Friday, March 21, 2008

Ray, Johari kuozea jela


Hii ni baada ya wasanii hao kwa mara nyingine tena, kushindwa kuitikia wito wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni – Kinondoni, kufika hapo kusikiliza shauri la madai lililofunguliwa dhidi yao.

Wiki iliyopita mahakama hiyo ilitoa tangazo katika vyombo vya habari, likiwataka wasanii hao kufika mahakamani hapo juzi Jumatano kuanzia saa 2:30 asubuhi ili kusikiliza shauri hilo lililofunguliwa na McDonald Mwakamele.

Mahakama ilifikia hatua hiyo baada ya wasanii hao kukataa kusaini samansi wanazopelekewa, huku wakidaiwa kumtisha karani anayewapelekea.

Baadhi ya mahakimu katika mahakama zilizopo Kinondoni, walipohojiwa kuhusu mwenendo wa kesi hiyo, walisema kitendo cha wasanii hao kukimbia kinawaweka hatarini kwani wanaweza wakafungwa kwa miezi sita kwa kosa la kuidharau mahakama.

“Kitendo hiki cha kutofika mahakamani ni kuonyesha dhahiri wanaigomea mahakama, sisi hatutaki kujua kama wameonewa au vipi tunachotaka waje wasikilize kesi zao kisha wajitetee wawezavyo, sasa kutofika ina maana gani?
“Unajua labda ni utoto unawasumbua maana wanaona kama wanaigiza vile, lakini wajue mahakama haichezewi, huyu Johari ndio hajawahi kukanyaga hata siku moja,” alisema hakimu mmoja.

Ray na Johari wamefunguliwa shauri hilo, ambapo McDonald analalamika kuibiwa filamu yake ya Revenge na wasanii hao, iliyomgharimu zaidi ya Sh milioni 30 na anadai arudishiwe na kulipwa fidia.

Shauri hilo la madai lililopewa na. 370 f 2007, linasikilizwa na Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi, Kalombola na limeahirishwa hadi Mei 6, mwaka huu.

Kuozea kwao jela kwa wizi kunakuja iwapo hukumu itatolewa bila wao kuwapo mahakamani, adhabu inayoweza kuambatana na dharau zao kwa mahakama kutokana na kuitwa na kukaidi.

No comments: