Tuesday, May 27, 2008

Mamaye Ballali alindwa

na Kulwa Karedia



HALI ya ulinzi mkali imeimarishwa nyumbani kwa mama mzazi wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) marehemu Daudi Ballali.

Habari za kuaminika zilizopatikana jana nyumbani kwa mama huyo Boko, Dar es Salaam, zinasema kuwa ulinzi huo umewekwa na serikali kupitia BoT tangu kutangazwa kwa kifo cha Ballali wiki iliyopita.

“Tumesikia ulinzi huu umewakwa na serikali kwa kushirikiana na BoT kwamba hakuna mtu yeyote kuingia hapa, tunashangaa sana kuona hata sisi ambao tumekuwa naye hapa tumebaki kuwa watazamaji tu,” alisema Seif Omar, mkazi wa Boko.

Alisema kitendo kilichofanywa na serikali si cha kiungwana, kutokana na ukweli kwamba msiba huwa hauchagui maskini au tajiri wa kwenda kuzika mwenzake au jirani yake.

Tanzania Daima jana ilipofika nyumbani kwa mama huyo anayeishi nyumba namba BNJ/BOKO/1081, ilishuhudia hali ya ulinzi mkali, kitendo kilichosababisha hata mwandishi wa habari hizi kuzuiwa kuingia ndani.

Baada ya kuwasili nyumbani, mmoja wa walinzi wa Kampuni ya Regimental Security aliyekuwa getini, alikataa katakata kufungua geti hilo kwa madai kuwa amepewa maelekezo kutoka ngazi za juu serikalini na BoT.

“Nikusaidie nini, unaitwa nani na una shida gani ndugu…tafadhali nionyeshe kibali chako cha kuingia humu ndani kutoka BoT, na kama huna, nakuomba uondoke eneo hili,” alisema mlinzi aliyekataa kutaja jina lake.

Alisema yeye amepewa maelekezo hayo na maofisa wa juu wa BoT, ambao hakuwa tayari kuwataja majina na kusisitiza kuwa anatekeleza majukumu yake ya kazi.

“Nashindwa jinsi ya kuwasaidia…jamani nawaomba sana muondoke hapa,” alisema mlinzi huyo na kuendelea kufunga geti hilo, kitendo kilichoashilia kuna shinikizo kutoka juu.

Juhudi za gazeti hili kumuona mama mzazi wa Ballali ziligonga mwamba kutokana na hali ya ulinzi iliyopo.

Wakati huo huo, baadhi ya wananchi waliohojiwa na Tanzania Daima kuhusiana na kauli ya serikali juu ya kifo cha Ballali wamesema serikali inapaswa kueleza ukweli baada ya kuuficha.

“Tumeshangazwa na kauli ya serikali, tunaelewa wazi kwamba Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, atakuwa ameelewa ukweli, sasa kwa nini atufiche?” alihoji Dickson Juma.

Alisema kama kifo hicho kisingekuwa cha siri, kwanini serikali ilipata kigugumizi kusema ukweli kuanzia ugonjwa wake hadi anafariki, jambo ambalo linazua maswali mengi.

“Sisi tunasema umefika wakati sasa wa kuelezwa ukweli na kama sivyo, basi iundwe tume haraka kabla ya mambo haya hajapoa, maana tunajua yakipoa, ndiyo yamekwisha,” alisema Juma.

Naye Mwanakombo Hussein alisema kitendo cha serikali kushindwa kushiriki katika mazishi ya Ballali kinaonyesha wazi kwamba kuna matabaka ndani ya viongozi wa serikali.

Aliwataka wananchi wote kuungana na kuishinikiza serikali ili kuhakikisha inaunda tume huru kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina na majibu yatolewe haraka.

Marehemu Ballali alifariki dunia Mei 16 jijini Washington, Marekani, alikokuwa akipata matibabu tangu mwaka jana, baada ya kufukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete, baada ya kuhusishwa na ufisadi katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ambako zaidi ya sh bilioni 133 zinadaiwa kupotea.

No comments: