Wednesday, November 10, 2010

Tukubali, tukatae, umma umemkataa Kikwete

Bakari M. Mohamed




MATOKEO ya Uchaguzi Mkuu, 2010 yametoa muelekeo wa wapi Jakaya Mrisho Kikwete ametoka, alipo (sasa), na anakoelekea!

Hakika, uchaguzi uliomalizika kwa yeye (Jakaya Mrisho Kikwete) kutangazwa mshindi wa jumla na hatimaye kuapishwa, umeonyesha jinsi kiongozi huyo alivyopoteza mvuto.

Mwaka 2005, wakati Jakaya Mrisho Kikwete alipoingia kwenye kinyanga’anyiro cha kugombea urais alikuwa na mtaji wa “mvuto”. Pamoja na kupewa nafasi kubwa ya kuwa “mkombozi”, vilevile alionekana ni “tumaini jema” kwa wananchi waliokata tamaa.

Na hata waandishi mahiri wa makala na vitabu (waliyejipendekeza na wengine kulamba viatu vyake) walimuandikia makala na au vitabu (na vijarida) kuonyesha matumaini yao kwake.

Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na kutengenezewa (kama anavyodai mwenyewe) Ilani ya CCM ya 2005-2010 alikuwa na “manifesto ya mtandao” iliyohanikiza “maisha bora kwa kila Mtanzania” na kwa kuwa wananchi wa Tanzania takriban asilimia 80 (au 90% kwa mujibu wa Taarifa ya Benki ya Dunia, 2007) ni maskini, wengi walimpa matumaini yao: kuondoa umasikini na kuboresha hali zao za maisha! Wapiga kura wa Tanzania kwa mwaka 2005 walikuwa na matarajio makubwa kwa Jakaya Mrisho Kikwete!

Ukiachilia mbali mvuto wa kisiasa kwa ahadi ya “maisha bora kwa kila Mtanzania,” Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa na uso wa bashasha na tabasamu (la kufa mtu), hali iliyowafanya baadhi ya watu wake hata kudiriki kumpa sifa hizi mgombea mzuri (wa sura) na mwenye tabasamu la huruma; mgombea kijana (japokuwa umri wake kwa wakati ule (2005) ulikuwa mkubwa dhidi ya Prof. Ibrahim H. Lipumba wa CUF na Freeman Mbowe wa CHADEMA).

Hata hivyo, wapiga kura hawakusikia ya mnadi swala wala mchota maji msikitini; Kikwete alikuwa chaguo lao!

Hata viongozi wa dini, hususan aliyekuwa Kiongozi Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam – Baba Askofu Methodius Kilaini alidiriki kutamka kwenye kongamano lililofanyika Jangwani kuwa, “Jakaya Mrisho Kikwete ni chaguo la Mungu.” Hata makanisa mengine ya “kilokole” si tu yalimualika mgombea huyo katika kuendesha harambee za kuchangia makanisa hayo, bali pia yalipata nafasi ya kumkabidhi “Biblia Takatifu” ili apate hekima kama ya Nabii Suleimani!

Hivi ndivyo ilivyokuwa, Jakaya Mrisho Kikwete aliwapendeza wengi na wapiga kura wengi walipatwa na raghba. Jakaya Mrisho Kikwete lilikuwa “chaguo” lililovutia na kuwaburuza wengi.

Hata pale alipoanguka jukwaani akiwa anahutubia Jangwani (CCM ilipokuwa inafunga kampeni zake Desemba, 2005) nchi nzima ilizizima kwa hofu ya kumkosa “kipenzi cha watu” kutokana na jinsi mgombea huyo alivyowavutia wengi.

Wapiga kura wa Tanzania walijielekeza kwenye vituo vya kupigia kura na hakika kura kwa Jakaya Mrisho Kikwete zilikuwa za “kishindo kikubwa”!

Pamoja waliojiandikisha kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu, 2005 walikuwa chini ya wale waliojiandikisha na kuhakikiwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010, Jakaya Mrisho Kikwete alipata kura 9,123,952 (tuseme milioni 9.1) hii ikiwa na maana kwamba mgombea huyo wa CCM (chaguo la Mungu wakati ule) alipata asilimia 80.28 (tuseme 80%)!

Huu ulikuwa ushindi mnono mno kushuhudiwa kwenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa katika Tanzania ukiachilia mbali “Enzi za Mwalimu” tulipokuwa na mfumo wa “ndiyo ni yeye tu; au hapana – nani mwingine isipokuwa yeye”.

Mambo yamebadilika sana! Miaka mitano (2005-2010) ya Jakaya Mrisho Kikwete tumeshuhudia ukali na ugumu wa maisha usiopimika, hususan kwa wananchi maskini ambapo kuna ongezeko kubwa la gharama za maisha ilhali kipato cha wananchi kiuchumi kimeshuka na au kupungua sana!

Ukiachilia umasikini na uduni wa kipato binafsi cha wananchi wa kawaida, Jakaya Mrisho Kikwete hakuonyesha jitihada zozote za makusudi na za moja kwa moja kuonyesha huruma kwa wananchi maskini (na fukara) wa Tanzania katika kuboresha hali zao za maisha. Ukweli na uhakika, hali za maisha ya wananchi wengi wa Tanzania ni ngumu na mbaya; na kama kuna mtu asiyeiona na au kuihisi hali hii, ana matatizo ya “ubinafsi kayaya”.

Maisha ya watu wengi wa Tanzania (wa mijini na vijijini) ni ya kubangaiza. Wananchi wengi: hawapati mlo kamili (na wenye kutia siha njema); hawana maji safi na salama (na ya uhakika); hawana nyumba bora (za gharama nafuu) kwao na familia zao; hawana mavazi ya sitara (ukiachilia mbali nguo kuukuu na mitumba); hawana huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu; hawana elimu bora ya watoto wao; na wametelekezwa kijamii.

Haya ndiyo maisha bora yaliyodhamiriwa na Jakaya Mrisho Kikwete? Sijui, jibu atakuwa nalo mwenyewe!

Lilikuwapo tangazo la ajira kwa vijana! Hili si tu liliwafanya vijana walipuke kwa furaha na wapagawe, bali pia liliwasukuma na kuwaburuzwa kwenye kampeni za kumshabikia na kumpenda kupita kiasi Jakaya Mrisho Kikwete pasipokuwa na yakini ya kupembua ahadi za kisiasa (propaganda).

Ahadi hii ilikuwa tamu mno, hata pale vijana walipokosa ajira rasmi waliendelea kusubiri kama afanyavyo fisi kusubiri mkono wa binadamu udondoke! Tahamaki, miaka mitano imekwisha na Jakaya Mrisho Kikwete alirudi tena, na mara hii sera ya “maisha bora kwa kila Mtanzania” na “mamilioni ya ajira” haikusikika kabisa.

Kipindi cha miaka mitano (2005-2010) ya Jakaya Mrisho Kikwete, ukiachilia ugumu wa maisha kiuchumi, kuliibuka suala nyeti na lililoondoa imani ya wananchi kwa Serikali ya CCM ufisadi! Ufisadi na ujambazi wa kiserikali uliyojificha kwenye vivuli vya marais watangulizi wa Jakaya Mrisho Kikwete, yaani Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, ulikomaa na kutoa sura mpya kwenye Awamu ya Nne (ya Kikwete).

Kama kawaida ya Jakaya Mrisho Kikwete alitoa hutuba huku akitabasamu na kusema, “wala rushwa anawafahamu; anawapa muda wajirekebishe.” Hii ilikuwa kauli mbaya kwenye mapambano dhidi ya ufisadi!

Jamii ya wananchi wa Tanzania walishuhudia kuibuliwa kwa ufisadi na ujambazi wa kiserikali (kleptocracy) kwenye sekta mbalimbai za shughuli za Serikali ya CCM: kashfa ya Richmond; kashfa ya mikataba ya madini; kashfa ya wizi wa fedha za EPA; kashfa ya matumizi mabaya ya ofisi za umma; kashfa ya rada; kashfa ya ununuzi wa ndege ya rais; kashfa ya uuzaji holela wa mali za serikali (viwanda, migodi, nyumba, na mashamba); kashfa ya Meremeta; na nyingine nyingi (kubwa na ndogo).

Hakika, hadi tunaingia kwenye Uchaguzi Mkuu, 2010 Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa hajaonyesha utashi wa kweli wa kisiasa katika kushughulikia ufisadi kwa upana wake! Kama Mwenyekiti wa CCM – Taifa na Rais wa Nchi, kiongozi huyo ameshindwa kuonyesha “mvuto” wake kama alivyowavutia wananchi mwaka 2005.

Kwa ujumla, Jakaya Mrisho Kikwete ameshindwa kuonesha ukomavu wa shakhsia ya uongozi makini na utumizi wa busara na hekima ya kuongoza jamii yenye kuzingatia haki, usawa, na uadilifu.

Mafisadi na majambazi wa kiserikali waliendelea kutumia fursa nzuri iliyotokana na mtaji wa kuwa na “rais mshikaji” hata kuigeuza Ikulu ya Magogoni kuwa kituo cha kupanga ufisadi wa kimfumo – hii ni hatari kwa mustakabali wa maendeleo na usalama wa taifa kiuchumi, kisiasa, na kijamii.

Jakaya Mrisho Kikwete amewakatisha tamaa wananchi wengi wa Tanzania na kwa jinsi hiyo, wengi wamepoteza matumaini ya mustakabali murua wa nchi yao kiuchumi, kisiasa, na zaidi kijamii.

Kwa kuwa Jakaya Mrisho Kikwete alitambua kupwaya kwake katika medani za kuongoza uchumi, siasa, na jamii katika kuwaletea wananchi “maisha bora”; na kwa kuwa alikuwa na hamu ya kuendelea kuwa “Rais wa Nchi” kwa kipindi kingine cha miaka mitano (2010-2015) ilimlazimu kujenga mazingira ya kufanikisha lengo hilo kwa kuwatumia watu (mke, watoto, marafiki, na wana mtandao) ambao sehemu yake ni wale wenye mahusiano ya kifisadi kwenye mfumo na au ndani ya mfumo (systematic and/or systematic corruption networks); kwa hivyo, ilimbidi kiongozi huyo kufunika kombe mwanaharamu apite!

Hii inadhihirika wazi kwenye maamuzi magumu na mazito ya kuwashughulikia mafisadi na kusuasua kwa mashauri yanayohusu ufisadi. Pamoja na hayo, tutosheke kusema kwamba Jakaya Mrisho Kikwete hakuwa ‘rais wa watu” kama walivyotegemea wapiga kura milioni 9.1 (80%) walioempigia kura mwaka 2005; bali alikuwa kiongozi aliyesukumwa na utashi wa kuwa “Rais wa Nchi” kuwakilisha na au kusimamia maslahi ya kundi fulani ndani ya chama chake – “CCM Maslahi”.

Zamani, wakati TANU (na ASP) inaanzishwa, na hatimaye CCM inazaliwa, lengo kuu la chama lilikuwa: “kujenga jamii ya watu waliyo sawa na huru”. Chama (CCM) kilisisitiza kwamba, “Serikali ya wananchi lazima itumie mali yote ya nchi yetu katika kuondosha umaskini, ujinga, na maradhi”.

Kama kiongozi mkuu wa nchi anayetokana na chama chenye lengo hili, ilimlazimu kuhakikisha kwamba “maisha bora kwa kila Mtanzania” yanazingatia matumizi mazuri na endelevu ya rasilimali za Tanzania katika kujenga mujtamaa mzuri wa maisha ya wananchi wa Tanzania kiuchumi, kisiasa, na kijamii.

Jakaya Mrisho Kikwete ameshindwa kufikia malengo ya walioempigia kura mwaka 2005. Kiongozi huyu ameonekana kuwa msaliti wa dhamiri za wananchi waliomuamini kwa kukosa “uoni angavu” wa kuwatumikia wananchi na badala yake kulitumikia kundi la watu wachache wenye uchu wa kuwekeza na kuzitumia rasilimali za Tanzania kwa manufaa ya kibinafsi.

Ushahidi wa kukata tamaa kwa wananchi wa Tanzania unaweza ukakokotolewa na au ukapatikana kwenye udondozi wa mchakato wa uchaguzi na matokeo ya Uchaguzi Mkuu, 2010.

Ni hivi: Jakaya Mrisho Kikwete, alipewa nafasi ya kipekee na chama chama chake kugombea urais kwenye kinyang’anyiro cha urais. Kwa kuwa alikuwa rais aliyepo madarakani na aliyedhaniwa kuwatumikia wananchi kwa utashi wa wananchi katika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, tulitegemea apate ushindi wa “tsunami” kama alivyokuwa akijinadi na chama chake!

Pamoja na kujulikana nchi nzima, CCM ya Jakaya Mrisho Kikwete ilitumia rasilimali nyingi (watu, vitu, na fedha) hata kuliko walivyotumia kwenye Uchaguzi Mkuu, 2005.

Pamoja na matumizi ya rasilimali za chama na michango wa wafadhili wa chama hicho (wafanyabiashara matajiri), Jakaya Mrisho Kikwete na chama chake wametumia taasisi za umma, viongozi waandamizi wa serikali, mali na vifaa vya serikali katika kuhakikisha ushindi kwa Jakaya Mrisho Kikwete na ushindi kwa CCM.

Hata hivyo, ushahidi wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu, 2010 unaonyesha Jakaya Mrisho Kikwete amepata ushindi mwembamba! Si mwembamba kwa uwiano wa asilimia, hasha; ni mwembamba kwa mujibu wa idadi ya waliyempigia kura ikilinganishwa na 2005.

Idadi ya kura alizopata Jakaya Mrisho Kikwete zinakadiriwa kufikia 5,276,827 (kama milioni 5.3 hivi) sawa na asilimia 61.17 (tuseme 61%) inayoafikiana na asilimia 27 ya wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura.

Ushindi huu wa kiongozi huyu si tu unaonyesha jinsi wapiga kura walivyopungua bali pia unaonyesha jinsi umma ulivyomkataa! Hii ni ishara mbaya kwa kiongozi aliyekuwa na “mvuto wa ajabu”.

Kama tutatumia hesabu za takwimu na hatimaye kuchambua na kuchanganua taarifa za matokeo ya kura za 2005 kwa ulinganifu wa kura za 2010 tunaweza kupata ukokotozi ufuatao.

Tuseme, kura milioni 9.1 (za 2005) tuzilinganishe kwa kura milioni 5.3 (za 2010) tunapata tofauti ya kura milioni 3.8; na tukizitafutia asilimia yake kwa kigezo cha kura alizopata 2005 ni sawa na asilimia 41.76 (tuseme 42%).

Kwa jinsi hii, Jakaya Mrisho Kikwete ameporomoka kwa asilimia 42! Hili ni “anguko” kubwa kwa kiongozi aliyekuja kwa mbwembwe za kuwaletea wananchi “maisha bora” kisha akashindwa kutimiza matumaini ya waliompigia kura.

Kutokana na ukweli wa takwimu za kura alizopata mwaka 2005 na alizopata 2010 zikilinganishwa na jinsi mgombea huyo na chama chake walivyotumia “nguvu za ziada” katika kuendesha kampeni ghali ni wazi kuwa umma wa wananchi wengi umemkataa. Kama umma wa wananchi umemkataa, lazima tujiulize: ni vipi anaweza akawakilisha masilahi ya wananchi wa Tanzania?

Kwa kuwa CCM ilishakuwa na mtaji wa kura takriban milioni 4.5 (pungufu au ziada) kutokana na wanachama wake nchi nzima, ni wazi kwamba kama tukitafuta tofauti ya kura alizopata Jakaya Mrisho Kikwete kutoka kwa wapiga kura ambao si wanachama wa CCM ni takriban milioni 0.8 (laki nane) sawa na asilimia 5.12 (tuseme 5%) ya waliojiandikisha kupiga kura 20,137,303.

Hii inaonyesha wazi kuwa wana CCM ndio waliomchagua Jakaya Mrisho Kikwete na kwa jinsi hiyo, “Jakaya Mrisho Kikwete ni Rais wa CCM; kwa jinsi hiyo umma umemkataa.”

Wakubali wakatae, huu ni uhalisia wa hesabu za takwimu na ukokotozi wa taarifa za kura zikilinganishwa kwa mwaka 2005 kwa kigezo cha mwaka 2005. Kama ilivyo kawaida ya takwimu na kwa mujibu wa Profesa Yule, “takwimu hazidanganyi, isipokuwa watu hudanganya.”

Inawezekana CCM na baadhi ya makada wake “uchwara” wakacheza na takwimu hizi ili kuwahadaa wananchi na au wanachama wao! Kwa kuwa njia ya muongo ni fupi, kivumbi cha “anguko la CCM” lililoonekana 2010 kitaendelea kukitafuna chama hicho na kuna kila sababu ya kusema kwamba, “kila uongo ni wenye kujirudia”; na ahadi za 2010 zitakimaliza chama hicho.




SOURCE

No comments: