Monday, February 18, 2008

LANGA KILEO MCHIZI WA WAKILISHA ANAYEZIMIA A.K.A ZA KIBANTU


Mwanamuziki, Langa Kileo, akiwa ni zao la Coca Cola Pop Stars ni miongni mwa wasani waliokuwa wakiunda Kundi la Wakilisha akiwa na wanadada wawili, Sarah Kaisi na Whitnes Mwaijanga.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa Langa kuingia katika gemu kwani akiwa katika kundi hilo, liliparaganyika kutokana na kila mmoja kutamani kutoka kivyake.

Aliyeanza kung’atuka alikuwa ni Sarah Kaisi ambaye aliweza kurusha hewani mipini kadhaa kabla ya kutawaliwa na kimya kingi, ambapo alifuatiwa na Langa anayetamba katika gemu kwa sasa.

Hata hivyo, baada ya wakali hao wawili kutoka kivyao, Whitnes Mwaijanga hakukaa kimya kwani aliweza kurusha hewani mpini wake mkali uliokwenda kwa jina la Kicheko ambao unatamba kwenye vituo mbalimbali vya redio.

Lakini katika safu hii leo tunamcheki nani kati ya wanamuziki hao watatu? Huyo si mwingine ila ni Langa mwanaume pekee aliyekuwa katika Kundi hilo la Wakilisha.

Je, ni kazi gani iliyomfanya mchizi huyo aonekane yuko juu hadi kumudu kusimama peke yake jukwaani? Langa hayupo mbani nasi hivyo ni fursa kwake kuweza kufafanua: “Kazi yangu ya kwanza ilikwenda kwa jina la Matawi ya juu iliyotoka 2005.

“Jina hilo la matawi ya juu lilidhihirisha hivyo pale video ya kibao hicho ilipotajwa kuwania Tuzo za MTV Base kwa upande wa hapa Bongo miaka michache iliyopita, kisha kutwaa Tuzo ya Kisima nchini Kenya.
“Moto huo uliwafanya baadhi ya wasanii wakongwe katika gemu ya Bongo Fleva kunitafuta na kunipa majukumu ya kushiriki katika kazi zao, ikiwemo Chagua moja ya Fid Q.

“Baada ya kuona wakongwe wamekubali vitu vyangu na kuanza kunishirikisha niliongeza spidi nikawa natembea kilometa 180 kwa saa, jambo ambalo liliniwezesha kubisha hodi Nairobi kwa Rais Mwai Kibaki kungali mapema.
“Nikiwa Nairobi niliweza kufanya kazi na vichwa vikali vinavyounda Kundi la Necessary Noise, Naaziz na Wayre ambapo nilifanikiwa kutoa mpini mkali unaojiuza kwa jina la Nakotoka.

Inawezekana wapo ambao hawampati vilivyo mshikaji, kama ndivyo ni kwamba, mchizi alizaliwa Dar es Salaam, Desemba 1985 na kupiga madarasa katika jiji la Kandoro kabla ya kutimkia Uganda kwa ajili ya masomo zaidi.

Akiwa huko Uganda alijikita katika Chuo cha Vienna kilichopo katika jiji la Kampala, kisha baadaye kumalizia katika Shule ya Hillside International Academy, Kama utauliza kwa sasa yupo wapi na anafanya nini, jibu lake ni rahisi kwani mchizi anapiga shule katika Chuo cha Biashara (CBE), Kanda ya Dodoma huku matarajio yake katika gemu ya muziki yakiwa kujiuza kimataifa zaidi.

Naelewa wazi kwamba wadau mtataka kujua mshikaji muziki alianza lini hasa, ukweli ni kwamba ilikuwa ni kabla ya Coca Cola Pop Stars kwani anasema:

“Niliupenda muziki tangu nikiwa shuleni, ambapo nilikuwa naimba nyimbo (kopi) za baadhi ya wasanii wa nje.
“Wanamuziki ambao nilikuwa napenda kugandamiza mipini yao ni kama Tupac, Bob Marley na wengine wengi wa miondoko hiyo.

Huyo ndiye Langa Kileo msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye anapenda kujiwakilisha kwa jina lake la Kibantu tofauti na baadhi ya wasanii wengine wa Kibongo ambao wanatumia a.k.a za viwanja.
Makala haya yameandaliwa na Fatma Amri.

No comments: