Friday, July 1, 2011

Katiba mpya kuzinduliwa Aprili 2014


Daniel Msangya, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ametangaza kuwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itazinduliwa katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano mwaka 2014.

Pinda alitangaza kauli hiyo jana mjini Dodoma alipokuwa akifungua semina elekezi kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa iliyohusu Mchakato wa kuelekea kuundwa kwa katiba mpya ya Tanzania kwa viongozi hao wa serikali.


Alisema mchakato wa maandalizi ya kuandika Katiba mpya unatarajiwa kukamilika Aprili 2014.

"Mchakato wa maandalizi ya kuandika Katiba mpya unatarajiwa kukamilika Aprili, 2014. Katiba hiyo mpya inatarajia kuzinduliwa ifikapo Aprili 26, 2014 katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar," alisema Waziri Mkuu Pinda.

Hadi kufikia siku hiyo ya Aprili 26, 2014 ni imebaki miaka miwili na miezi kumi kuanzia sasa.

Kutokana na hali jiyo Pinda aliwataka viongozi hao kujiandaa kikamilifu kutekeleza mpango wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi.


Akizungumzia muswada huo, Pinda alifahamisha kuwa umeainisha hatua mbalimbali zitakazopitiwa kuelekea mabadiliko ya katiba ya nchi.

Aliainisha hatua hizo kuwa ni pamoja na zinazomhusisha Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kufanya makubaliano ya kuunda Tume itakayoratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko hayo.

Pia kutoa hadidu za rejea zitakazotumiwa na tume ya kukusanya maoni, kuweka mfumo wa kitaasisi wa kuandaa na kuwasilisha taarifa kuhusu maoni yaliyokusanywa kuhusu katiba mpya ya nchi.

“ Pia mchakato huo utahusu kuweka utaratibu wa kuunda Bunge la Katiba litakalojadili rasimu ya katiba mpya, kuweka utaratibu wa upigaji wa kura ya maoni kuhusu kukubali au kuikataa katiba iliyopitishwa na Bunge la Katiba,” alifafanua Waziri Mkuu Pinda.

Alitaja majukumu ya Tume hiyo, kuwa ni pamoja na kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi, kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa misingi ya kikatiba inayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utwala wa sheria na utawala bora.

Jukumu lingine la tume hiyo ni kutoa mapendekezo kwa kila hadidu za rejea, kuandaa na kuwasilisha taarifa ya maoni kwa wananchi.

Pinda alisema katika kukusanya maoni ya wananchi, maeneo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa yametajwa kuwa ni nafasi na majukumu ya mihimili mitatu ya dola ikiwemo Mahakama, Serikali na Bunge na masuala ya haki za binadamu na utawala bora.

Waziri Mkuu alisema katika hatua hiyo, tume hiyo itazunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara na ya ndani na nafasi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia kwa wakuu wa mikoa na wilaya ni kutoa ushirikiano wa kutosha kwa tume kwa kuwezesha mikutano hiyo kufanyika pamoja na upatikanaji wa mahitaji yote katika uendeshwaji wa mikutano hiyo.

“Ni matarajio yangu baada ya semina hii, mtawaelimisha wananchi kuwa hatua inayoendelea hivi sasa siyo ya kutunga katiba mpya, bali ni kuunda Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi, kuelekea kutungwa kwa katiba mpya,” alisisitiza Pinda.

Alitahadharisha viongozi hao kutoingiza siasa katika mchakato huo na kutowashawishi wananchi wakati wa kutoa maoni, badala yake wawape uhuru wa kupendekeza wanachoona ni bora pasipo kuwashinikiza.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Mkuchika, alisema: “Bahati mbaya katika hatua za mwanzo za mchakato huu, baadhi ya wananchi wameonekana kukosa uelewa juu ya dhamira ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mchakato na hatimaye kuandikwa kwa katiba mpya.”

Mkuchika alimwambia Waziri Mkuu kuwa wizara yake imeandaa semina hiyo ili kuwawezesha viongozi wa Serikali katika ngazi ya mikoa na wilaya kupata uelewa sahihi kuhusu hatua zilizoanzishwa katika mchakato huo wa kuwa na katiba mpya.

No comments: