Thursday, September 13, 2007

Faida za kufunga mwezi wa Ramadhani

Shabani Matutu
KUFUNGA mwezi wa Ramadhani ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu, ambayo Muislamu yeyote asiye na matatizo kiafya anatakiwa kuitekeleza, ambako asiyefunga, atakuwa ni miongoni mwa watu waliovunja nguzo hii.
Tukirejea katika Qur’an tukufu, Mwenyezi Mungu anasema; “Enyi mlioamini (Waislamu) mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa wale waliokutangulieni ili muwe wenye subira siku chache tu kwa kufunga huko.” (2:183-4).
Siku chache hizo (siku 30 ama 29, inategemea na kuandama kwa mwezi, ndizo ambazo Waislamu wameamriwa kufunga, kwani mwezi huu ni mwezi mtukufu kuliko miezi mingine katika mwaka wa Kiislamu.
Kwanini unasemwa kuwa mwezi mtukufu kuliko mingine? Qur’an inasema kuwa, mwezi huu ndio mwezi ambao kipenzi chetu, Mtume Muhammad (S.A.W) aliteremshiwa Qur’an ndani ya usiku wa ‘Lay-la tul kadir’.
Kufunga hakukuja wakati wa zama za Mtume (S.A.W), bali tangu wakati wa baba yetu Adam.
Kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Amiyrul Mumineen Ali, inasema: “Mtu wa kwanza ulimwenguni aliyefaradhiwa kufunga ni baba yetu Adam.”
Pia Waislamu wameamrishwa kufunga ili wale waliojaliwa mali, nao wapate kujua uchungu wa njaa inayowakuta masikini wanapokuwa wanawalilia njaa.
Mwisho wa aya ya 183 inasema kwamba: “Mjizuieni kufanya uovu na maasi, kwani inavunja nguvu ya matamanio.”
Aya hii ina maana kuwa iwapo muumini atakuwa anashindwa kuepuka vitendo vya matamanio na maasi, basi akifunga atakuwa ameepuka vitendo hivyo kwani swaumu hupigana na vitendo hivyo.
Kwa wale wenye kufunga, thawabu zake hazina mfano wala makisio, Mwenyezi Mungu katika ‘Hadithul Qudsi’ (hadhithi takatifu) anasema kuwa: “Swaumu ni yangu na mimi ndiye nitakayetoa thawabu zake.”
Kwanini swaumu inakuwa na swawabu kubwa? Hii inatokana na kuwa muumini anapokuwa anaswali, lazima wanadamu watakuona, ukienda kuhiji Makka, lazima utaonekana na ukitoa zaka muhusika uliyempa atajua, lakini ukifunga, ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye anayejua kama kweli utakuwa umefunga au la. Kwa mtu mwingine kujua ni vigumu.
Qur’an inasema kwamba kwa aliyefunga hastahili kujionyesha kwa kuonyesha unyonge hali ya kukasirika, mithili ya mtu aliyeudhiana na watu na isitoshe awe mkarimu kwa watumishi wake mpaka watu wengine wa nje.
Kitabu kinachojulikana kwa jina la ‘Wasa-ilu-sh-shia’, kinazungumzia hadithi iliyopokelewa na imamu wa sita, Imaam As-Saadiq inayosema kwamba mwenye kufunga swaumu anakuwa katika ibada, hata kama atakuwa amelala, anapata thawabu ya ibada ikiwa hakumsema mtu.
Pia imepokelewa hadithi na Imaam As-Sadiq inayesema kwamba: “Mwenye kuificha saumu asihubiri mtu kama amefunga, basi Mwenyezi Mungu atawahubiri malaika hivi ‘kiumbe wangu ametakiwa alindwe na adhabu yangu, basi mlindeni’ na malaika watakulinda.”
Kilicho bora kufanywa wakati wa Ramadhani
Kwa maelezo aliyoyatoa Mtume (S.A.W) katika hotuba yake ya mwisho ya Ijumaa ya mwezi wa Shaaban, aliwaeleza waumini kwamba wafanye fadhila, utukufu na amali bora.
Baada ya Mtume Muhammad kumaliza hotuba hiyo, Ameerul-Mu-mineen Ali alimuuliza mtume kuwa, amali njema ni ipi? Akajibu: “Uchaji wa Mwenyezi Mungu kwa kila kilichokubaliwa na kukatazwa.”
Uchaji wa Mwenyezi Mungu ni jambo kubwa kuliko lingine lolote katika mwezi huu wa Ramadhani pamoja na kwamba yapo mambo mengine ya sunna kama kusali sunna, kufanya ibada, kusoma Qur’an, kulisha, kuvisha na mambo mengine ya heri.
Uchaji wa Mwenyezi Mungu si jambo la mwezi wa Ramadhani pekee, bali kufanya hivyo kunatakiwa kufanyika kwa wakati wote wa maisha ya binadamu.
Daraja za swaumu
Daraja ya kwanza ni wale waumini wanaojizuia na vitu vinavyovunja swaumu na kujiondoa na kundi la wale wasiofunga.
Mtume (S.A.W.) anasema kwamba: “Katika vitu rahisi zaidi, alivyovikubali Mwenyezi Mungu ni juu ya mwenye kufunga katika kufunga kwake ni kuacha kula na kunywa.”
Daraja la pili ni yule afungae, kujizuia kuvunja swaumu, ikiwa ni pamoja na kujizuia na matamanio ya viungo vyake na mambo yasiyokubalika mbele za Mwenyezi Mungu.
Imamu Jaffer As- Sadiq alisikika akisema kuwa; ‘kujizuia kula na kunywa tu hakuitwi kufunga, lakini ukifunga, ujifunge macho, masikio, ulimi, tumbo, utumbo wako, mikono na miguu yako, na kila unachokatazwa, kukaa kimya uwezavyo ila kwa jambo la heri na uwe mpole kwa mtumishi wako.’ Aina hii ya funga mtu anatakiwa kufunga pasipo kufanya madhambi.
Kuna hadithi inasema kwamba, siku moja mtume S.A.W. alimuona mama mmoja aliyefunga swaumu na akamtukana mtumishi wake, hapo Mtume aliamuru mama yule aletewe chakula ili ale.
Baada ya kuletewa chakula, yule mwanamke akasema: “Yaa Rasuulallah, nimefunga mimi.” Mtume akamwambia; ‘hukufunga kwa sababu umemtukuna mtumishi wako’.
Pia kuna hadithi ya swahaba mmoja, Imaam Al Baqir (A.S) alisema kwamba: “Uongo humfuturisha aliyefunga.”
Waislamu kote nchini, na duniani kwa ujumla, wanatarajiwa kuanza kutekeleza ibada ya kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani kuanzia leo ama kesho, kutegemea na kuandama kwa mwezi.

No comments: