Wednesday, February 20, 2008

CHADEMA wavutana na polisi



YAMEIBUKA malumbano ya hoja kati ya Jeshi la Polisi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu wahusika waliowavamia, kuwashambulia na kuwajeruhi viongozi na makada wa chama hicho, walio katika kampeni zenye mvutano mkubwa za ubunge katika Jimbo la Kiteto, mkoani Manyara.
Wakati jeshi hilo likisema kwamba watu waliofanya vurugu hizo ni morani wa Kimasai, CHADEMA wao wanasema wahuni hao ni watu wanaojulikana, na ambao kimsingi wanatakiwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Manyara, Luther Mbutu alisema jana kuwa, uchunguzi walioufanya umebaini kwamba, waliofanya uvamizi huo si polisi wala makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), bali ni morani waliokerwa na makada hao wa CHADEMA waliokuwa wakitangaza kuwa uchaguzi jimboni humo utafanyika Februari 25 (Jumatatu ijayo) badala ya Jumapili ya Februari 24 kama ilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wakati RPC Mbuttu akitoa maneno hayo, Mkurugenzi wa Vijana na Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika alisema jana kuwa, wahusika wa shambulizi hilo wanafahamika, hivyo kuna haja ya kuwakamata ili waisaidie polisi kueleza aliyewatuma kufanya unyama huo.

Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, CHADEMA imesikitishwa na vitendo vinavyofanywa na wafuasi wa CCM wanaoshirikiana na baadhi ya polisi kuendesha uharamia katika mchakato wa kidemokrasia kama huo wa uchaguzi.

“Tunaamini kuwa, tukio hili ni pigo kwa harakati za demokrasia nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho serikali imekuwa ikidai kuimarisha demokrasia na mahusiano na vyama vya upinzani. Ni kwa sababu hiyo tunawaomba wapenda demokrasia na maendeleo nchini, ikiwa ni pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, viongozi wa dini, vyombo vya habari na wadau wengine, kulaani uharamia huu,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari juzi mchana, Kamanda Mbutu alidai kuwa katika maelezo yao, polisi wahanga wa tukio hilo wamedai kuwa wamepigwa na watu wasiojulikana na ambao hawawafahamu, jambo ambalo limekanushwa na viongozi hao waliojeruhiwa.

Mbuttu alidai pia kuwa, kupigwa kwa viongozi hao wa CHADEMA kunatokana uamuzi wao wa kumpiga askari polisi mwenye namba E 7177 Godwin, ambaye alikuwa na silaha na mgambo mwenye namba MG 245487.

“Walimpiga mtama polisi huyo na bunduki ikadondoka, pia wakamvamia mgambo mwingine, ndipo wananchi wakishirikiana na Wamasai wakapandwa na hasira na kuanza kuwapiga viongozi hao,” alisema Mbutu na kuongeza kuwa, bunduki hiyo iliokotwa na raia wema na kuisalimisha katika kituo kidogo cha polisi.

Alisema hata hivyo, kutokana na tukio hilo na madai ya viongozi wengine wa CHADEMA wakiwemo wabunge waliopo jimboni humo kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi huo mdogo, ameamua kumuondoa kituoni hapo mkuu huyo wa kituo aliyemtaja kwa jina la Koplo Mgaya, mwenye namba E1972.

Kamanda huyo alisema kuwa, hadi hivi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusu tukio hilo, ingawa awali wakati akizungumza na Tanzania Daima mbele ya viongozi wa CHADEMA, akiwemo mbunge wa Karatu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa viti maalum, Grace Kihwelu na Lucy Owenya, alidai kuwa kuna watu wawili ambao wanaisaidia polisi.

Alidai mbele ya wabunge hao kuwa, watu hao wawili ambao baadaye walikuja kutambulika kwa majina ya Hamisi Kilindo na Keneth Mbilinyi, wanatuhumiwa kuhusika katika tukio hilo, lakini alitoa maelezo ya utata zaidi alipodai kuwa dereva wa chama hicho, Baraka Daudi, alijigonga mwenyewe katika gari.

Hati za matibabu za viongozi hao waliojeruhiwa ambazo zimesainiwa na Dk. Bartazar Mosha wa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto (Tanzania Daima ina nakala zake), zinaeleza kuwa licha ya majeraha yaliyotokana na vipigo, macho ya viongozi hao yameathiriwa na kemikali waliyomwagiwa usoni, ambayo bado haijatambuliwa.

Dk. Slaa alieleza kushangazwa kwake na kauli za Mbutu ambazo zinatofautiana na alizozitoa awali.

“Kuna tatizo na tunawasilisha barua kwa IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini) ya kueleza kutokuwa na imani na mkuu huyo wa kituo na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Luther Mbutu,” alisema.

Kufuatia hali hiyo, viongozi wa CHADEMA ambao wapo mjini Kiteto, jana asubuhi waliamua kuwaondoa hospitalini wahanga wa tukio hilo na kuwahamishiia hosteli za KKKT.

Tofauti na maelezo ya awali ya kamanda huyo kuwa walizungumza na wahanga wa tukio hilo, jana asubuhi Tanzania Daima ilishuhudia askari wa upelelezi ndio wakichukua maelezo ya wahanga hao katika hosteli hiyo.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, alieleza kusikitishwa kwake na tukio hilo, na kueleza kuwa limekisikitisha na kukifadhaisha chama hicho.

“CUF inasikitishwa zaidi kwamba, kwa mujibu wa taarifa hizo, maafisa kadha wa Jeshi la Polisi wa Kituo kidogo cha Polisi cha Kijungu walishiriki katika hujuma hizo dhidi ya majeruhi hao,” alisema Hamad katika taarifa iliyosambaza jana.

Alisema kuwa CUF inalaani vikali matumizi ya nguvu, vitisho na kujiingiza kwa maofisa wa polisi katika vurugu ambazo zikiachiwa bila ya hatua madhubuti kuchukuliwa kwa wahusika, zinaweza kuipeleka nchi kubaya.

Maalim Seif alilitaka Jeshi la Polisi kujitoa katika ushabiki wa kisiasa na kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo baya na kutosita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika katika kujeruhi wananchi wasio na hatia bila ya kujali itikadi za kisiasa za wahujumu hao.

“Ili haki itendeke na ionekane ikitendeka, CUF inamuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi kusimamia mchakato wa kuwapata wahalifu na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria bila ya kuchelewa,” alisisitiza.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CUF amevitaka vyama vya siasa vyote vinavyoshiriki katika kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Kiteto na kwengineko nchini, kujiepusha na vitendo vya hujuma dhidi ya wapinzani wao, vurugu, ubabe na chokochoko zozote zinazoweza kuchafua amani nchini mwetu. Inavitaka vyama vya siasa kufanya kampeni kwa ustaarabu na kwa kuzingatia sheria za nchi, na kujiepusha kujichukulia sheria mikononi mwao.

No comments: