• Asema mgombea binafsi lazima
na Deogratius Temba
MWENYEKITI wa Chama cha Demokratiki (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amesema uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba hautafanyika bila kuwepo kwa mgombea binafsi.
Pia amesema Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Philipo Marmo, amevunja Katiba ya nchi na kukiuka sheria kwa kutoa matamshi yanayokiuka maamuzi ya Mahakama Kuu bungeni kuwa suala la mgombea binafsi halitawezekana katika uchaguzi huu unaofauata.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika hoteli ya Travertine, Magomeni, jijini Dar es salaam, Mtikila alisema pamoja na Marmo kukiuka sheria na Katiba ya nchi, pia anapaswa kushtakiwa kwa kuidharau Mahakama Kuu sambamba na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye alipaswa kujiandaa kutoa maelezo ya rufaa hiyo, lakini hakufanya hivyo.
“Kitendo cha Waziri Marmo, kulizungumzia suala hili bungeni ni kuidharau Mahakama Kuu na ya Rufaa ambazo suala hili liko chini yao. Waziri anajua Aprili 8, rufaa itaendelea mfululizo halafu anafanya kosa kubwa tena la jinai anavunja sheria na Katiba,” alisema.
Alisema kitendo cha Waziri Marmo kufanya hivyo kinatokana na tabia ya viongozi wengi wa serikali kupuuza maslahi ya taifa na kujali maslahi yao binafsi.
“Watanzania wanapaswa kupuuza maelezo ya waziri, kama vile mtu asiye na elimu, hatutarajii mtu kama waziri kuvunja sheria hadharani vile. Waziri Marmo anatakiwa kuchukuliwa hatua, apelekwe mbele ya sheria kwani ni kosa kubwa alilolifanya,”aliongeza.
Mtikila ambaye ana historia ya kufungua kesi nyingi za Kikatiba alisema uchaguzi ni suala nyeti ambalo ni lazima liheshimiwe, Bunge na serikali wanapaswa kutekeleza maagizo ya mahakama na siyo kuingilia mahakama.
Alisema kinachoshangaza ni jinsi ambavyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali alivyojitetea mahakamani kuwa ofisi yake haijajiandaa juu ya rufaa ambayo waliifungua wao wenyewe.
“Mwanasheria anaomba miezi minne kana kwamba si yeye aliyeipeleka rufaa hiyo, kama alishindwa kujiandaa kwa miaka minne tangu Mei 5, 2006 hadi leo miezi minne itamtosha? Je, ni nani anapaswa kufanya marekebisho ya Katiba kama si wao? Na walitaka wayafanye lini wakati hukumu ilishatoka?” alihoji Mchungaji Mtikila.
Mtikila aliendelea kusema kuwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba ni lazima uandaliwe kwa utaratibu wa kuwepo kwa mgombea binafsi, la sivyo utaahirishwa hadi Februari, ili marekebnisho yanayotakiwa yafanyike.
Mtikila ambaye kwa sasa ana kesi ya kutuhumiwa kumkashifu Rais Jakaya Kikwete, kwa kumuita gaidi, jana alimtaka Rais kutokuogopa mgombea binafsi kwani hiyo ni moja ya changamoto na kama amefanya mazuri atarudi madarakani lakini kama hakufanya ataukosa urais.
“Rais Kikwete, asiogope mgombea binafsi, kama amefanya kazi vizuri ya kusaidia wananchi anaogopa nini? Si wananchi wataona? Na kama hakufanya si wananchi watamwadhibu kwa kumpa huyo mgombea binafsi?” alisema.
Alisema anampa Rais Kikwete ushauri wa bure kuwa aachie ngazi mapema ya kuto kugombea kwani mgombea binafsi akitokea CCM, chama kitamfia mikononi mwake kutokana na kumeguka na mgombea binafsi atatoka humo.
Katika mkutano huo, Mtikila alitishia kuwa yeye ni kiongozi wa dini na kama serikali haitasikiliza suala hilo na kuiheshimu mahakama, ameshawasiliana na viongozi wengine wa dini waitishe maandamano makubwa ya kulaani kitendo hicho na kuikataa CCM, kabla ya kwenda mahakamani kuupinga uchaguzi huo.
Monday, February 15, 2010
Mtikila aivaa serikali
Posted by Mafia Kisiwani at 4:33 PM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment