Tuesday, February 26, 2008

CCM YASHINDA KITETO

• Matokeo ya kata 13 kati ya 15 yathibitisha hivyo
• Hadi usiku alikuwa akiongoza kwa kura 4000
• Viongozi Chadema wakiri kupoteza uchaguzi
• Kambi ya upinzani yapigwa butwaa, yatafakari
• Sasa matokeo rasmi kutangazwa leo saa 5:00

MATOKEO ya awali ya Uchanguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Kiteto mkoani Manyara yanaonyesha kuwa mgombea ubunge wa Chama cha mapinduzi (CCM) Benedict ole Nangoro ameshinda
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima ilizipata jana usiku baada ya kura kuhesabiwa katika kata zote 15 (ukiacha maeneo machache ambayo yalikuwa hayajakamilika) yalikuwa yakionyesha kuwa, Nangoro alikuwa amevuna kura takribani 15,000 dhidi ya 11,000 alizokuwa amepata mshindani wake mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Victor Kimesera.

Habari ambazo Tanzania Daima ilikuwa imezipata majira ya saa 5.00 usiku wa kuamkia leo zilikuwa zikionyesha kuwa Nangoro alikuwa ameshinda katika takriban kata 11 kati ya kata zote 15 zilizokwishahesabiwa huku mpinzani wake alishinda katika kata nne tu.

Kwa mujibu wa habari hizo, hadi kufikia nyakati hizo, mgombea wa CCM alikuwa akiongoza kwa kuvuna wastani wa asilimia 59 ya kura zote zilizokuwa zimehesabiwa na hivyo kusababisha kimesera, mwanasiasa aliyekuwa akipewa nafasi kubwa kushinda akiwa amejinyakulia asilima 41 ya kura zote zilizokuwa zimehesabiwa hadi wakati huo.

Taarifa ambazo Tanzania Daima ilikuwa imezikusanya kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo zinaonyesha kuwa, wakati CCM walikuwa wamejikusanyia kura nyingi kutoka maeneo mengi ya mashambani na waliko wafugaji wengi, mgombea wa Chadema alikuwa amevuna kura nyingi katika maeneo ya mijini.

Mwenendo huo wa mambo ambao awali ulionekana kuwapa faraja na matumani makubwa ya kushinda kwa wana Chadema, ulibadilika ghafla wakati matokeo kutoka mashambani yalipoanza kufika makao makuu ya wilaya ya Kiteto yaliyonyesha kuwa Nangoro ambaye awali alonyesha kupwaya akivuna kura nyingi kiasi cha kumwaga mpinzani wake Kimesera.

Matokea hayo ya baadaye usiku yalisababisha kunyong’onyea na kupoteza matumaini kwa viongozi wa Chadema na makada wao, waliokuwa wakiongozwa na mwenyekiti wao. Freeman Mbowe aliyekuwa ameandamana na takribani wabunge na viongozi wote wajuu wa chama hicho.

Kiongozi mmoja wa juu wa Chadema aliyezungumza na Tanzania Daima majira ya saa 4.45 usiku aliyaelezea matokea ambayo walikuwa wameanza kuyapokea wakati huo kuwa ni ya kushtua na ambayo yalianza kutoa mwelekeo mbaya kwa chama chao na mgombea wao.

Hali hiyo ya mambo iliwafanya viongozi wa chama hicho cha upinzani wanze kujipanga kukabiliana na kile kinachoweza kuwakuta leo hii wakati matokeo hayo yakitangazwa na Msimamizi wa Uchunguzi wa Jimbo hilo.

Hata hivyo habari zaidi kutoka ndani ya chumba cha kuratibu mwenendo wa uchunguzi cha Chadema ambacho kulikuwa kikisimamiwa na mkurugenzi wa Taifa wa Uchunguzi. Msafiri Mtemelwa na Naibu Katibu wa chama hicho, Zitto Kabwe zilikuwa zikieleza kuwa, baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho walikuwa wakiendelea kusubiri hadi hatua ya mwisho wa uhesabuji wa kura ili kupata uhakika wa kitu gani hasa kimetokea na nani ameibuka mshindi.

Wakizingumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jana usiku, mwenyekiti wa Taifa wa chadema Freeman Mbowe na Kabwe walikiri kupoteza ushindi katika jimbo hilo ambalo awali lilionyesha matumaini makubwa.

‘Hali si nzuri CCM wanaongoza kwa takriban kura 4,000 hivi sasa (saa 4.30) usiku. Kuna kila dalili kwamba tumeshindwa,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake Kabwe alisema kushindwa kwao kunaonyesha mgawanyiko mkubwa wa kura kati ya wakulima na wafugaji, kwani katika maeneo yenye wakulma wengi Chadema walipata kura nyingi kuliko maeneo ya wafugaji.

Habari ambazo Tanzania Daima ilikuwa imezipata kutoka katika kata saba kati ya 15 ambazo matokeo yake yalikuwa yameshapatikana .

Baada ya kupata matokeo hayo ya awali, baadhi ya wafuasi wa Chadema walianza kupita mitaani wakishangilia, jambo ambalo lilisababisha askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kupiga vingora na kuwatawanya.

Awali mwenendo wa uchunguzi wa jana ulionyesha kuwa mamia ya wakazi wa jimbo la kiteto mkoani Manyara, walikuwa wamejitokeza kupiga kura katika uchunguzi huo, uliofanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Benedict Losurutia aliyefariki Novemba Mwaka jana.

Watu wengi walijitokeza na kufanya misururu ambayo hata hivyo haikuwa mirefu, pengine kutokana na kuwepo kwa vituo vingi katika kata za jimbo hilo.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Faustine Kang’ombe alithibitisha jana kuwa uchaguzi huo umefanyika kwa amani na utulivu katika vituo vyote 222 na kuwa atakuwa tayari kutangaza matokeo ya jumla ya uchunguzi huo leo majira ya saa 5 asubuhi baada ya kupokea matokeo kutoka katika vituo vyote.

(IMTOLEWA NA MTANZANIA DAIMA 25TH February, 2008)

No comments: