Friday, October 12, 2007

Maajabu kesi ya Balozi Mahalu

na Happiness Katabazi
UPANDE wa mashitaka katika kesi ya kuhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Ricky Mahalu na mwenzake, umekiri kwamba hakuna mlalamikaji katika kesi hiyo.
Maelezo hayo yalitolewa na Mwanasheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Abubakar Msangi, wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Pamoja na Balozi Mahalu, mtuhumiwa mwingine katika kesi hiyo ni Grace Martin.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa saa 3:30 asubuhi mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Sivangilwa Mwangesi, huku upande wa utetezi ukiwa na jopo la mawakili wanne wa kujitegemea, ambao ni Dk. Sengondo Mvungi, Cuthbert Tenga, Bob Makani na Alex Mngongolwa, aliyekuwa kiongozi wao.
Jana, upande wa utetezi uliwasilisha maombi manne, la kwanza likiwa ni kutaka wapatiwe maelezo ya mlalamikaji katika kesi inayowakabili wateja wao.
Ombi la pili lilikuwa ni kupatiwa vielelezo vilivyoambatanishwa kwenye hati ya maelezo ya makosa na ushahidi, kwa kuwa awali taasisi hiyo ilitoa hati isiyo na vielelezo vyenye orodha ya mashahidi. Aidha, mawakili wa utetezi waliomba pia kupatiwa orodha ya mashahidi.
Katika ombi la nne, mawakili hao waliitaka mahakama iizuie TAKUKURU isiwabughudhi watuhumiwa. Ombi hilo lilitokana na taarifa kuwa maofisa wa TAKUKURU waliwaita watuhumiwa ofisini kwao na kuwataka waorodheshe mali zao, jambo ambalo ni kuingilia kazi ya mahakama na kudai kuwa watuhumiwa hapaswi kufanya kazi za kipelelezi.
Katika majibu yake, mwanasheria wa TAKUKURU, alikubaliana na ombi la kwanza, kuwa wanayo haki ya kupewa maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo lakini aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo haina mlalamikaji na kuwa tuhuma za kesi hiyo zilikusanywa kutoka kwenye vyombo vya habari.
“Mheshimiwa hakimu, katika ombi la kwanza, upande wa utetezi unayo haki, lakini kwa bahati mbaya kesi hii haina mlalamikaji kwa sababu tuhuma za kesi hii tulizikusanya kutoka kwenye vyombo vya habari yakiwemo magazeti,” alisema Wakili Msangi na kuwaacha baadhi ya wananchi wakiwamo waandishi wa habari na mawakili wa kujitegemea wakiangua vicheko mahakamani hapo.
Aidha, akijibu ombi la pili, Msangi alidai kwamba upande wa serikali hauwezi kutoa orodha ya vielelezo vya mashahidi kwa sababu kufanya hivyo kutahatarisha usalama wa mashaidi.
Katika jibu jingine, alidai kuwa TAKUKURU iliwataka watuhumiwa hao waorodheshe mali zao kwa sababu kifungu cha 26 na 27 cha Sheria ya Rushwa ya mwaka 2007 vinairuhusu TAKUKURU kumwita mtu yeyote na kumtaka aorodheshe mali zake, endapo itapata taarifa za tuhuma za kujilimbikizia mali dhidi ya mtu huyo.
Kwa msingi huo, Msangi aliitaka mahakama itupilie mbali ombi hilo na badala yake iendelee na usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo.
Baada ya majibu hayo, Mgongolwa alisema iwapo kesi hiyo haina mlalamikaji, inapaswa kuondolewa mahakamani hapo na kunukuu vifungu mbalimbali vya sheria na kuieleza mahakama kwamba kesi yoyote ya jinai huanza kwa malalamiko kutoka kwa mlalamikaji na inashangaza kuwa katika kesi hiyo hakuna mlalamikaji.
Aidha, alisisitiza kuwa ni lazima upande wa utetezi upatiwe vielelezo na orodha ya mashaidi kwa kuwa hilo ni hitaji la kisheria na linaendana na ibara ya 13 ya Katiba ya nchi inayotaka mtu aelezwe vizuri shitaka, vielelezo na mashahidi ili ajue yanayomkabili na kuandaa utetezi wake.
“Kwa kuwa upande wa serikali umekiri wenyewe mahakamani hapa kwamba kesi hii haina mlalamikaji, kwa sababu tuhuma walizipata kwenye magazeti, ndiyo maana wameshindwa kumtaja mlalamikaji, ni nani au idara gani ya serikali inayowashitaki wateja wetu kwa wizi?” alihoji Mgongolwa na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo kwa kuwa kisheria hakuna kesi isiyokuwa na mlalamikaji.
Baada ya malumbano hayo ya kisheria, Hakimu Mwangesi aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 17 atakapotoa uamuzi.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa wiki mbili baada ya Mahakama Kuu kutoa amri ya kusitishwa kwa usikilizwaji wa ombi la Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), lililotaka kupitiwa upya kwa dhamana ya watuhumiwa hao

No comments: