Friday, September 14, 2007

Mwislamu afanye nini mwezi wa Ramadhani?

Na Barnabas Maro

KUFUNGA ni moja ya nguzo tano za Kiislamu.
Kwahiyo katika mwezi wa mfungo - Ramadhani, Mwislamu anawajibika kuacha kila jambo linalokatazwa na Qur’an Tukufu pamoja na hadithi za Mtume na Fiqih (vitabu vya sheria).
Kusimamisha (kudumu) katika swala tano - alfajiri, adhuhuri, alasiri, magharibi na isha.
Pia atoe zaka na mali au nafaka.
Zaka ni kutoa mafungu nane kwa yatima, wapita njia, wajane, wenye kugharimika (wasiojiweza), wenye kusimamia dini, watumikiao dini, ujenzi wa nyumba za Mungu na usambazaji wa mafundisho ya Mungu.
Kufunga mwezi wa Ramadhani maana yake ni kujinyima vitu vilivyozoeleka kwa matumizi ya binadamu. Mwislamu anapaswa kujizuia na mambo yanayoweza kuharibu funga yake.
Sababu za kufunga
Kuuona mwezi wa Ramadhani (taz.Qur. 2:185); kuthibitisha ukweli wa mtu aliyeuona mwezi na kuangalia uadilifu wake; kwa habari za mapokeo yenye uadilifu kwa dhana ya kuingia kwa mwezi wa Ramadhani na kwa kukamilika siku 30 za mwezi wa Shabani, yaani mwezi mmoja kabla ya Ramadhani.
Sharti za kufunga
Awe Mwislamu; mwenye akili timamu; mtu aliyetakasika na ajue wakati wa kuingia kwa mwezi wa Ramadhani.
Sharti za wajibu
Kuwa Mwislamu; kujilazimisha kufunga; kuwa na uwezo wa mali na chakula, kuwa na afya nzuri na kuwa na msimamo usioyumba.
Nguzo za funga
Kutia nia kila siku; kuacha vyenye kusababisha kufungua na asiwe mjinga kwa kutojua afanyalo.
Vibatilishaji vya funga (vitu vinavyoweza kusababisha funga yako isihesabiwe)
Kuvunja nia ya kufunga, kupata siku kwa wanawake, kupata nifasi, kutokuwa na akili hata kwa dakika moja, kama kwa hasira. Ikiwa hivi anabidi afungue.
Pia mwenye kifafa hatakiwi kufunga na anayepatwa na kifafa wakati wa kufunga, basi funga yake ni batili na kulewa hapana.
Imezoeleka na wengi kuwa, wakati wa mwezi wa Ramadhani wafungaji hujilimbikizia kila aina ya chakula, kwa tamaa ya macho.
Haitakiwi kuwa na hofu ya kufunga kwa kujilimbikizia vyakula vya kila aina. Unapofanya hivyo, funga yako ni batili.
Maana unapojilimbikizia vyakula vya kila aina, hutoweza kuvimaliza. Kwa nini basi usijiandalie chakula cha kutosha kufuturu na ziada ukawapa masikini au wasio nacho?
Kumbuka huu ni wakati wa kufanya toba kwa Mwenyezi Mungu na kinachotakiwa ni kuwa mwadilifu na mkarimu kwa wengine.
Baadhi ya watu hutoka majumbani mwao asubuhi wakisema wamefunga, lakini mbele ya safari hula kwa kujificha. Hawa wanawafungia wanadamu au Mwenyezi Mungu?
Unapofunga unatubu madhambi uliyofanya kwa kipindi cha mwaka mzima uliopita. Anayejua madhambi yako na toba unayofanya ni Mungu wako. Sasa unapoongopa kufunga ilhali hufanyi hivyo, hujui kuwa wajidanganya mwenyewe na kujiongezea dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu?
Mwislamu anapochelewa kulipia deni la funga kabla ya mwezi mwingine wa Ramadhani, funga yake ni batili.
Katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani, mfungaji hatakiwi kusema uongo, kusengenya, kugombanisha watu na kufanya isirafu, yaani kuzidisha matumizi, hasa ya chakula katika futari, kuvimbiwa.
Mwezi wa Ramadhani, wafanyabiashara hupandisha bei za bidhaa ili kujinufaisha kwa faida. Mfanyabiashara Mwislamu, hatakiwi kupata faida na badala yake awasaidie wengine.
Aidha, asiwe kero kwa ajili ya biashara zake, avae mavazi ya kusitiri mwili na asiwe mwenye kejeli.
Wanawake waonekane nyuso na viganja vya mikono, tu huku miili yao ikiwa imefunikwa. Haiswihi mwanamke wa Kiislamu kuvaa nguo zisizofunika mwili wake kuanzia miguuni mpaka juu.
Baibui ndilo vazi rasmi la heshima kwa mwanamke wa Kiislamu.
Aidha hatakiwi kujiremba mno kwa kujipaka wanja, rangi za midomo na mafuta mazuri, kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha funga ya wengine kwa kuwaingiza kwenye matamanio ya kimwili.
Kuna baadhi ya Waislamu wanaoishi nje ya ndoa na wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani huendelea kuishi pamoja huku wakifunga. Huko ni kujidanganya, kwani funga ya watu hao ni batili.
Kuishi wawili bila ndoa ni uhawara, na kamwe hawastahili kuwa mke na mume. Watu wa aina hiyo hawana tofauti na wazinifu.
Unapokuwa katika swaumu kisha ukaahidiana na hawara yako kuwa mkutane baada ya kufuturu ili muendelee na mambo yenu au kuwekeana miadi ya kurudiana baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, yaani mfungo mosi na kuendelea, funga yako huwa batili.
Kuna maneno mengine mawili yanayotumika sana, hasa siku moja kabla ya kuandama mwezi wa Ramadhani. Wengi husema ‘vunja jungu’ wakimaanisha kufanya kila aina ya uchafu kabla ya kufunga! Nani aliwadanganya kuwa kabla ya kufunga watu hutakiwa kufanya dhambi kwa kushangilia ndipo waingie katika funga? Huko ni kujiongezea madhambi.
Waislamu wanatakiwa kuamini kuwa kheri na shari hutoka kwa Mwenyezi Mungu.
marobarnabas@yahoo.com
0756 855 314
0784 334 096

No comments: