Monday, November 23, 2009

Waziri Mkuu azuiliwa kuendelea na msafara -Newala

Tukio hilo lilitokea Jumamosi majira ya mchana wakati Pinda akielekea kwenye bonde la mto Ruvuma kukagua kituo cha maji cha Mkunya na kupokea taarifa ya kilimo cha umwagiliaji kwenye bonde la mto Ruvuma katika ziara yake.


Mara baada ya kufika njiani hapo msafara huo ulikuta njia imefungwa na wananchi wakwia wamekaa kando ya barabara, na hatimaye Waziri Mkuu aliteremka kutoka kwenye gari yake na kuwasikiliza wananchi hao.

Katika mazungumzo yao wakazi hao walisema wana kero ya kutopata maji safi na salama, kutolipwa malipo ya korosho na kutopatiwa pembejeo za ruzuku lakini uongozi wa wilaya umekuwa ukiwapuuza na kuficha taarifa badala ya kuwasaidia.

Walisema kwamba tatizo la uhaba wa maji katika eneo lao limedumu kwa zaidi ya miaka 15 jambo ambalo linawafanya watumie muda mwingi kusaka maji badala ya kuutumia muda huo kwenye kilimo.


Kuhusu mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani, wakazi hao walisema hawautaki kwa sababu hawalipwi fedha zote za Sh. 700 kwa kila kilo kama walivyoahidiwa.


Pia waliiomba Serikali iwasaidie kuwapatia pembejeo na mbolea za ruzuku kwani bei ni kubwa na wengi wanashindwa kuzimudu.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwaahidi wakazi hao kuwa kabla hajaondoka, atakuwa amepata ufumbuzi wa matatizo hayo na kukutana na wahusika mara moja.


Kuhusu mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani, Waziri Mkuu alisema hauna tatizo ila una kasoro ambazo itabidi ziangaliwe upya na kumtaka Mkuu wa Mkoa huo, Kanali (mstaafu) Anatory Tarimo, kujipanga upya na kusambaza elimu ya mfumo huo kwa wakulima.


Kuhusu pembejeo za ruzuku, Pinda alisema atahakikisha anafuatilia suala hilo ili katika mwaka wa fedha ujao, mikoa ya Lindi na Mtwara iingizwe katika programu hiyo.

No comments: