Tuesday, April 1, 2008

Vilio Mirerani


Watu hao walifariki dunia baada ya kufukiwa na vifusi wakiwa katika mashimo ya madini kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko katika eneo hilo la Mererani.

Mpaka tunakwenda mitamboni maiti sita zilikuwa tayari zimeshaopolewa na kati ya hizo nne zilikuwa zimetambuliwa ambazo ni za Nelson Mmari, Yuda Sebastiani, Yona Paul na mwingine aliyetajwa kwa jina moja tu la Mushi.

Mmoja wa watu walionusurika katika ajali hiyo, Edward Dodosya alisema kuokoka ni kama bahati tu na wala haoni kama ni ushujaa.

“Ni bahati tu kwa sababu niliona maji yakiingia kwa wingi shimoni nami nikaamua kutoka nje kuona kuna nini. Wakati natoka nilikutana na maji mengi sana nikajua kuwa nje kuna mvua nyingi.

“Nilijitahidi kuyapangua maji hayo ingawa yalikuwa yakinisukuma kutaka kunirudisha shimoni, niliweza kutoka nje nikiwa hoi, namshukuru Mungu,” alisema Edward.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekifu alisema jana kuwa serikali imeunda kamati maalum yakushughulikia zoezi la uokoaji ambayo inaongozwa na Kamanda Venance Tossi wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

Alisema serikali imeagiza pampu maalum kutoka Kenya kwa ajili ya uokoaji na kuongeza kuwa katika ajali hiyo watu 166 wamepotea ndani ya mashimo yaliyokumbwa na mafuriko, waliokolewa ni 93, ambao hawajulikani walipo ni 67 na sita wamepatikana wakiwa wafu.

Mawaziri watatu, Philip Marmo (Sera, Bunge na Uratibu) Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Laurence Masha wapo mkoani Manyara kutathmini maafa ya mafuriko hayo.

Watu walionasa katika mashimo hayo wanahofiwa kufa kutokana na harufu kali inayotoka katika mashimo hayo ya madini.Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Peter Pinda amewataka mawaziri hao watathimini hali ilivyo na baadaye kutoa taarifa itakayoiwezesha serikali kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo.

Mafuriko hayo yalitokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita Machi 29, 2008 na kusababisha maji kuingia katika machimbo ya madini, hivyo, kusababisha maafa hayo.

No comments: