Wednesday, November 10, 2010

Kwa ushindi huu, JK hawezi kucheza 'Kiduku'

Joseph Sabinus




BUNGE lililopita, limepita. Japo lilikuwa na changamoto nyingi, lakini liliwaliza Watanzania. Watanzania wamelia; kila mmoja kwa sauti na machozi ya aina yake.

Wamelia kama vile wangekuwa watoto yatima wasio na mwangalizi, mtetezi wala mwakilishi, lakini walikuwa na wawakilishi wao; walikuwa na wabunge wao.

Walikuwa na wabunge ambao ni watetezi na wawakilishi walioomba kuwawakilisha Watanzania huku mikono yao ikiwa nyuma kama tulivyoona katika kampeni zilizomalizika hivi karibuni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Ili kuonyesha kuwa ni wakarimu na watu wa watu, wengine wakadiriki hata kutoa shikamoo na kupiga magoti mradi tu, waonyeshe unyenyekevu, upendo na uwakilishi dhidi ya wapiga kura wao wakati wakiomba kura.

Wengine katika harakati za kuomba kura, waliangua hata vilio vya kuonyesha uchungu kwa taifa lao huku wengine wakicheza “kiduku” kama ishara ya kujichanganya na jamii.

Huu ni wosia kwa wabunge wapya wa Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania. Wabunge walioapa kwa paa na ayara wa porini, kuwalinda na kuwatetea Watanzania bila ubinafsi, woga wala ubaguzi; wakasema, NITUME MIMI nao Watanzania wakasema, “Nendeni mkaitangaze Injili… Muwe watu wa kutumikia na sio kutumikiwa.”

Wabunge wapya wakumbuke kuwa, Bunge lililopita lilikuwa ni sawa na mbwa mkali mwenye afya, lakini mwenye meno ya plasitiki; kama yale ya watoto wachanga yanayong’olewa kliniki.

Ikumbukwe kuwa, si kwamba wabunge wote walikuwa wakifurahia kuwa na meno ya plastiki, bali walibanwa na ugonjwa wa uchama; wakasahau kuwa mbunge safi anatambua wajibu wake mkubwa kwamba ni kwanza, kwa taifa, kwa jimbo lake la uchaguzi, kwa chama na ikibidi sasa kwake au kwa familia.

Wenzetu maslahi ya taifa iliachwa kuwa kitindamimba, na maslahi binafsi na ya chama ikawekwa mbele. Hii ilikuwa mithili ya mchezo wa sarakasi; kichwa chini miguu juu.

Wengi walikuwa wakidhani mwaka 2010 ni mbali na hata wakajisahau na kila mmoja miongoni mwa wegi, akajitengenezea kadunia kake na kujivisha umungumtu.

Huu ni umungumtu wa kupenda kutumikiwa kuliko kutumikia, umungumtu wa kupenda kula hadi kuvimbewa na kukaribia kutapikia soksi, huku wengine wakikosa hata uji wa muhogo usio na ndimu.

Bajeti zikapita na kupigiwa makofi kuwa ni nzuri, lakini ni mtihani mzito kwa wabunge nchini maana ukipenda kichuguu, penda na matope yake na pia, ukipenda boga, penda na ua lake.

Walianza kwa mkwara lakini mwishoni, bajeti zote nzuri na mbaya zikapita bila kupingwa na palipoibuka hoja, bunge likakimbilia kupiga kura ili demokrasia iseme, “wengi wape”. Safari hii, hilo halitaluwa na nguvu maana wabunge wa upinzani ni wengi.

Ilikuwa hivyo maana kilichokuwa kikilindwa ni uchama na sio utaifa. Kwamba hoja ya mwana CCM mwenzetu lazima ipite, kumbe hiyo ni hoja ya kuwaua Watanzania wenzetu, lazima ipite.

Matokeo yake, kila mwaka maisha yakazidi kuwa magumu kuliko mwaka jana. Uchache wa wabunge wa kambi ya upinzani, ukatumiwa na baadhi ya wabunge wa chama tawala kujinufaisha na kukinufaisha chama chao; haijalishi Watanzaia wegi wataubebaje mzigo huo.

Wabunge waliotumwa bungeni na wananchi ili wakawaletee matumaini, wakatetee masilahi ya wapiga kura wao, wakaenda kujipa raha na kujitetea wenyewe mradi tu, wengine ni mawaziri.

Wabunge wengi wakasahau kuwa katu hawakutumwa kwenda kutetea mishahara wala posho nzuri, hawakutumwa kwenda kuchagua mashangingi ya rangi wala aina nzuri; hawakutumwa kwenda kunenepesha tumbo hata zikaribie kudondoka kiasi cha kunusurika kwa msaada wa mkanda wa suruali, bali kuwawakilisha wapiga kura wao; wananchi.

Wabunge wapya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nyie onesheni tofauti; nendeni huko mkijua kuwa Watanzania wamewapa dhamana kubwa. Kumbukeni hata namna walivyokuwa wakishinda njaa na kushindia juani ili kuhudhuria mikutano yenu ya kampeni.

Kumbukeni namna walivyokuwa “wakiwaka” pale wanapodhani kuwa mnadhulumiwa.

Japo utendapo wema ondoka bila kusubiri shukurani, nyie onyesheni moyo wa shukurani na fadhila kwa utumishi na uwakilishi wenu mzuri. Wamewachagua ishara thabiti ya kuwa tayari kushirikiana nanyi kujiletea maendeleo.

Kwa msingi huu, wabunge wapya, mtakapokuwa mnajadili masuala mbalimbali hasa bajeti katika vikao vijavyo fanyeni yanayotarajiwa kufanywa ili Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uwakute mko tayari, maana kesheni mkisali na pia, safari moja huanzisha nyingine.

Nendeni bungeni kwa moyo wa kukubali kutumwa; muwe watumwa wa kutumikia wananchi kwa upendo, sio watumwa wa kujituma kujitumikia na wala msiwe wabunge waliojiandaa kutumikiwa, bali kutumikia umma kwa wakati wote.

Wabunge wanapojadili mambo mbalimbali yanayobeba maslahi ya taifa ikiwamo bajeti wajiulize kuwa, maamuzi wanayoyatoa mathalani kama ni nyongeza ya ushuru katika bidhaa za mafuta ya taa, petroli na dizeli na ada za leseni za magari, wanapunguza au wanachochea sumu ya ukali wa maisha kwa kukata tawi la mti walilokalia!

Wabunge wawe kweli wacha Mungu na wasio wanafiki, kamwe wasiruhusu bajeti na maamuzi machafu kupita bungeni huku wakipiga makofi na kusema naunga mkono kwa asilimia 100, huku wakijua inakwenda kuwaua wapiga kura wao maana wakifa hao, mwaka 2015 nani atapiga kura?

Watanzania waliigundua dosari ya uwepo wa wabunge wachache wa upinzani bungeni. Wameaongeza kiasi kikubwa huku ndani ya wabunge wa chama tawala pia wakiwamo baadhi ambao wametawaliwa na moyo wa uzalendo; unganisheni nguvu muwalinde Watanzania.

Wabunge wapya hasa wa upinzani, nendeni bungeni muoneshe tofauti na mliondolee Bunge ile fedheha ya wabunge kuendekeza kasumba chafu ya kuanza kuchangia hoja bungeni kwa kuainisha mapungufu mengi na makubwa hasa katika bajeti, lakini mwisho wa mchango wao, wanaunga mkono kwa asilimia 100.

Hii ni kusema kuwa, wanaonyesha dosari, lakini wanaunga mkono bila dosari hizo kuondolewa; huu ni mchezo wa kuigiza; ni upuuzi, utoto au uendawazimu.

Kwa mtindo huo, utakuta mapungufu yanabaki palepale; bajeti ibaki ileile, ubovu kama upo na hasa huo waliouona ubaki uleule, ugumu wa maisha ubaki uleule au zaidi, Watanzania wateseke, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ukikaribia, waanze kuonyesha makeke ya kukosoa hata mazuri na kuja kwa maneno matamu ya kuchezea akili za wapiga kura ili warudishwe tena kuzifinyanga akili za watu.

Hapo, wawatafute akinamama wawadanganye kwa chumvi, vitenge na makopo ya mbege na kimpumu huku wengine wakidanganywa kwa kuandikwa namba za kadi zao kwa wajumbe wa mashina.

Uchaguzi Mkuu wa 2015 hauko mbali; umefika, unafika huku ukiwa umebeba ungo kwa ajili ya kuwapepeta wagombea maana wale wabunge safi watakaofanya waliyotumwa, wanasikika na wanaonekana hao, njia ni pana kurudi tena bungeni kutumiza wajibu wao wa kuutumikia umma. Mfano mzuri umeonekana safari hii kiasi kweamba, sungura wengi wamewaangusha tembo wa kisiasa.

Kwa wanaokwenda kutetea mashangingi huku wakitelekeza barabara za maeneo yao ; wanaokwenda kutetea posho na mishahara, njia ya kurudi bungeni itakuwa ngumu na nyembamba mithili ya ile iendayo uzimani.

Wabunge kama hao, mwaka 2015 unawasubiri kwa hamu ili waje; waje na majibu midomoni na mifukoni; majibu ya kweli na ya uongo, walete kauli, ahadi, vicheko na tabasamu za kuchonga. Watakuwa wamesahau na kuendelea kudhani kuwa Watanzania wa sasa bado ni wale wa zama za Mwanzo za Mawe.

Waje wamejiandaa ili wakiulizwa kwanini walibariki bajeti inayowasulibisha Watanzania, watoe majibu; wakiulizwa kwanini waliwaacha Watanzania wakaingia gizani kwa kukosa umeme, wasicheke wala kuleta ukarimu wa kuchonga kwa kukashifu wengine, bali watoe majibu; wajibu hoja.

Wakiulizwa kwanini kilimo kimeuawa na kuzikwa kikiona na kulia mithili ya dagaa, watoe majibu; midomoni na mifukoni kama yapo, waeleze kwanini siku zilizopita walikaa kimya na wengine kwa ujasiri, wakatetea kupanda bei ya mafuta ya taa, petroli na dizeli! Wagombea ubunge wa mwaka 2015 wajiandae kujibu maswali kuwa, watu wakasage katika mashine gani, wajawazito wajifungulie katika pori gani, na pia waeleze kuwa, robo kilo ya unga; nazi na matembele wanajua yanauzwa bei gani kama wataacha kila kitu kipande bei ovyovyo ?

Wabunge wakae bungeni wakijadili bajeti huku pia wakikumbuka kuwa, wakati ukifika wananchi watahoji kama wabunge hao walijua wanachotumwa kwenda kufanya bungeni; waseme kama walitumwa kutafuta unene, umaarufu, mashangingi au kuitwa MHESHIMIWA MBUNGE…

Safari hii, wabunge hao waonyeshe kwa wapiga kura wao; wamesaidia kujenga shule ngapi? Je, zina walimu, vifaa na mazingira bora ya kutolea elimu, au ni idadi ya majengo ya kuombea kura? Waseme na waoneshe!

Watanzania safari hii hawataki takwimu za majengo ya shule na hospitali huku shule zikiwa hazina walimu, vitabu wala maabara. Watanzania hawataki elimu ya ubaguzi tena. Watoto wasome shule mchangnyiko si wengine St. Kayumba na wengine nje ya nchi ili baadaye wasomi waliokwenda nje, waje kurithi nafasi za baba zao.

Hata hivyo, nendeni mkatumikie kiadilifu mkiwa kifua mbele maana jamii imewaamini na kuwapa dhamana. Safari hii Bunge liwasikilize Watanzania. Wabunge wajue wakiwaliza Watanzania wasitarajie kuliona tabasamu la Mungu.


SOURCE

No comments: