekula rushwa wanadhani hata mwingine naye hufanya hivyo
Je, Zitto alichanganya vifungu vya sheria katika hoja yake?
Wakati Karamagi anajibu hoja binafsi ya Zitto alilieleza Bunge kwamba Zitto wengi tunayemwona au kudhani ni makini sana, alichanganya vifungu vya sheria mbili tofauti.
Sheria hizo (Sheria ya Madini ya mwaka 1998 na Sheria ya kodi ya mwaka 1973) na hivyo kuifanya hoja yake isipate nguvu ya nukuu ya sheria yoyote iliyovunjwa. Suala hili ni muhimu wananchi wakapata ukweli wake, kwani linamtia doa shujaa wetu kutoka Kigoma Kaskazini na chama chake kwamba hakina wataalamu washauri wa kuweza kusaidia wabunge wake.
Maagizo ya Rais na taratibu zote za kisheria zilifuatwa?
Zitto katika hoja yake alidai maelekezo ya Rais hayakufuatwa. Waziri ameeleza jinsi kamati ya ushauri ya madini na ofisi ya mwanasheria mkuuu wa serikali zilivyofanya kazi na kutoa kibali kwa mkataba mpya wa Buzwagi kusainiwa.
Ameeleza kwamba maagizo ya kupitiwa upya kwa mikataba ya zamani yamefanyika na kamati iliyoundwa iliwasilisha mapendekezo yake Septemba 14, 2006. Mapendekezo hayo yametumika katika kufikia makubaliano na marekebisho ya baadhi ya vipengele katika mikataba ya zamani. Je, kuna yeyote mwenye taarifa tofauti? Aitoe tuione.
Zitto ameonewa kwa kuzuiwa kuingia bungeni?
Bunge linadai limechukua hatua kulingana na taratibu za uendeshaji wake zilivyo.
Si Zitto wala CHADEMA waliopinga kama kanuni hizo hazisemi hivyo zaidi ya kutumia mwanya huo kuingia barabarani na kulifanya ajenda ya kisiasa.
Kumbukumbu za Bunge zinaonyesha hata wabunge wa CCM waliwahi kuzuiwa kuingia bungeni baada ya kufanya makosa kama ya Zitto (kulidanganya Bunge).
Je, serikali imejibu hoja za Zitto?
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mjadala wa Bunge ulivyokuwa, inaonyesha serikali imejibu vipengele vyote ikiwa ni pamoja na kuwatoa wasiwasi wabunge na wananchi kwa kuthibitisha kwamba mkataba mpya wa Buzwagi umeboreshwa zaidi kuliko awali na hivyo kutoona sababu ya kuutilia wasiwasi au kuunda tume itakayopoteza fedha bure.
Hatua za CHADEMA na wapinzani zina faida yoyote kwa umma?
Baadhi ya Watanzania nikiwamo mimi tunaamini kuwa baada ya kufanya vibaya sana kwa upinzani katika uchaguzi uliopita, kumeufanya ukate tamaa kabisa na hatua inazochukua sasa ni katika kujaribu kutafuta njia ya kuuchanganya uma na ikiwezekana uwaunge mkono.
Lakini historia ya mabomu ya Mzee Mrema na alipofikia sasa kisiasa haitoi matumaini yoyote kwa upinzani. Kutumia mabomu yasiyo na ushahidi wowote na kutarajia kuungwa mkono na uma uliopevuka kisiasa wa nchi yetu.
Hata hivyo wengi tunaamini sakata hili la Zitto na mabomu ya Dk. Slaa yameiwezesha CHADEMA kuwa mbele ya vyama vingine vya upinzani.
Leo kukiwa na safari ya mkoani wote hupata lifti ya Mbowe na hivyo kuonekana kama wasindikizaji tu. Kama kuna anaepinga muda upo utaamua.
Kwa nini wapinzani hawataki kulipeleka suala la ufisadi katika vyombo vya kisheria?
Ni dhahiri kulipeleka suala hili mahakamani ni vigumu kwa kuwa ushahidi uliopo kama si wa kwenye mtandao ambao haujulikani kaandika nani, basi ni hisia zilizojengeka kutoka kwa wanaotuhumu.
Lakini najiuliza kama kila anayemtuhumu mwenzake bila kutoa vielelezo atakamatwe, baada ya mwezi mmoja kuna atakayebaki?
Hapa ndipo ninapoona wapinzani wanapoteza muda bure. Kama wana ushahidi waende katikia vyombo husika na sisi sote tutawapongeza.
Je, wapinzani wanaaminika?
Hili nalo limekuwa swali gumu kulipatia majibu na ingekuwa vyema wapinzani wakachukua hatua, vinginevyo watabaki kulalama wakati wananchi wakiendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi kila uchaguzi unapofika.
Wakati Zitto anaadhibiwa kwa madai ya kulidanganya Bunge, Dk. Slaa amekuja na madai mazito ya ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali na anataka wananchi wamuamini.
Watetezi wa serikali wanadai kama Dk. Slaa anataka aaminiwe basi alipeleke suala hilo Takukuru akiambatanisha na vielelezo vyake, ili wahusika waweze kulishughulikia badala ya kupayuka barabarani.
Ni imani yangu tukiweka mijadala yetu wazi na pasipo kuwa na agenda za siri, tutagundua suala hili halina nguvu tena baada ya majibu yaliyoyaoanishwa.
Tukifanya hivyo tutaepuka siasa zinazoanza kujenga chuki kati ya wanasiasa wetu. Tufuate utaratibu wa kupingana na kukosoana katika mambo ya kweli na ya msingi bila kugombana.
Katika siasa za wenzetu walioendelea kidemokrasia, hali ya uendeshaji wa shughuli za kisiasa ni tofauti sana na mwenendo ambao vyama vyetu vinakwenda nao.
Wenzetu mara tu uchaguzi unapokwisha wanahamishia ushindani wao ndani ya Bunge, wanalitumia kupinga mambo ya msingi kama sera au sheria wanazoona zitazuia maendeleo ya nchi.
Jambo hili hufanyika kwenye mijadala ya bajeti, ya sheria mpya na wakati wa kuthibitisha wateule wa Rais wa kushika nafasi nyeti katika serikali.
Maandamano ya kumpokea Zitto na mikutano ya wapinzani sehemu mbalimbali nchini iliyofuatia baada ya hapo, iliyopambwa kwa shutuma mbalimbali za rushwa na ufisadi kwa viongozi waandamizi wa serikali. Hapo ndipo nadhani tulipoanza kupoteza mwelekeo sahihi wa siasa za ushindani.
Mwandishi wa makala hii alikuwa mkurugenzi wa habari na uenezi wa Chama cha Wananchi (CUF). Sasa ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na anapatikana kwa simu namba 0784263798.

No comments: