Saturday, August 4, 2007

Simba kujitoa, ni mwanzo wa mwisho wa Tusker?


MICHUANO ya sita ya Kombe la Tusker inaendelea kufanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Safari hii, timu zilizobahatika kushiriki kinyang’anyiro hicho ni Yanga, Mtibwa Sugar, Prisons, na Kagera Sugar za nchini na Tusker ya Kenya na SC Villa ya Uganda. Michuano hii inafanyika Mwanza kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001. Mara zote ilikuwa ikifanyika Dar es Salaam na Simba ilikuwa ikitwaa ubingwa hadi mwaka jana ilipoachia kombe hilo kwa kucharazwa bao 2-1 na Kagera Sugar. Tofauti na miaka iliyopita, safari hii michuano hiyo inachezwa bila kuwapo kwa Simba, bingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, hali inayoifanya kukosa msisimko na kuzua maswali mengi kwa wadau wa soka licha ya kuzungumziwa karibu kila kukicha. Simba ilijitoa kwenye michuano hiyo dakika za mwisho baada ya kutofautiana na wadhamini, Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL), na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kila mmoja anazungumza lake kuhusu kujitoa kwa Simba; wapo wanaoona walikuwa sahihi na kuna wengine wanaona kuwa wamepotoka. Na hiyo ndiyo sababu kubwa ya kupungua kwa msisimko wa michuano hiyo mjini hapa kwani mahudhurio ya mashabiki uwanjani si ya kuridhisha. Licha ya TFF kuonekana kutokuwa wazi katika hilo, lakini ukweli ni kwamba imeathirika kimapato na pengine inaendesha michuano hiyo kwa hasara tofauti na ilivyotegemea. Tayari Simba kupitia Katibu wake mkuu, Mwina Kaduguda, imetangaza kutoshiriki michuano hiyo hadi itakaposikilizwa madai yake. Swali la kujiuliza, ni je, michuano hiyo itaendelea kufanyika bila kuwapo kwa klabu hiyo mojawapo kongwe na maarufu Tanzania? Ni ukweli usiopingika kuwa michuano ya mwaka huu imekosa msisimko, tena kuanzia kwa wadhamini, kwani zile shamrashamra za matangazo redioni, vipeperushi sehemu mbalimbali na hata baa, hayakuwapo tena kama ilivyokuwa niaka ya nyuma. Kila upande kati ya TFF na wadhamini, unaonekana kutojali kujitoa kwa Simba, lakini ukweli ni kwamba kumeathiri hata biashara ya wadhamini ambayo ndiyo lengo kubwa la mashindano hayo. Meneja Masoko wa EABL, Gasto Lyaruu, anakiri kupooza kwa michuano ya mwaka huu, na kueleza kuwa moja ya sababu kubwa ni kutokuwapo kwa maandalizi ya mapema kuhusu kufanyika kwa michuano hiyo jijini Mwanza. Anasema tangu awali michuano hiyo ilikuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kuhamishiwa Morogoro na dakika za mwisho kupelekwa CCM Kirumba, Mwanza. “Ni kweli michuano ya mwaka huu imepooza si kama miaka mingine na hasa mwaka 2005 ilipofanyika hapa, kulikuwa na kila aina ya msisimko na watu waliitikia kwa moyo mmoja mpaka hata ikatutia moyo sisi kama wadhamini. “Lakini kwa kweli mwaka huu ni tofauti kabisa kama unavyoona mwenyewe, lakini naamini kwamba kadri itakavyokuwa ikisonga mbele ndivyo watu watakuwa wanahamasika kuja uwanjani,'' anasema. Anasema mashabiki wa soka wa Mwanza na mikoa ya jirani hawakujua kama michuano hiyo ingehamia Mwanza, hivyo hakuna mtu aliyekuwa amefanya maandalizi ya kwenda kushuhudia michuano hiyo. “Kwa mfano mwaka 2005, tulitangaza mapema kabisa kwamba michuano itakuwa Mwanza kwa hiyo watu wengi walijiandaa kuja kushuhudia mashindano hayo, na ndiyo maana watu walikuwa wengi, lakini ya mwaka huu kwa kweli kulikuwa na misukosuko mingi mara Dar, mara Morogoro, lakini katika dakika za mwisho kabisa ndiyo ikaletwa hapa Mwanza,” anasema. Lyaruu anakiri pia kujitoa kwa Simba ni sababu ya michuano hiyo kuondoka msisimko kwani klabu hiyo ni moja ya klabu kubwa nchini na ukanda wa Afrika Mashariki. “Hili halina ubishi, ni kweli nalo limechangia kudorora kwa michuano ya mwaka huu kwa sababu hakuna ubishi kwamba Simba ni timu kubwa hapa nchini na hata kwa nchi za Afrika ya Mashariki. “Kwa hiyo kutokuwepo kwake katika mashindano ya mwaka huu pia imechangia kupunguza msisimko wake,” anasema Lyaruu. Akizungumzia la mustakabali wa kampuni hiyo kuendelea kudhamini michuano hiyo ama la, Lyaruu anasema kwa sasa wako katika mchakato wa kusuka mkataba mzuri ili kuendelea kuboresha zaidi michuano hiyo. Anasema maneno yanayoelezwa mitaani kwamba huenda wakajitoa katika kudhamini michuano hiyo na hasa kufuatia mgongano uliotokea na kuisababisha Simba kujitoa katika michuano hiyo dakika za mwisho, si ya kweli, kwani anaamini kuanzia msimu ujao mashindano hayo yatakuwa bora zaidi. ''Hapana sisi kama TBL hatuna ugomvi na Simba wala TFF, hayo mambo yaliyojitokeza ni ya kawaida kwa sababu hii ni hiari ya klabu kushiriki ama kutoshiriki,ingawa kitendo hiki si cha kiungwana, haileti picha nzuri. “Lakini nikuhakikishie tu kwamba sisi hili hatuna presha nalo na tunachokifanya hivi sasa ni kuangalia ni namna gani tutaboresha zaidi mashindano haya,'' anasema Lyaruu. “'Nataka niwaondoe wasiwasi wapenzi wa soka wa Tanzania na nchi zote za Afrika ya Mashariki kwa ujumla ambazo timu zao zinanufaika na udhamini wetu kwamba wasiwe na wasiwasi, sisi tayari tulishalenga kudhamini mashindano haya kwa nia ya kuinua kiwango cha soka pamoja na cha wachezaji kwa ujumla. Kwa hiyo, sisi tupo na hasa kwa klabu zitarajie mabadiliko makubwa katika mkataba wetu mpya tutakaoingia kuanzia msimu ujao,” anasema. Kwa maelezo ya wadhamini hao, je wataendelea kudhamini michuano hiyo kwa hasara? Kwa maana kwamba kama Simba itaendelea na msimamo wake, michuano itaendelea kudorora, na je, huu si mwanzo wa mwisho wa Kombe la Tusker? Tusubiri tuone.

No comments: