Thursday, November 5, 2009

Simba, Yanga zavuna mil. 180/-

na Makuburi Ally




MECHI ya Ligi Kuu namba 57, kati ya Simba na Yanga, iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ambayo iliisha kwa Simba kushinda bao 1-0, imeingiza shilingi 420, 235,000, huku kila timu ikilamba sh mil. 90.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, mapato hayo yametokana na jukwaa la VIP A ambalo kiwango kilikuwa sh 60,000, kuingia watu 388, hivyo kupatikana sh 23,280,000.

Kwa jukwaa la VIP B ambalo kiingilio kilikuwa sh 50,000, kulikuwa na watazamaji 293, hivyo kuingiza sh 14,650,000.

Jukwaa la VIP C, ambalo kiingilio kilikuwa sh 30,000, walioingia ni 1,090, hivyo kuingiza sh 32,700,000, huku jukwaa la rangi ya chungwa ambako kiwango kilikuwa sh 20,000, wakiingia watazamaji 2982, hivyo kupatikana sh mil. 59,640,000.

Viti vya rangi ya chungwa ambavyo kiingilio kilikuwa sh 10,000, jumla ya tiketi 7,241 ziliuzwa, hivyo kupatikana sh 72,410,000.

Mwakalebela, alisema viti vya bluu ambavyo vilitozwa shilingi 7,000, watazamaji walikuwa ni 17,045, hivyo kuingiza sh 119,315,000.

Jukwaa la kijani ambalo kiingilio kilikuwa sh 5,000 ziliuzwa tiketi 19,648, hivyo kupatikana sh 98,240,000.

Kuhusu uuzaji wa tiketi, Mwakalebela alisema zile za sh 5,000 na 10,000 zote ziliuzwa huku baadhi ya mashabiki wakiingia bure, hivyo kupunguza mapato, tofauti na ilivyokuwa imetarajiwa.

Mwakalebela alisema gharama za uwanja ni sh 80,118,040; Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh 3,004,426; gharama za mchezo ni sh 80,118,040.

No comments: