Monday, March 31, 2008

Chameleon jambazi


Mdau huyo (jina tunalo), aliliambia gazeti hili wikiendi iliyopita kuwa Chameleon ni jambazi wa kazi za wasanii wenzake na kuongeza kwamba ameshajitengenezea pesa nyingi kwa wizi, hivyo Watanzania wanatakiwa kumuogopa.

Alisema, kitendo cha Watanzania kuendelea kumpenda mwanamuziki huyo raia wa Uganda na kununua kazi zake, wakati alimuibia ala (beats), Mtanzania mwenzao, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ ni sawa na kukosa uzalendo.

“Chameleon hana ubinadamu, alichomfanyia Profesa Jay hakikuwa kitu cha kiungwana hata kidogo, unajua ile ‘beat’ aliyomuibia ilimuingizia shilingi ngapi za Kiganda? Alimkumbuka mwenzake?” Alihoji mdau huyo.

Aliendelea kusema, pamoja na kuiba beat ambayo aliitengenezea wimbo na kujiingizia mamilioni ya shilingi, Chameleon alifanya kiburi kwa kukaa kimya bila kutoa kauli yoyote, wakati Profesa Jay alipokuwa akilalamika kuibiwa.

Aliongeza, licha ya kufanya kiburi, bado msanii huyo alianzisha ‘bifu’ na Jay katika ugomvi ambao chanzo ni yeye kumuibia mali yake.

“Ugomvi huo, uliisha pale Jay alipokwenda Uganda. Alimtafuta Chameleon na alipoonana naye, alimuambia hana bifu naye, halafu alitunga wimbo wa Ndivyo sivyo ambao waliimba pamoja.

“Baada ya kurekodi wimbo huo, Chameleon aliusajili kama wake, wakati mtunzi ni Jay na ndiye aliyeandika mashairi. Kwa sasa jumuiya za kimataifa zinatambua wimbo ni wa Chameleon,” alisema mdau huyo.

Alifafanua kuwa hivi karibuni msanii huyo alipewa tuzo kupitia wimbo huo wa Ndivyo sivyo, wakati mtu ambaye aliistahili ni Profesa Jay kwakuwa ndiye aliyefanya kazi kubwa.

Hata hivyo, mdau huyo aliwataka wasanii wa Kitanzania kuamka, kuzisajili nyimbo zao na kuzipatia haki miliki ili wapate utetezi pale watakapoibiwa na wenzao wenye nguvu kuliko wao.

Wimbo wa Profesa Jay ambao beat yake iliibiwa na Chameleon unaitwa Nikusaidieje ambao mkali huyo wa Bongo Flava aliufyatua mwaka 2005.

No comments: