Friday, October 12, 2007

Hivi ndivyo Sikukuu ya Idd inavyotakiwa kusherehekewa

Shabani Matutu
IDD EL FITR ni Sikukuu ya Kiislamu inayosherehekewa baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kumalizika.
Siku hii Waislamu huitumia katika kufurahi na kumshukuru Mwenyezi Mungu sambamba na kuomba wakubaliwe funga zao kwa kuwafutia madhambi yao na hatimaye kuwafikisha kwenye heri.
Sikukuu ya Idd huhitimishwa kwa kuswaliwa swala ya Idd el Fitr wakati wa asubuhi sambamba na kumtukuza Allah (S.W) kwa takbira (Allahu Akbar).
Swala ya Idd el Fitr inaswaliwa kwa rakaa mbili ikifuatiwa na khutba mbili kama zile zilizosomwa kabla ya swala ya Ijumaa. Swala hii ina takbira 12.
Takbira saba hutolewa katika rakaa ya kwanza kabla ya kusoma Suratul Faatiha na takbira tano hutolewa katika rakaa ya pili kabla ya kusoma Suratul Faatiha.
Mahali panapofaa kuswaliwa swala ya Idd panatakiwa pawe pakubwa, ingawa kuswali msikitini si dhambi ila ni bora sehemu kubwa iliyo wazi, patakaposaidia kukusanyika Waislamu wengi zaidi kutoka sehemu tofauti.
Katika hadithi ya Anas (Radhi yallahu Anhu-R.A) anaeleza kuwa Mtume Muhammad (SAW) alikuwa haswali Idd el Fitri hadi ahakikishe amekula japo tende katika idadi ya witri yaani namba zisizogawika kwa mbili na yenyewe.
Hadithi ya Burayda (R.A) inasema kwamba kipenzi cha Mwenyezi Mungu Mtume Muhammad (SAW) alikuwa hatoki kwenda kuswali swala ya Idd el Fitr hadi awe amefuturu kitu.
Ni sunna pia kuleta takbira mara kwa mara kuanzia pale mwezi unapoandama hadi baada ya swala ya Idd el Fitr.
Mambo yanayotakiwa kufanywa Siku ya Idd
Ni jambo la heri kwa Mwislamu Siku ya Idd kuoga, kuvalia nguo nzuri ikiwa ni pamoja na kupaka uturi (manukato) mazuri kwa wanaume.
Pia ni siku inayofaa kwa Waislamu kupika vyakula vizuri na vinywaji visivyokuwa na kilevi, na kwale wafugaji na walio na uwezo ni sunna kumchinja mnyama aliye bora zaidi kuliko wengine katika mifugo yake.
Hadithi ya Hassan Asibbit (R.A) inasema kwamba Mtume (SAW) ametuamrisha katika Idd mbili kuvaa vizuri zaidi kadri tuwezavyo, tupake uturi bora zaidi kuliko wote tulionao na tuchinje wanyama wenye thamani zaidi kuliko wote tulionao.
Ni sunna pia kuwakaribisha ndugu, marafiki, majirani, maskini, yatima na wengine wasiojiweza.
Pia ni sunnah kuwatembelea wagonjwa, maskini na watu wasiojiweza ikiwa ni pamoja na kupeana zawadi.
Mwisho wa Ramadhan isiwe mwanzo wa maasi, ila iwe kipimo cha kuendeleza kufanya mema kwa Waislamu na kuachana na maovu.
Zakatul Fitr
Hii ni zakat inayotolewa baada ya Waislamu - wake kwa wanaume - kumaliza funga yao ya Ramadhan na hutolewa kabla ya swala ya Idd el Fitr.
Kwa wale wasio na uwezo watalipiwa na mawalii wao kwa mfano mume atawatolea wazazi wake kama hawana uwezo wa kujilipia na baba atalazimika kuwalipia Zakatul Fitr wale wote walio chini yake iwapo kama anauwezo.
Umuhimu wa Zakatul Fitr ni faradhi iliyoambatanishwa na faradhi za mwezi wa Ramadhani. Mtume amsema ili kuiwezesha swaumu yako ipokelewe vizuri na Allah ni lazima kwa mwenye uwezo aitolee Zakatul Fitr.
Anayestahili kutoa Zakatul Fitr ni mwenye chakula cha kuwatosha watu wake anaoishi nao na kuwa na ziada ya kutosha usiku na ile ziada nyingine ndiye anayetakiwa kutoa Zakatul Fitr.
Kiwango cha Zakatul Fitr
Kwa mujibu wa hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (R.A) anasema kwamba kiwango kinachotakiwa kutolewa kwa kila mtu ni ‘sai’ moja ya chakula kinachopendwa sana katika sehemu husika.
Kwa mfano, pwani wakati wa sikukuu hupendelea kula wali au pilau na sai inayozungumziwa hapa kwa nyakati hizi ni sawa na kilo mbili na nusu za bidhaa husika.
Kutokana na hali halisi ya kimaisha ni vyema zaidi mtoaji atoe fedha kuliko bidhaa ili kumsaidia mhusika unayemtolea kununua bidhaa ambayo anaipenda mwenyewe.
Muda unaofaa kutolewa Zakatul Fitri umebainishwa kwenye hadithi iliyotolewa na Ibn Umar (R.A). Inasema kwamba Mtume (SAW) aliwaeleza watu kuwa watoe Zakatul Fitr kabla ya kuswali Idd el Fitr.
Kulipa Zakatul Fitri mapema kabla ya kuswali Idd au mapema zaidi ya hapo kutamwezesha unayempatia kufurahia Idd na Waislamu wengine.
Iwapo itatokea sababu ya msingi kama vile kusahau hadi Idd ikaswaliwa, huna budi kuitoa baada ya swala na iwapo ataacha kutoa kwa makusudi au kwa uzembe basi ajue kutoa kwake huko hakutamnufaisha kwa chochote.
Watu wanaostahili kupewa Zakatul Fitr
Ni chakula cha maskini na wale wasiojiweza kujipatia chakula pamoja na wale walio chini ya uangalizi wao kwa Siku ya Idd na usiku wake, ili na wao wajisikie na kufurahia Idd na Waislamu wenzao wenye uwezo.
Iwapo Zakatul Fitr atapewa mtu aliye na uwezo na kuachwa asiye nao, wote watakaokuwa wametoa na kupokea Zakatul Fitr hiyo watakuwa wameidhulumu haki ya anayestahili kupewa. Hivyo watakuwa wamekwenda kinyume na matakwa ya Mwenyezi Mungu.
Sikukuu ya Idd itasherehekewa kufuatana na mwandamo wa mwezi na iwapo mwezi hautaonekana, basi Waislamu wanatakiwa waendelee kufunga hadi kukamilisha siku 30 kamili ndipo watakaporuhusiwa kufungua.
Sikukuu ya Idd haistahili kusherehekewa kwa kupiga muziki, ngoma, kunywa mapombe na kufanya mambo yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu, kwani utakiwa umemuasi.
Siku ya Idd si siku ya kufanya maasi, kwani Mtume (SAW) anasema: “Kumuasi Mwenyezi Mungu Siku ya Idd ni sawa na kufanya uasi siku ya kiyama”.
*Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa barua pepe; kimyamatutu@yahoo.com.

No comments: