Monday, February 18, 2008

BUSH: KIKWETE MWAMINIFU
• ASEMA YEYE HASHUGHULIKI NA VIONGOZI MAFISADI
• ASAINI MKATABA WA MSAADA WA MABILIONI.

Rais George Bush wa Marekani, amemsifu Rais Jakaya Kikwete kuwa ni kiongozi makini, hodari na mwaminifu.

Rais Bush ambaye yupo nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku nne, alitoa pongezi hizo jana asubuhi, baada ya kusaini makubaliano ambapo Marekani itaipatia Tanzania dola milioni 700 (karibu sh Bilioni 800 za Tanzania), kupitia mpango wa Milleniumii, Challenge compact (MCC).

Makubaliano hayo yalisainiwa saa 5:30 asubuhi katika viwanja vya Ikulu jiijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na viongozi wa ngazi za juu wa Tanzania na Marekani pamoja na waandishi wa habari.

Marekani haishirikiani na watu wanaoiba fedha za wananchi, ndiyo sababu tumesaini mkataba mkubwa wa fedha kuwahi kutolewa kwa nchi ya Kiafrika katika historia ya watu wa Marekani.

“Tunakupongeza kwa kupambana na rushwa, na serikali yako kuheshimu utawala bora. Marekani itaendelea kukuza urafiki na ushirikiano uliopo,” alisema Rais Bush.

Katika hotuba yake iliyokuwa na mvuto wa kipekee, Rais Bush alisifu mapokezi makubwa na ya kipekee aliyoyapata kutoka kwa Watanzania alipowasili Jumamosi jioni.

Kutokana na kuridhishwa na utendji kazi wa Serikali ya Kikwete katika kupambana na rushwa, umasikini na maradhi, Rais Bush aliahidi kuipatia misaada zaidi Tanzania.

Akizungumzia suala la mgogoro wa kisiasa wa Zimbabwe, Rais Bush alisema wananchi wa nchi hiyo wana haki ya kupata serikali ambayo italinda na kupigania maslai yao.

“Wananchi wa Zimbabwe wanahitaji serikali yenye kuheshimu demokrasia na yenye kujali maslai yao,” alisema.

Kuhusu machafuko yanayoendelea jimboni Darful nchini Sudan, Rais Bush alisema kinachoendelea ni mauaji ya kimbari (genocide), na kuhaidi kuendelea kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kwa kushirikiana na nchi, pamoja na taasisi nyingine za kimataifa.

Pia alitangaza rasmi uamuzi wake kwa kumtuma Condoleezza Rice, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwenda Kanya leo, kusaidia juhudi za kusaka amani.

Kwa upande wake, Rais Kikwete alimshukuru Rais Bush kwa kulipa Bara la Afrika kipaumbele katika kukabiliana na umasikini maradhi, na suala zima la amani.

Aliishukuru Marekani kwa msaada wa dola milioni 700, na kuahidi kuzitumia kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo kwenye mkataba.

“Kilio cha muda mrefu kuhusu ubovu wa miundombinu hasa ya barabara na umeme sasa kimepata ufumbuzi,” alisema Rais Kikwete baada yakusaini makubaliano ya MCC.

Alisema kutokana na misaada mingi ya kifedha iliyotumika katika mapambano dhidi ya malaria na Ukimwi, Rais Bush atakumbukwa kwa miaka mingi kutoka kizazi hadi kizazi.

Mapema Bush na ujumbe wake, akiwamo Waziri wa Mambo ya nje, Condoleezza Rice, aliwasili Ikulu asubuhi na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete kwa zaidi ya saa mbili.

Alipata nafasi ya kushikana mikono na baadhi ya watu waliokuwa wamejipanga katika lango kuu la kuingilia Ikulu mapema jana asubuhi.

Baadaye mchana alitembelea Hospitali ya Amana, iliyopo Ilala, kushuhudia namna fedha zilizotolewa na utawala wake kusaidia wagonjwa wa Ukimwi zinavyowasaidia waathirika.

Ulinzi mkali uliimarishwa katika eneo lote la Ikulu, huku walinzi wa Bush wakichukua nafasi ya wenzao wa Tanzania ambao walibaki kuwa watazamaji,

Kila kitu kiliandaliwa na walinzi hao kutoka Marekani, kuanzia jukwaa hadi mahali pa kuketi wageni mashuhuri walioongozana na Bush pamoja na viongozi wakuu wa Tanzania, wakiwamo Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na waziri kiongozi, Shamsu Vuai Nahodha,

Baadhi ya walinzi hao walikua juu ya jingo la Ikulu, wakizunguka kutoka upande moja hadi mwingine kuhakikisha kiongozi huyo, anayewindwa kwa udi na uvumba na magaidi duniani, yupo salama.

Hata wapiga picha ambao kutoka ndani na nje ya nchi, ambao katika matukio kama hayo huranda randa kutoka sehemu moja hadi nyingine kutafuta eneo zuri la kupiga picha, waliwekwa sehemu maalum ambako hawakutakiwa kusogelea maeneo mengine.

Bush yupo katika ziara ya nchi kadaa barani Afrika na kabla ya nchi ndogo iliyopo afrika Magharibi.

Kutoka hapa atakwenda Rwanda na kasha Ghana na kumaliza ziara yake Liberia Februari 21 kabla ya kurejea nyumbani.

Hii ni ziara ya pili ya Rais huyo wa taifa kubwa na lenye nguvu dunani barani Afrika katika mataifa ambayo anasema yameonyesha mfano mzuri katika demokrasia na utawala bora. Mara ya kwanza, alitembelea Afrika mwaka 2003, miaka miwili baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Marekani Januari 2001.

(IMETOLEWA NA GAZETI LA MTANZANIA 18/2/2008)

No comments: