Tuesday, May 19, 2009

Malecela: Busanda CCM maji shingoni

• Awaangukia wafanyabiashara kuiokoa


na Kulwa Karedia, Busanda
MAKAMU Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, John Malecela, maarufu Tingatinga, amekiri kuwa chama hicho kinakabiliwa na upinzani mkali katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Busanda na kwamba sasa maji yako shingoni.

Akizungumza na wafanyabiashara zaidi ya 50 katika soko kuu la mji mdogo wa Katoro, jana, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za ubunge katika Jimbo la Busanda, Malecela alisema hali ya mambo si shwari na kuwaomba kuiunga mkono CCM.

“Nimewatembelea hapa kujua matatizo yenu pamoja na kuwaambia kwamba, tunakabiliwa na uchaguzi ndani ya jimbo hili, nawaomba mtumie fursa hii kuchagua CCM ili iweze kumaliza matatizo madogo madogo yaliyopo,” alisema.

Malecela ambaye alifika sokoni hapo majira ya saa 7 mchana akiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser, yenye namba za usajili T 509 AFZ, aliwataka wafanyabiashara kutobabaishwa na sera za vyama vingine.

Kauli ya Malecela ilionekana kuwa mwiba mchungu kwa wafanyabiashara hao ambao waligeuka na kumweleza kuwa umefika wakati wa kufanya mabadiliko.

“Tunasema kama CCM mnasema maji yamefika shingoni, tunasema ni haki yenu kwani sisi tukiingia humo tutazama, sasa kwanini tujitafutie matatizo hivyo,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao, Marando Mayalla.

Alisema kwa kipindi kirefu CCM imetumia mwanya wa kuwadanganya katika masuala mbalimbali ya kijamii, ikiwamo ahadi ya kupelekewa umeme, lakini imeshindwa kutimiza.

“Tumekuwa watu wa kudanganywa kila mwaka sisi… tumeahidiwa umeme hapa miaka mingi, leo tena mnakuja na sera eti ya kuwachagua, tunasema kila jambo lina mwanzo na mwisho wake,” alisema Mayalla kwa niaba ya wenzake.

Alisema hata kitendo cha CCM kumrejesha mmoja wa wanasiasa maarufu wa chama hicho, aliyegoma kupanda jukwaani, Donald Maxi, hakutasaidia kitu kwani mwenyewe amejimaliza kisiasa.

“Sisi tunasema hata huyo Maxi ambaye mmeamua kumrudisha CCM kwa ajili ya kusaidia kampeni, amechemsha kwani huko ni kujimaliza kisiasa... inakuwaje agome kupanda jukwaani mpaka rais aaingilie kati?” alihoji Mayalla.

Kutokana na kauli za wafanyabiashara hao, Malecela aliamua kuondoka eneo hilo, huku akinyonyeshewa vidole kwa alama ya V ambayo hutumiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika kupeana salamu za chama.

Tangu CCM ilipozindua kampeni zake, imekuwa na wakati mgumu kutokana na viongozi wake kuzomewa karibu mikutano yote inayofanywa hali ambayo imesababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe anatarajiwa kuwasili leo jimboni hapa na kuanza kutumia helikopita kumnadi mgombea wa chama hicho, Finias Magessa.

Ratiba inaonyesha kuwa, Mbowe anatarajiwa kufanya mikutano saba kwa siku moja ambapo ataanzia katika viijiji vya Rwamgasa, Kaseme, Katoro na Ibondo kwa nyakati tofauti.

Katika hatua nyingine, vijana wa CCM, maarufu kama Green Guard, jana waligeuza Kijiji cha Nyachilulula kuwa uwanja wa vujo baada ya kutembeza kipigo kwa baadhi ya wafuasi wa CHADEMA.

Tukio hilo ambalo limeonekana wazi kubadili sura ya kampeni, lilitokea majira ya saa 5:40 asubuhi kijijini hapo wakati CCM ilipokuwa ikimnadi mgombea wake, Lolencia Bukwimba, ambaye amekuwa na wakati mgumu kutokana na kuzomewa kila anapopanda jukwaani.

Tangu CCM walipofanya mkutano wao katika Kijiji cha Katoro wiki iliyopita, wamekuwa wakitumia vijana wa Green Guard kukamata na kuwapiga vijana wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa vyama vya upinzani, jambo ambalo limezua malalamiko mengi.

Wakati mkutano huo wa Nyachilulula ukiwa unaendelea, vijana watatu ambao wanasaidikiwa kuwa ni wafuasi wa CHADEMA, walipita karibu na eneo la mkutano, huku wakipeperusha bendera ya chama hicho.

Vijana hao wakiendelea na safari, walishitukia wakifuatwa na gari aina ya Toyota Prado, yenye namba za usajili T 718 na waliokuwamo ndani kushuka ghafla na kuanza kuwapiga.

Waliopigwa ni pamoja na Chacha Magabe na Lucas Tigamanya ambao baada ya kipigo hicho haikujulikana mara moja walipelekwa wapi.

Wakati tukio hilo linaendelea, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, alikuwa jukwaani akimnadi mgombea wa CCM.

Hata hivyo, lawama nyingi zimeelekezwa kwa Jeshi la Polisi kwani hawahudhurii mikutano mingi ya kampeni.

Mmoja wa wanakijiji wa Nyachilulula, Mabula Shijja alisema amesikitishwa na kitendo cha CCM kupiga watu kila wanapofanya mikutano.

“Hii ni tabia mbaya kwani CCM sasa wamekuwa na tabia ya kupiga watu kila wanapofanya mkutano, juzi tumeshuhudia pale Katoro watu walivyopigwa vibaya na kuswekwa ndani,” alisema Shijja.

Alisema umefika wakati hatua za haraka zichukuliwe ili kudhibiti hali hiyo ambayo inavunja misingi ya demokrasia.

Akimnadi mgombea wake, Kilango aliwataka wakazi wa Kijiji cha Nyachilulula, kutumia fursa ya kuchagua kiongozi bila ya shinikizo lolote la kisiasa.

“Tumieni fursa yenu kuhakikisha kwamba mnachagua kiongozi ambaye mnamtaka, msibabaishwe na vita ya mafisadi inayoendelea ndani ya chama chetu.

“Ni ukweli usiopingika kwamba ndani ya chama changu kuna baadhi ya wananchama na viongozi wanaojihusisha na ufisadi, lakini si wote,” alisema Kilango.

Katika hatua nyingine, askari polisi zaidi ya 45 ambao wamepelekwa jimboni Busanda kwa ajili ya shughuli za ulinzi, wamelalamikia posho ya sh 1,000 ambayo wanalipwa kwa siku.

Wakizungunza jana mjini hapa, na kuomba majina yao yasitajwe gazetini, askari hao walisema kiasi hicho ni kidogo ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

“Hata wewe fikiria kwamba tumeacha familia zetu, ndugu yangu tunalipwa sh 1,000 kwa siku, unadhani inaingia akilini? Basi ndiyo hivyo tena, hatuwezi kulalamika kwa wakubwa,” alisema mmoja wa askari hao.

No comments: