Tuesday, February 16, 2010

Lowassa, Sitta wagomea suluhu

• Kamati ya Mwinyi yaongezewa muda

na Mwandishi Wetu




HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) kimeshindwa kuwasuluhisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa na Spika wa Bunge Samuel Sitta, Tanzania Daima limeelezwa.

Taarifa za uhakika kutoka katika kikao cha NEC kilichoketi Dodoma tangu juzi, zinasema kwamba makundi ya vigogo hao yalikuwa yanakamiana kumalizana na kutunishiana misuli, huku Sitta akidai hana sababu ya kusuluhishana na Lowassa kwa sababu hawana ugomvi binafsi.

Kutokana na kushindwa kuwasuluhisha mahasimu hao wawili na wapambe wao, kikao hicho kilipendekeza Kamati ya Mwinyi iongezewe muda ili kuwapa fursa nyingine ya kufikia hatima ya uhasama huo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka miwili.

Awali, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipendekeza kamati hiyo ipewe mwezi mmoja kukamilisha usuluhishi huo, lakini wajumbe walidai hautoshi.

Vyanzo vya habari vinasema kambi za Sitta na Lowassa zilitunishiana msuli ndani ya NEC na kukwamisha kile kilichokuwa kimeandaliwa na Kamati ya Mwinyi; na kumpa wakati mgumu Rais Kikwete.

Kabla ya kikao hicho, Kamati ya Mwinyi ambayo iliundwa na NEC miezi kadhaa iliyopita kuchunguza chanzo cha uhasama miongoni wa wabunge wa CCM, ilikuwa na mapendekezo makali ambayo yaliwavuruga wajumbe.

Baadhi ya mapendekezo hayo yalitaka wanachama na viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wanyang’anywe uongozi na watimuliwe uanachama ili kukisafisha chama mbele ya umma.

Hata hivyo, mapendekezo hayo yalileta mvutano mwingine ndani ya kamati yenyewe, hata kabla ya kuwasilishwa kwa NEC, kwa kuwa wajumbe wawili kati ya watatu wanaoiunda walikuwa na pande zao ndani ya makundi ya Lowassa na Sitta.

Kamati hiyo inaongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Wajumbe wengine ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa, na Spika Mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahmani Kinana.

Habari zinasema Kinana na Msekwa wako katika kambi mbili tofauti, na walitoa mapendekezo yanayopingana, hivyo kukwamisha utekelezaji wake.

Wapambe wa Lowassa walidai kwamba Waziri Mkuu huyo mstaafu alikuwa tayari kusulushishwa na Sitta, lakini Sitta aligoma kwa maelezo kuwa yeye anapiga vita ufisadi, si Lowassa.

Sitta amekuwa anatajwa kuwa kinara wa wabunge wa CCM waliokuwa wanajinadi kuwa wapambanaji dhidi ya ufisadi kabla ya kunyoosha mikono wiki hii.

Mvutano wa Sitta na Lowassa ulizuka waziwazi mwaka juzi ilipoundwa Kamati ya Bunge kuchunguza mchakato wa kile kilichokuja kujulikana kama kashfa ya Richmond, iliyosababisha Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu Februari mwaka juzi.

Tangu wakati huo, kumekuwapo mvutano mkubwa kati ya kundi la Lowassa na la Sitta; na katika kikao cha NEC kilichopita, wajumbe wanaomuunga mkono Lowassa, ambao ndio wengi ndani ya NEC, walitoa azimio la kumvua Sitta uanachama, ubunge na uspika.

Katika kuokoa jahazi, Rais Kikwete aliunda Kamati ya Mwinyi, ambayo baadhi ya wananchi waliitafsiri kuwa ililenga kuwaziba mdomo wabunge wa CCM waliokuwa wanaikosoa serikali bungeni.

Hata sasa, wabunge wa CCM walio upande wa Lowassa wanamlaumu Sitta kwamba anaisaliti serikali na CCM kwa kuruhusu mijadala mikali bungeni dhidi ya serikali.

Wakati Sitta amekuwa anashambuliwa na kundi la Lowassa, wananchi walio wengi wamekuwa wanamuunga mkono yeye na wabunge wenzake kwa maelezo kuwa ukali wao ndiyo unalifanya Bunge lionekane makini.

Hata hivyo, wiki iliyopita Bunge lilinywea kwa kuamua kunyamazia ripoti isiyoridhisha juu ya serikali ilivyotekeleza maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya Richmond. Pale pale, Spika alitangaza kufunga mjadala wa Richmond, bila kujali kwamba serikali imegoma kuwawajibisha watendaji wa Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyestaafu na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.

Jukumu la kuwawajibisha lilikuwa mikononi mwa Rais Kikwete.

Lakini wachambuzi wa kisiasa wanadai ubutu huu wa akina Sitta, ulilenga kumnusuru Kikwete asipigiwe kura ya kutokuwa na imani naye, na vile vile kujenga mazingira ya kuwasuluhisha kina Sitta na Lowassa katika kikao cha NEC.

Hadi tunakwenda mitamboni, kikao cha NEC kilikuwa kinaendelea Dodoma, na hakukuwa na uwezekano wa kuwasuluhisha mahasimu hao.

Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vya habari vilidai kikao hiki kimerejesha umoja na mshikamano miongoni mwa wanaCCM kueleka uchaguzi mkuu; ingawa kutosuluhishana kwa Lowassa na Sitta kunaweza kuendeleza mgawanyiko utakaokiyumbisha chama hicho kueleka Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

No comments: