Friday, October 29, 2010

Mbowe auteka mji wa Arusha

na Ramadhani Siwayombe, Arusha
MWENYEKITI wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, jana aliuteka kwa muda mji wa Arusha baada ya kupata mapokezi makubwa kutoka kwa wakazi waliofurika kwenye mkutano wa kampeni za chama hicho.

Mbowe jana alihutubia katika viwanja vya NMC, ambapo alitumia nafasi hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, sambamba na kuwaomba wananchi wamchague mgombea urais wa chama hicho Dk. Willibrod Slaa ili maisha ya Watanzania yaboreke.

Akihutubia katika mkutano huo, Mbowe alisema kuwa katika saa 72 zilizobakia Watanzania wanapaswa kufanya maamuzi ya busara kwa kuhakikisha kura zao zinakuwa ukombozi wao kwa kuwachagua wagombea wa CHADEMA ili kufanya mabadiliko ya msingi ambayo yatawawezesha kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

“Ndugu zangu wana wa Arusha saa 72 zimebaki kabla ya nguvu ya kura kufanya maamuzi juu ya maisha yenu ya baadaye pamoja na watoto wenu naomba muipumzishe CCM, ili CHADEMA iweze kuwaletea mabadiliko ya kweli ya kiuchumi na elimu katika nchi hii,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba askari wa Jeshi la Polisi kuipa kura CHADEMA ili ipate fursa ya kuwatumikia na kuwaboreshea maisha yao kwa kuongeza masilahi yao.

Aliwasihi wananchi kuwaacha kupambana na polisi licha ya jeshi hilo kwa hivi sasa kutenda kazi kwa shinikizo la chama tawala kwa kuwa hata askari wanaolitumikia jeshi hilo nao wanahitaji mabadiliko kwa sababu wanakabiliwa na maisha magumu kama walivyo watumishi wengine wa serikali.

“Wana wa Arusha, sisi CHADEMA tunahitaji kura za hawa askari wetu hivyo msigombane nao kwani wao ni sehemu ya wananchi waliopigika na wanahitaji ukombozi wa wetu kuboresha masilahi yao,” alisema Mbowe.

Katika mkutano huo aliwaomba wananchi kumchagua mgombea urais wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, ili chama hicho kiweze kukamata dola ambapo ndani ya siku 100 kiweze kuanza mchakato wa kubadili katiba kwa lengo la kuwapa mamlaka zaidi Watanzania tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo rais amekuwa na madaraka makubwa zaidi.

Alisema madaraka makubwa aliyonayo hivi sasa rais ni kuwa ndiye mwenye uwezo wa kufanya uteuzi wa viongozi wengi wa kitaifa ikiwemo wa majeshi usalama wa taifa, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, hali inayosababisha wengine kuwepo na mwanya wa kuwateua kwa misingi ya kirafiki, kindugu au kijamaa.

Alitoa wito kwa wakazi wa Jimbo la Arusha kutofnya makosa kwa kuchagua mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, kwani kwa Mkoa wa kilimanjaro tayari wao wamemaliza kazi hiyo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mbowe, mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, aliwaomba wananchi kutofanya kosa keshokutwa kwa kuichagua CHADEMA ili iweze kuongoza nchi.

No comments: