Tuesday, May 27, 2008

MKAPA, MRAMBA, MEGHJI



Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, mwanasheria maarufu nchini Mabere Nyaucho Marando alisema kuwa ingawa kifo cha Ballali kimefanya ushahidi upungue kwa vile hakuongea ama kuhojiwa, haizuii kufanyika kwa uchunguzi kwa vile vitabu vipo vinavyoonyesha jinsi pesa zilivyoondolewa benki na zilipokwenda.

Aidha, alisema kuwa lazima aliyekuwa Rais kipindi hicho, Bw. Benjamin Mkapa na waliokuwa Mawaziri wa Fedha, Basil Mramba na Zakia Meghji pamoja na Andrew Chenge ambaye alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali waingie matatani kufuatia ubadhirifu huo wa mabilioni ya pesa.

Aliongeza kuwa haiwezekani hata kidogo ubadhirifu wa kiasi hicho kikubwa cha pesa ukatokea wakati kuna viongozi wa nchi waliopewa dhamana, washindwe kuzuia ama kujua zilipokwenda.

‘’Unajua kuwa viongozi hao niliowataja lazima wahojiwe polisi waeleze pesa hizo zilipokwenda kwa kuwa haziwezi kuondolewa benki bila wao kuidhinisha ama kujua, hivyo kwa namna nyingine wanajua kilichofanyika, kwa maana hiyo serikali isije ikatafuta njia ya kudhoofisha uchunguzi huo kwa kuwa Dk. Ballali hayupo (amekufa),’’ alisema Marando.

Hata hivyo, mwanasheria huyo wa siku nyingi alisema kuwa kunahitajika uchunguzi wa kina na baadaye wananchi waelezwe ukweli kuhusiana na sakata hilo kwa kuwa hivi sasa kila mwananchi ameamka na analifuatilia kwa ukaribu suala hili kiasi kwamba hakuhitajiki kupinduliwapinduliwa.

‘’Rais Jakaya Kikwete asipokuwa mkali katika hili na mambo mengine ya kifisadi yanayoendelea kufanyika nchini ni wazi kwamba atajipunguzia imani kwa wananchi, ‘’ alisema Marando.

Naye Ofisa Habari wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Omega Ngole alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa uchunguzi kuhusiana na ubadhirifu huo unaendelea kama kawaida na kwamba kifo cha Ballali hakiathiri chochote.

Ballali aliyezikwa Ijumaa iliyopita jijini Washington DC katika makaburi ya Gate of Heaven, anadaiwa kulishwa sumu na watu madai ambayo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe amekanusha lakini familia imesema itazungumzia suala hilo wakati wa arobaini ya marehemu itakayofanyika Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu alisema wiki iliyopita kuwa madai kwamba Ballali kauawa kwa sumu hayana maana yoyote kwa kuwa inajulikana alikuwa mgonjwa.

Mapema mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alimfuta kazi Marehemu Ballali kutokana na upotevu wa shilingi bilioni 133 za EPA na akaunda timu ya watu watatu inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika kuchunguza tuhuma hizo ili ifikapo Juni 9, mwaka huu iwe imeshamaliza kazi hiyo na kukabidhi ripoti kwake.

No comments: