Thursday, April 10, 2008

Mwanaume aliyepachikwa mimba aliwahi kuwa miss


Thomas Beatie (34) ambaye ana mimba ya miezi sita aliyoipata kwa njia ya kupandikizwa mbegu za uzazi kwa sindano, aliyasema hayo wakati akihojiwa katika kipindi maarufu cha luninga kinachoendeshwa na mwanamama machachari, Oprah Winfrey, “The Oprah Winfrey Show” Alhamis iliyopita.

Beatie alisema kuwa wakati akiwa na umri wa miaka kumi, baba yake alikuwa akimhimiza kuwa mwanamitindo na hatimaye akafanikiwa kuwa “Miss Hawaii Teen USA”.

Akionekana kutokuwa na wasiwasi wowote wala dalili ya kujutia uamuzi wake huo, Beatie alisema kuwa yeye bado ni mwanaume imara na anaona kuwa suala la kutamani kuwa na mimba ni jambo la kibinadamu.

“Mimi ni binadamu na nina haki kabisa ya kuwa na mtoto wangu mwenyewe,” alikaririwa akisisitiza
Beatie, mtu ambaye amezua mijadala miongoni wa wanamaadili na wanaharakati wa mambo ya familia.

Beatie alifanyiwa upasuaji kumbadili kuwa mwanaume miaka kumi iliyopita, ambapo aliondolewa matiti yake lakini aliamua kubaki na viungo vya uzazi vya kike kwa sababu alikuwa na ndoto ya kuzaa mtoto baadaye.

Mke wa Beatie aitwaye Nancy alisema kuwa majukumu katika familia hayatabadilika hata kama mume wake atajifungua mtoto hivi karibuni.

“Ataendelea kuwa baba na mimi nitakuwa mama,” alisema Nancy ambaye kwa mujibu wa maelezo yake ndoa yao inatambulika kisheria.

Nancy ana watoto wawili aliowapata katika ndoa yake ya awali kabla ya kuolewa na Beatie. Kwa mujibu wa magazeti ya “Telegraph” na “Herald Sun” watu wengi hasa wanamaadili wamepinga hatua ya Beatie na mke wake kupata mtoto kwa njia hiyo.

“Kama walitaka mtoto wangeweza kwenda vituo vya watoto yatima" amenukuliwa na gazeti la Telegraph. Baadhi ya watu wengine waliotoa maoni yao katika gazeti la Herald Sun wamepinga vikali suala la Beatie kubeba mimba.

No comments: