Tuesday, March 4, 2008

Yanga, Adema waingiza mil. 65.2/-

na Dina ZubeiryWAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likizipongeza timu za Simba na Yanga kwa kusonga mbele kwenye michuano ya kimataifa, mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na AS Adema, iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, imeingiza sh mil. 65. 2.

Mechi hiyo iliyokwisha kwa Yanga kusonga mbele kwa jumla ya ushindi wa mabao 2-1, katika mechi ya kwanza, Yanga ilifungwa 1-0 kabla ya kushinda 2-0 katika mechi hiyo ya marudiano.

Yanga sasa itakumbana na Al-Qada ya Libya huku Simba iliyoifungasha virago AWASSA City ya Ethiopia, ikikumbana na Enyimba ya Nigeria.

Mechi za kwanza za raundi ya pili ya michuano hiyo (Ligi Mabingwa na Shirikisho), kwa Yanga na Simba, zitafanyika ugenini kati ya Machi 21 na 23, kabla ya kurudiana kati ya Aprili 4 na 6.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage, kama Simba na Yanga zitajipanga vema katika mechi zao, hakuna kitakachozuia kusonga mbele.

Kuhusu mapato ya mechi ya Yanga na AS Adema, Kaijage alisema, fedha hizo zimepatikana kutokana na watu 12,112 walioingia katika mechi hiyo na kulipa.

Mechi hiyo iliyoisha kwa Yanga kushinda 2-0, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-1, viti maalumu ilikuwa ni sh 20,000, jukwaa kuu sh 15,000, sh 8,000 kwa jukwaa la kijani na sh 3,000 kwa mzunguko.

Kwa mapato hayo, Yanga imepata sh mil. 41.6 huku TFF na CAF zikilamba sh 9,591,410, Uwanja sh 6, 394, 410, huku gharama za mchezo zikiwa ni sh 2,186, 000.

Katika hatua nyingine, kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyoikumba Cameroon, TFF imelazimika kutuma barua kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kupata uhakika wa mahali itakapofanyika mechi ya Twiga Stars.

Kaijage alisema, TFF imechukua hatua hiyo baada ya CAF kusitisha mechi za klabu, hivyo TFF imetaka kufahamu mahali ambako mechi hiyo ya marudiano itachezwa.

Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Februari 23, Twiga Stars ilifungwa mabao 3-0, hivyo kuhitaji ushindi wa mabao 4-0 katika mechi ya marudiano.

Mshindi wa mechi hiyo, atakuwa amejitwalia nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wanawake, zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea baadaye mwaka huu.

Alisema, ukiondoa utata huo wa mahali itakapofanyika mechi hiyo, maandalizi mengine ya safari ya kwenda Cameroon, yanaendelea vema kwani Twiga Stars inatarajiwa kuondoka nchini Machi 6.

Aidha, TFF imekata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kazi kumpa ushindi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Ashery Gasabile.

Gasabile aliyeajiriwa na TFF Julai 16 mwaka 2006, alikuwa akipinga taratibu zilizotumiwa na TFF kusitisha ajira yake Desemba 17, mwaka huo na Mahakama ya Kazi chini ya Jaji Mfawidhi Ernest Mwipopo, kuridhia pasipo shaka kuwa Gasabile, aliachishwa kazi kimakosa.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage, Shirikisho hilo limekata rufaa kupitia kwa wakili wake, Alex Mgongolwa, kupinga hukumu hiyo.

No comments: