Monday, May 19, 2008

Israel nchi yenye raha na machungu


Kaanaeli Kaale
Daily News; Monday,May 19, 2008 @00:05


Mwandishi wa HabariLeo, Kaanaeli Kaale akiwa na kundi la wanajeshi vijana wanaolinda eneo la kitalii ambalo Yesu alizikwa.
Habari nyingine
Israel nchi yenye raha na machungu
Wadau wakataa maombi ya kupandisha bei ya maji Mbeya
Mapinduzi Culture Troop chachu ya maendeleo ya jamii Morogoro
Binti aliyezaa na baba yake watoto saba
PPF Shirika linalofikiria mbele zaidi
Athari za kutomnyonyesha mtoto maziwa ya mama
Kombe la Taifa liwe mgodi wa vipaji
Ngoma za Asili fahari ya Utamaduni wa Mtanzania
Gofu sasa mchezo wa watu wote
Kukosa umakini, kitanzi cha wasanii wa bongo

UKIBAHATIKA kwenda katika nchi ya Israel, hakika utajiuliza maswali mengi, ambayo majibu yake hayawezi kupatikana kwa haraka. Maswali hayo yanatokana na mitazamo tofauti, kuhusu nchi hiyo. Watu wengi hususan Wakristo, wanaamini kuwa Israel ni nchi Takatifu.

Pia wapo wanaodhani kuwa vita kati ya Waisrael na Wapalestina, vinasababisha watu kuwa na maisha ya huzuni kwa miaka yao yote. Chriss Thomas (38) ni miongoni mwa wageni waliopata mshtuko, baada ya kufika Israel na kukuta watu wakiwa na maisha ya kawaida, kama ilivyo katika miji mingine mikubwa sehemu mbalimbali duniani.

“Kwa kuwa Israel ni nchi Takatifu, nilidhani kuwa wanawake huvaa nguo ndefu mithili ya watawa, lakini naona hapa wasichana wanavaa kaptula fupi sana na sehemu kubwa ya miili yao iko wazi…..jambo hili limenishtua sana,” Thomas anaeleza. Anasema hayo muda mfupi baada ya kutoka nje ya Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion katika Mji wa Tel Aviv.

Thomas ambaye ni raia wa Kenya, anasema kuwa alikuwa akiamini kuwa nchi ya Israel haina walevi, makahaba wala watu wanaojiingiza kwenye matendo maovu, kwa kuwa nchi hiyo ni Takatifu.

“Pia nilidhani Israel hakuna maeneo ya starehe, kama vile baa na kumbi za disko, lakini naona vitu hivyo vimepewa kipaumbele na vijana wa hapa wanastarehe kuliko walioko kwenye miji ya Nairobi, Dar es Salaam na Kampala kule Afrika Mashariki,” Thomas anaeleza.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje Israel, Emanuel Seri, anasema kuwa nchi hiyo ni ya kidemokrasia na inazingatia misingi ya haki, hivyo watu wanafanya kila kitu kama ilivyo katika nchi nyingine.

“Hapa watu wanaruhusiwa kuvaa wapendavyo….Waisrael wanaheshimu tamaduni za jamii nyingine na wanavumiliana ili kudumisha demokrasia…hapa kuna tamaduni tofauti na watalii wengi wanafika kutoka sehemu mbalimbali duniani,” anasema Seri. Katika Mji wa Tel Aviv watu hunywa pombe, kuvuta sigara na kukesha katika majumba ya starehe wakila na kucheza.

Mji huo ni kimbilio la vijana wanaopenda starehe za kupindukia. Pia, vijana wanaojiingiza katika tabia ngumu, kama vile mashoga na wasagaji, hukimbilia katika mji wa Tel Aviv ambako vitendo hivyo vinaruhusiwa.

Vijana wa mji wa Tel Aviv hupenda kuwatania wenzao wa mji wa Yerusalem, kuwa ni wavivu na kazi yao ni kunywa maziwa nyakati za jioni na kulala usingizi mzito. Pia, vijana wa Yerusalem wanauelezea mji wa Tel Aviv, kama mji wa anasa, wenye watu wanaojua kula na kucheza nyakati za usiku, kisha kulala nyakati za mchana.

Kwa ujumla, maisha ya Waisrael ni ya kawaida, siyo kama baadhi ya watu wanavyodhani, kuwa wamefungwa na sheria za kidini. Ingawa nchi hiyo inakabiliwa na vita vya muda mrefu, Waisrael wanaendelea na shughuli zao za kila siku bila kujali milio ya mabomu na risasi zinazolia upande wa pili wa mji.

Seri anasema kuwa Waisrael wana kiwango kikubwa cha uvumilivu na wanamudu maisha katika mazingira ya kivita.

Watoto wanakwenda shule kama kawaida na kama darasa moja, litaharibiwa kwa bomu, wanahamia darasa lingine na kuendelea na masomo kama kawaida. Hali kadhalika, kwa watu wazima, nyumba ya jirani ikilipuliwa kwa bomu, askari wanafika haraka kuokoa majeruhi, lakini majirani wanaendelea na shughuli zao.

“Hapa jirani anapatwa na msiba, lakini siwezi kwenda…ninaendelea na shughuli zangu kama kawaida, siwezi kuhudhuria mazishi...na kama nikipata nafasi ninaweza kumpigia simu kumpa pole…kusema kweli hatuna muda wa kuomboleza,” anasema Myahudi mmoja, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Israel ilipata uhuru miaka 60 iliyopita, lakini hakuna siku imepita bila Waisrael kusikia milio ya bunduki au mabomu, kutokana na vita vya muda mrefu. Maisha hayo ya vita, yamewafanya Waisrael kutokuwa waoga.

Wanapanga mikakati ya maisha na kufanya mambo ya maendeleo, bila kujali kama ipo siku watakufa au nyumba zao kuteketezwa na silaha za kivita. Balozi Dan Shaham anasema kuwa Waisrael wanajituma na wanafanya shughuli nyingi za maendeleo, lakini waandishi wa habari wanafumbia macho maendeleo ya nchi hiyo na kuandika habari za vita pekee.

“Hapa Israel watu wana maisha ya kawaida…ingawa kuna vita, tumepiga hatua kubwa katika masuala ya kilimo, uvunaji wa maji na masuala ya tiba, lakini waandishi wa habari hawaoni hayo, wakati wote wanaandika masuala ya vita na kuifanya dunia kuamini kuwa Israel ni sehemu ya vita,” anasema Shaham.

Ingawa Israel ina ulinzi wa hali ya juu, wanajeshi wa nchi hiyo wanaonyesha upendo na urafiki mkubwa kwa wananchi na wapita njia.

Tofauti na wanajeshi wa Tanzania, ambao mtu wa kawaida hawezi kuwapiga picha, wanajeshi wa Israel wanakubali kupigwa picha na kupiga picha na wapita njia. Vijana wa kijeshi wanaweza kuweka kambi katika maeneo yenye watu wengi au katikati ya miji.

Wanapokuwa katika malindo, hukaa kwa starehe mithili ya vijana wa kawaida wanaojipumzisha ufukweni, lakini wao hubeba silaha nzito za kijeshi. Vijana hao wa kijeshi wanasema wanafurahia maisha na kubwa zaidi wanajivunia kulinda nchi yao, hivyo ni lazima waonyeshe upendo kwa raia ili kujenga mazingira ya utulivu.

“Nilitoka nchi za mbali kuja katika nchi ya ahadi, kwa lengo la kuungana na Wayahudi wenzangu kujenga Taifa la Israel…hata kama hapa pana vita, siwezi kuondoka na sasa nimejiunga na jeshi ili kuongeza ulinzi dhidi ya Waisrael, “ anasema mwanajeshi, ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Hata hivyo, wanajeshi hao hawapendi kuzungumza kwa muda mrefu na raia. Ikiwa mwandishi wa habari atachukua muda mrefu, kuzungumza na mmoja wa wanajeshi hao, wanapeana ishara wote kushoto au kulia, jambo linalomlazimu mwandishi aondoke.

Nchi ya Israel ina makundi matatu ya kijamii, ambapo kundi la Wayahudi linachukua asilimia kubwa, kilifuatiwa na kundi la Waarabu kisha la Wapalestina. Ingawa hapa Tanzania ni rahisi kumtambua mwanamke wa Kiislamu, kutokana na mavazi yao, wanawake wa Kiislamu katika nchi ya Israel, wanavaa nguo za kawaida, hivyo ni vigumu kwa mgeni kuwatofautisha na wanawake wa makundi mengine.

“Hapa wanawake walioshika dini, wanavaa nguo ndefu, lakini sio rahisi kwa mgeni kutofautisha wanawake wa Kiarabu, Kiyahudi na Kipalestina…sisi wenyeji ndio tunaweza kuwatambua, wakati mwingine mavazi yanatofautiana kwa rangi tu,” anasema Shlomit Sufa.

Sufa ambaye ni Katibu wa Idara ya Masuala ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, anasema kuwa ipo tofauti kubwa baina ya utamaduni wa wanawake wa Kiyahudi, Kiarabu na Kipalestina. Lakini, hakuwa tayari kuelezea jinsi ya kuwatambua wanawake hao.

Ingawa Waisrael wamekuwa katika vita kwa muda mrefu, wana utamaduni wa kuheshimiana na kila mmoja anaheshimu mila na utamaduni wa jamii nyingine. Hata hivyo, hawachanganyiki sana, kutokana na ukweli kuwa kila jamii ina dini yake, tofauti na Tanzania ambako watu wa kabila moja wanaweza kuwa na dini tofauti. Kwa upande wa Israel, Wayahudi wana dini yao na masoko yao.

Asilimia kubwa ya Waarabu ni waumini wa dini ya Kiislam na wana masoko yao, wakati Wapalestina ni wafuasi wa Kristo na katika hali ya kawaida hawachanganyiki na Wayahudi.

No comments: