Saturday, February 23, 2008

Wanajeshi wageuka mbogo Dar

Na Dunstan Bahai


Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jana lilivamia ofisi ndogo za Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASCO) zilizopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuanza kuwashambulia kwa mateke na marungu wafanyakazi watano wa shirika hilo mbele ya familia zao.

Mbali na kuwapiga vibaya wafanyakazi hao, waliwalazimisha kuwafungulia maji waliyokatiwa juzi kutokana na kutolipa deni la Sh. milioni 276.

Wanajeshi hao walitumia nguvu kuwabeba hadi kambi ya jeshi la Lugalo.

Tukio hilo lilitokea jana saa 4.00 asubuhi ambapo baada ya saa tatu, waliwatoa jeshini na kuwarejesha ofisini hapo ambako waliendelea kuwashambulia na kuwataka wawafungulie maji.

Wafanyakazi hao walisema, maji hayo hawakufunga wao na kuwashauri wawasiliane na DAWASCO Makao Makuu, lakini wanajeshi hao waliendelea kuwaonyesha ubabe.

Kutokana na tukio hilo, maofisa wa DAWASCO wakiongozwa na Ofisa Mkuu wa Biashara, Bw. Raymond Mndola na Meneja Uhusiano, Bi. Badra Masoud, walifika eneo la tukio, nyuma ya Chuo Kikuu cha Ardhi.

Wakiwa katika eneo la tukio, Bw. Mndolwa aliwashauri kufanya mazungumzo ya amani ili kujua kulikoni, lakini wanajeshi hao walionyesha ubabe huku wakizungumza kwa jazba na vitisho.

Ofisa huyo ghafla alishangaa kuvamiwa na kuanza kukwidwa na kulazimishwa kuingia ndani ya gari la wanajeshi hao lenye namba 2543JW97 kutoka kikosi namba 302.

``Niliwagomea na walishindwa kunichukua Hawawezi kuwazuia wafanyakazi wetu kufanya kazi zao, huu ni unyanyasaji... Vitendo walivyowafanyia walitakiwa kuwafanyia Ofisa Mkuu Mtendaji Bw. Alex Kaaya au mimi mwenyewe au Bodi ya shirika maana hao ndiyo waliowatuma kazi.

``Hatuwezi kuvumilia Wameondoka baada ya kutusikia tunawasiliana na mabosi wao makao makuu. Hawa walikuwa ni wahuni tu hawakuja rasmi, kwa nini wameondoka sasa, hata hawakutumia taratibu za kisheria. We unadaiwa halafu unalazimisha mdeni wako aendelee kukupatia huduma,`` alisema Bw. Mndolwa akiwa amevaa uso wa mshangao.

Wanajeshi hao waliwaweka kizuizini kwa takribani saa mbili maofisa, wafanyakazi wa DAWASCO na waandishi wa habari huku wakiwa wameegesha gari lao ndani ya geti la ofisi hizo ambapo walikuwa wakirandaranda kama wameweka lindo sehemu yenye tukio kubwa la uhalifu.

Kutokana na mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa na maofisa hao wa DAWASCO na makao makuu ya JWTZ, askari hao wapatao saba, wengi wao wakiwa hawana vyeo, walikurupuka eneo hilo majira ya alasiri kwa kutumia gari lao aina ya Land Rover 110 lililokuwa likiendeshwa na askari mwanamke na kuwaacha waandishi na maofisa hao kuangua vicheko, huku wakiahidi kurudi tena.

Hali hiyo iliwaudhi ambapo walipofika nje ya geti walirudi na kumkamata mpiga picha wa gazeti la Mwananchi, Bw. Fidelix Felex na kumpora kamera yake na kutokomea nayo.

Wafanyakazi waliopigwa na askari hao ni Samuel Masawe, Josephine Kombo, Marick Rajabu, Charles Memba na Zuhura Salum.

Wafanyakazi hao na mwandishi huyo, wakiongozwa na Bw. Mndolwa, walikwenda kituo cha polisi cha Chuo Kikuu na kufungua kesi.

DAWASCO juzi walilazimika kukata maji kwenye vikosi, nyumba za maofisa wa jeshi hilo, hospitali ya Lugalo na maeneo mengine yanayomilikiwa na jeshi hilo kutokana na deni la Sh. milioni 276.

Mafundi watano wakiwa wanakata maji juzi kwenye majengo yanayokaliwa na maofisa wa jeshi hilo eneo la Alykhan, ghafla walifika askari na kuwachukuwa na kuwapeleka makao makuu ya jeshi Upanga ambako waliandikisha maelezo kisha kuwaachia.

Aidha, waandishi na wapiga picha wakiwa katika nyumba hizo, walivamiwa na watoto na wafanyakazi wa ndani wa kiume na kuwatishia kuwapiga kwa marungu na masululu ili wasitimize wajibu wao, lakini baadaye walishindwa na wapiga picha waliendelea na kazi yao.

Katika ziara yake Jumatano wiki hii ya kutembelea vyanzo vya maji na mitambo ya kusukuma maji jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Mark Mwandosya, aliwakingia kifua Mawaziri wasiandikwe kwenye magazeti hata kama ni wadeni sugu.

``Mawaziri ni sura ya nchi, sasa unapowaandika kuwa hawalipi bili zao ni kuidhalilisha nchi?kama wapo naomba mnipatie majina yao nitawafuatilia hadi walipe,`` alisema.

Aidha alilitaka shirika hilo kuharakisha kutoa huduma hiyo kwa wananchi pale wanapoihitaji.

Wakati huo huo, jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesikitishwa na kitendo cha Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASCO) kuwakatia maji, na hasa ikizingatiwa kuwa jeshi ni taasisi ya serikali ambayo inategemea fedha kutoka serikalini na kwamba pia ni wadau wakubwa wa shirika hilo.

Masikitiko hayo yamo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jioni na jeshi hilo na kueleza madhara makubwa yanayoweza kutokea baada ya kukata maji hayo hasa sehemu muhimu kama kambi ya Lugalo ambayo ina hospitali kubwa ya kijeshi.

Taarifa hiyo ilitaja madhara hayo kuwa ni pamoja na kusimamisha shughuli zote za kiulinzi zinazoendeshwa kutoka Lugalo na kuwepo uwezekano wa milipuko ya magonjwa katika eneo hilo ambalo linakaliwa na wanajeshi na familia zao takribani 5,000.

``Kitendo cha kulikatia jeshi maji kinaleta picha potofu mbele ya Watanzania kwamba jeshi haliwajibiki katika kulipia huduma wanazopewa wakati jeshi linalipia huduma zote hizo kulingana na bajeti. Pamoja na hali hii jeshi limekuwa mstari wa mbele kuisaidia DAWASA na DAWASCO pale panapotokea madhara katika mfumo wa maji,`` ilieleza taarifa hiyo kutoka makao makuu ya JWTZ.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jeshi kwa mwaka huu wa fedha lilitengewa Sh. 2,019,178,555.35 katika bajeti yake ya maji na kwamba hadi mwezi Januari mwaka huu, lilipatiwa Sh. 1,285,917,708 kutoka wizara ya Fedha ambazo zililipia gharama za maji katika vikosi vyote nchi nzima.

``Hundi ya mwisho ni ya Sh. milioni 78 waliyolipwa DAWASCO mwezi Januari, mwaka huu,`` ilieleza taarifa hiyo na kutoa mchanganuo wa malipo hayo kuanzia Julai, mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kulipia gharama za maji ni kidogo, bili nyingi za DAWASCO sio sahihi na hivyo kuhitaji kuhakikiwa na kwamba tabia ya shirika hilo kupandisha gharama za maji katikati ya mwaka wa fedha kumechangia jeshi kuchelewesha kulipa kwani halikuwa na fedha za ziada.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao cha mwisho kujadili mustakabali huo kilikaa baina ya Mnadhimu Mkuu wa Jeshi na Meneja Mkuu wa DAWASCO, Februari 21, mwaka huu na kukubaliana kuwa shirika hilo kurejesha maji siku inayofuata, lakini hawakufanya hivyo.
SOURCE: Nipashe

No comments: