Wednesday, February 20, 2008

Bush aondoka, mipango yapangwa


na Lucy Ngowi


RAIS wa Marekani, George Bush, jana alihitimisha ziara yake ya kiserikali ya siku nne nchini, na kuagwa na maelfu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam huku serikali ikitoa mipango ya matumizi ya mabilioni yaliyosainiwa na rais huyo.
Msafara wa rais huyo wa Marekani, ulifika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere majira ya saa 1:48 asubuhi akiambatana na mkewe, Laura na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice.

Baada ya kufika uwanjani hapo, alipokewa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa na mkewe Salma, ambao walifika uwanjani hapo saa 1:10. Baada ya kupokewa na mwenyeji wake, walianza kuangalia vikundi mbalimbali vya ngoma vilivyokuwa vikitoa burudani.

Baadaye, Bush na Kikwete waliongozana hadi eneo maalumu lililotengwa na kupigiwa nyimbo za taifa za Tanzania na Marekani.

Baada ya kupigiwa nyimbo hizo, Bush akiongozana na mwenyeji wake alisimama kuagana na viongozi na wananchi mbalimbali kabla ya kuingia kwenye ndege yake Air Force One yenye namba ya mruko 28000.

Kabla ya kujitoma ndani ya ndege, Bush na mkewe walisimama juu ya ngazi na kuwapungia mikono maelfu ya watu waliokuja kuwaaga.

Ndege iliyombeba Bush ilianza kuzunguka uwanjani hapo saa 2:11 na kuruka saa 2:15 kuelekea nchini Rwanda ambako ana ziara ya siku moja.

Kabla ya ndege hiyo ya Rais wa Marekani haijaruka, ilitangulia ndege nyingine yenye uwezo sawa nayo, pia zinafanana, Air Force Two, yenye namba ya mruko 29000.

Awali ndege iliyowabeba waandishi wa habari kutoka nchi za nje na maofisa mbalimbali wa Marekani yenye namba ya mruko N 277 WA ilianza kuruka kabla hata Rais Bush hajawasili uwanjani hapo.

Wakati huo huo, Ikulu jana ilitoa taarifa inayoonyesha jinsi fedha zilizotolewa na Marekani kupitia MCC zitakavyotumika katika miradi kadhaa ya maendeleo nchini.

Msaada huo mkubwa kuwahi kutolewa na Marekani ulisainiwa na Rais Bush na Kikwete Jumapili ya Februari 17.

“Lengo kuu la MCC ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuinua kipato cha wananchi, na kuwaletea maisha bora kupitia uimarishaji wa njia za usafiri na usafirishaji, pia kupitia katika uboreshaji wa miundombinu ya nishati na maji,” ilisema sehemu ya taairfa ya Ikulu.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa thamani ya MCC ni dola za Marekani milioni 698 na sehemu kubwa ya kiasi hicho itaingizwa katika miradi ya usafirishaji kwa maana ya ujenzi wa barabara, ikifuatiwa na sekta ya nishati, na hatimaye sekta ya maji.

Taarifa hiyo ilitaja miradi itakayotekelezwa chini ya MCC kuwa ni barabara za Tanga-Horohoro (kilomita 68), Tunduma-Sumbawanga (kilomita 224), Songea-Namtumbo (kilomita 61), Peramiho-Mbinga (kilomita 78) na kilomita 35 za barabara mbali mbali za Pemba. Pia fedha hizo zitatumika kuufanyia matengenezo Uwanja wa Ndege wa Mafia.

Kwa upande wa nishati, miradi itakayotekelezwa ni kutandaza nyaya za umeme baharini kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar, ujenzi wa chanzo cha umeme wa maji kwenye Mto Malagarasi kwa ajili ya miji ya Kigoma, Uvinza na Kasulu, ukarabati wa vituo vya umeme na usambazaji umeme katika miji ya Mbeya, Iringa, Dodoma, Morogoro, Tanga na Mwanza.

Kwa upande wa maji, miradi itakayonufaika ni pamoja na upanuzi wa mitambo ya kusukuma maji Ruvu Chini kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam, udhibiti wa upotevu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na pia kuongeza upatikanaji wa maji katika mji wa Morogoro.

Taarifa hiyo ilisema kuwa chombo maalumu tayari kimeundwa na rais kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa MCC na kukitaja chombo hicho kinachojitegemea kuwa ni MCA-T.

“Chombo hiki kiliundwa rasmi na rais kupitia GN Na. 202 ya Septemba 21, mwaka jana, 2007. Chombo hiki tayari kimeanza kazi. Ajira katika ngazi ya wakurugenzi na baadhi ya maofisa waandamizi imekwisha kukamilika na zoezi linaendelea. Mtendaji Mkuu wa MCA-T ni B.S. Mchomvu,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa ilieleza kuwa baada ya kutiwa saini kwa MCC, sasa unafuata utekelezaji na kuwa kazi inayofanyika sasa, kama itakavyokuwa kwa sehemu kubwa ya mwaka huu wa 2008, ni maandalizi ya utekelezaji.

“Itaandaliwa michoro (designs) ya miradi, zitaandaliwa taarifa za mazingira, zitaadaliwa nyaraka za kuwania kazi zitakazofanyika chini ya mkataba huo, zitatengenezwa tenda na zitachambuliwa, kabla ya hatimaye kuteua makandarasi,” iliongeza taarifa hiyo.

No comments: