Saturday, March 29, 2008

Hatari


Habari za ndani zinasema kwamba purukushani zilizofanywa na changudoa huyo (kama anavyoonekana pichani ukurasa wa kwanza wa gazeti hili), hasa baada ya kulazimisha kufanya mapenzi kwa nguvu na mwandishi wa gazeti hilo, zilimfikia mkewe ambaye bila kujua mumewe alikuwa kazini, alifungasha virago na kutimkia nyumbani kwao.

Ilielezwa kuwa fujo zilizofanywa na mwanamke huyo, ziliamsha baadhi ya majirani wa nyumba ya tukio, ambapo kati ya hao, wapo wanaomfahamu mwandishi huyo (Jina tunalo) na kuamua kufikisha umbea kwa mke wake.

“Kuna majirani ambao walimtambua mwandishi wa gazeti hilo, hasa ukizingatia kwamba kutoka nyumba iliyofanyika tukio siyo mbali na anapoishi, kwahiyo tunahisi kuna mtu alimpigia simu mke wake,” kilisema chanzo chetu.

Kiliendelea: “Tuliamini kuwa kuna mtu alimpigia simu mke wake kwasababu hakuchelewa kufika eneo la tukio, ingawa alikuta changudoa huyo ameshaondoka.”

Chanzo hicho kiliongeza, mara baada ya mwanamke huyo kufika eneo la tukio, alimvaa mumewe na kumtuhumu kuwa anatamaa, ndiyo maana alimuacha nyumbani na kwenda kuhangaika na machangudoa.

Sambamba na kumporomoshea tuhuma hizo, habari zinadai kuwa mwanamke huyo alidai apewe talaka kwa vile mume wake amemdhalilisha kwa kitendo hicho.

Hata hivyo, chanzo hicho kiliongeza kuwa timu ya waandishi wa Ijumaa Wikienda ambayo ilikuwa pamoja na ‘kachero’ aliyekumbwa na kizaazaa hicho, ilimuelewesha mwanamke huyo ukweli kwamba mume wake hakuwa na nia ya kimapenzi na changudoa huyo, isipokuwa alimchukua kwa minajili ya uchunguzi wa kikazi.

“Aliambiwa kwamba mume wake alikuwa kazini, lakini hakuelewa, badala yake akawa anasisitiza apewe talaka kwa madai kuwa mume wake hafai.

“Usiku huohuo, hakulala nyumbani kwake, badala yake alikwenda kwa rafiki yake. Asubuhi, alirudi nyumbani kuchukua nguo na mizigo mingine, kisha akatimkia kwa wazazi wake, Tandika, Dar es Salaam,” alisema mtoa habari huyo.

Risasi, liliongea na mwandishi anayedaiwa kukachwa na mkewe, ambaye alisema kuwa anafikiria mwanamke huyo anaweza kubadilisha uamuzi wake wa kuondoka, baada ya Gazeti la Ijumaa Wikienda, kutoa habari, inayoelezea ukweli wa tukio hilo, Jumatatu hii.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mwandishi wake mmoja, usiku wa Ijumaa Kuu, alimnunua changudoa huyo kwa shilingi 7000 kwa lengo la kukamilisha uchunguzi wa kukithiri kwa vitendo vya ukahaba ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Baada ya kumnunua, mchunguzi huyo hakutaka kufanya naye mapenzi, hivyo aliishia kumhoji maswali yanayohusiana na biashara ya ukahaba na changamoto zinazowakumba wao kama wahusika wakuu.

Hata hivyo, mwandishi huyo alimpatia changudoa huyo pesa waliyokubaliana bila kufanya mapenzi, kitendo ambacho kilipingwa na mwanamke huyo, aliyesema hataki kupewa hela ya bure mpaka aifanyie kazi.

Katika kusisitiza hilo, mwanamke huyo alivua nguo na kubaki mtupu, kisha akawa anamlazimisha mwandishi wa gazeti hilo, afanye naye mapenzi.

Pamoja na kulazimisha ngono, mwanamke huyo aliyekuwa amelewa, alifanya fujo zilizoamsha majirani wa nyumba hiyo, iliyopo Kijitonyama, jijini.

No comments: