Saturday, February 23, 2008

CCM nayo yaingia Kiteto na helikopta

Na Simon Mhina


Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kutua wilayani hapa akiwa na helikopta kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimejibu mapigo kwa kuleta helikopta yake.

Helikopta ya CCM kwa mara ya kwanza ilitua jana katika uwanja wa mpira wa Kiteto ikitokea jijini Dar es Salaam na habari zilisema ndege hiyo imekuja kutokana na jituihada za Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM).

Helikopta hiyo yenye namba za usajili 5Y-BTW imekodiwa kutoka kampuni ya Tropic Air ya nchini Kenya.

Ndege hiyo ilitua uwanjani hapa majira ya saa tano asubuhi huku ikiwa na makada mbalimbali wa Chama hicho, akiwamo mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.

Bw. Sendeka alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelazimika kubadili staili ya kampeni zake katika uchaguzi huo mdogo, ili kuweza kuwafikia wananchi wa jimbo hilo kwa haraka, mbali ya kutegemea usafiri wa magari.

``Sababu nyingine iliyotufanya tulete ndege hii, ni kujaribu kupita sehemu zote walizopita CHADEMA kupotosha umma kwamba uchaguzi utakuwa tarehe 25 badala ya tarehe 24 mwezi huu kama ilivyopangwa na Tume ya Uchaguzi,`` alisema.
Kuhusu vibali vya ndege hiyo, Sendeka alisema.

``vibali vya ndege hii na taratibu zote zimekamilika. Hakuna shaka kuhusu kuhusu ulali wa ndege hii kuwapo hapa,``alisema.

Katika hatua nyingine, wakati Chama Cha Mapinduzi kikifurahia ujio wa ndege hiyo, helikopta ya CHADEMA jana ilishindwa kuruka katika uwanja wa ndege wa Dodoma, kutokana na hitilafu ya kiufundi.

Baada ya kutua Kijungu, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akiwa na mgombea wake, Victor Kimesera, aliendelea na mikutano mingine katika Kata za Langatei, Sunya na Dongo kabla ndege hiyo haijaenda kulala Dodoma.

Akiongea kuhusu helikopta ya CCM, Bw. Mbowe alisema: ``Nimesiki CCM nao wameleta helikopta, hiyo haina tatizo kwa sababu dhamira ya kampeni si helikopta. Kampeni ni hoja. Naomba CCM wajue kwamba hatushindi Kiteto kwa sababu ya helikopta bali hoja.``

Kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo la Kiteto zimevuta hisia za Watanzania wengi waliolekeza macho yao katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika kesho.

Kubwa ni kwa wananchi wa Kiteto wanaoshuhudia vituko na vibweka mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vyenye ushindani mkubwa katika kuwania jimbo hilo lililoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wake, Benedict Losurutia (CCM).

No comments: