Thursday, November 5, 2009

Waraka wa El-nino wasambazwa

na Hellen Ngoromera




SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, imetoa waraka kwa Halmashauri na wadau wote nchini kuandaa mipango madhubuti ya kukabiliana na mvua za El-nino ambazo zimetangazwa kuwepo nchini mwaka huu.

Ofisa wa Kitengo cha Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Shiyo, alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV cha jijini Dar es Salaam.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, wamezitaka pia mamlaka zote na majiji nchini kuzibua mifereji na mitaro na mambo mengine. Pia wananchi hasa wanaoishi mabondeni kuhama kabla mvua hizo hazijaanza.

Naye Meneja wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Kibavi Tawakal, alisema wameandaa vifaa mbalimbali kama vile mahema, machela na vingine kwa ajili ya kukabiliana na majanga hayo.

“Tuna vijana pia ambao wamejiandaa kukabiliana na mambo haya, tumeandaa vipeperushi kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu El-nino na kwa sasa vinakamilishwa kuandaliwa, tunashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuandaa taarifa sahihi,” alisema Tawakal.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Mohamed Matitu, alisema matayarisho kwa ajili ya kukabiliana na mvua hizo yapo, hivyo wananchi wajiandae vyema. Aliongeza kuwa, mvua za safari hii hazitakuwa kubwa kama zilizowahi kunyesha miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa Matitu, mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa itapata mvua za wastani wakati Singida na Dodoma itapata mvua za kawaida. Hakutaja zaidi kuhusu mikoa mingine.

Aliongeza kuwa, pamoja na kuwepo kwa hali hiyo katika mikoa aliyoitaja, mafuriko pia yanaweza kutokea hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari.

No comments: