Monday, August 27, 2007

Hoja za Simba S.C kupinga maamuzi ya TFF

MWISHONI mwa wiki, habari zilizotawala mazungumzo ya wadau mbalimbali wa michezo, ilikuwa ni sakata la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Seif Kaduguda.TFF ilimtuhumu Kaduguda kuwa amelipaka matope shirikisho hilo, kuwa linapata sh milioni 40 kama mgawo wa michuano ya Kombe la Tusker kutoka kwa wadhamini Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).Baada ya utetezi wa awali kukataliwa na TFF na Kaduguda kutakiwa afike mbele ya Kamati ya Mashindano, Jumamosi iliyopita, kujitetea, aliwasilisha barua yake ya kupinga jambo hilo, na TFF ikatangaza kumfungia miezi sita kwa sababu mbalimbali.
Yafuatayo ni maelezo ya klabu ya Simba yaliyotolewa Jumamosi, muda mfupi kabla ya TFF kutangaza kumfungia Kaduguda:
REJEA barua yako yenye kumb: TFF/ADM/COM.07/04 ya tarehe 23.08. 2007, inayomtaka Mwina Kaduguda, Katibu Mkuu wa Simba Sports Club kuhudhuria kikao cha Kamati ya Mashindano kitakachofanyika Jumamosi 25.8.2007 Uwanja wa Taifa, saa nne asubuhi. Uongozi wa Simba Sports Club umekuwa ukifuatilia kwa makini matamshi au kauli za Katibu Mkuu wa TFF, kuhusiana na madai yake kwamba, KATIBU MKUU wa Simba wakati akitoa ufafanuzi kuhusu Simba kujitoa katika mashindano ya Tusker 2007 alipotosha umma.Katibu wa TFF amekuwa akitoa kauli zinazoishawishi jamii, kwamba taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Simba, 29.07.2007 ni yake binafsi au ilikuwa inawakilisha mawazo ya familia yake na sio Kamati ya Utendaji ya Simba S.C.Cha kusikitisha zaidi, kauli zake zimekuwa zikikwepa hoja ya msingi ya TFF, kuweka hadharani mkataba wa Tusker, ili klabu ambazo ni wadau wakubwa na ndizo zinazofanya promosheni zielewe haki zao ndani ya mkataba na badala yake amekuwa akilikuza suala la 40,000,000/=.Kwa mfano: Siku mbili baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba kuwasilisha ufafanuzi, Mwakalebela kupitia vyombo vya habari alikaririwa akisema, “Kaduguda hakujibu chochote”.Wiki mbili baadaye, Mwakalebela huyohuyo, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa Kikao cha Kamati ya Mashindano kilichokutana 18.08.2007 kimetupilia mbali utetezi wa Kaduguda.
Kisheria, Mwakalebela hakutakiwa kutoa maamuzi au hukumu kabla kamati haijakaa. Hii inamaanisha kwamba alikuwa anatumia nafasi au wadhifa wake kuishawishi kamati itoe maamuzi au hukumu anayoitaka yeye binafsi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Simba SC unapenda kuifahamisha TFF kwamba hauna imani na Kamati ya Mashindano na kwamba Kaduguda kama Katibu wa Simba hatohudhuria kikao bali wanaopaswa kuhudhuria kikao ni viongozi wote wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC.
Zifuatazo ni sababu za msingi kuikataa Kamati ya Mashindano:
1.Kifungu cha 40 (2) cha Katiba ya TFF ya 2006 iliyofanyiwa marekebisho Januari 2006 na kugongwa muhuri wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo Nchini, 2.05.2006 (English version), kinaainisha bayana kazi za Kamati ya Mashindano. Hivyo basi, wakati KATIBU MKUU WA SIMBA anatoa ufafanuzi kupitia vyombo vya habari, Simba SC haikuwa kwenye mashindano, kwa maana hiyo kamati haina uwezo kisheria kusikiliza au kutoa adhabu (Incompetent) kwa mujibu wa Katiba ya TFF ya 2.05.2006.
2.Baadhi ya wajumbe wanaounda kamati hiyo ni waajiriwa wa TFF, hivyo basi ni dhahiri kwamba hawatoitendea haki Simba SC kwani:
(a) Kibinaadam upo uwezekano mkubwa wa kufuata ushauri wa bosi wao Mwakalebela.
(b) Wajumbe hao waajiriwa ni sehemu ya TFF. Kisheria huwezi ukamtuhumu mtu au ukamshitaki mtu kisha wewe mwenyewe ukawa sehemu ya chombo kinachotoa maamuzi au hukumu dhidi ya mshitakiwa.
3.Mmoja wa wajumbe wanaounda kamati hiyo ni kiongozi wa ngazi za juu wa Chama cha Makocha wa Soka nchini (TAFCA), ambaye alitoa mchango wa hali na mali kumsimamisha kwa mizengwe Mwina Kaduguda Ukatibu Mkuu wa TAFCA, Machi 2006 na kushindwa kumuita hadi leo mbele ya Mkutano Mkuu wa TAFCA ili ajibu tuhuma za Kamati ya Utendaji ya TAFCA mpaka Kamati hiyo ya Utendaji ya Chama cha Makocha nchini imemaliza muda wake wa kukaa madarakani 1.08.2007 bila ya kumwita Kaduguda mbele ya Mkutano Mkuu wa TAFCA, hivyo hawezi kumtendea haki Katibu Mkuu wa Simba.
4.Mwakalebela alikaririwa na vyombo vya habari Jumatatu akitangaza Kamati ya Mashindano kumwita Kaduguda 20.08.2007, lakini barua ambayo ndio wito rasmi umemfikia Katibu Mkuu wa Simba SC Alhamisi 23.08.2007 saa 10:00 jioni, hii inaonyesha kwamba:Mwakalebela anafanya kazi kupitia vyombo vya habari kitu ambacho si sahihi.
5.Kanuni zinazotumika kutoa adhabu ni za Ligi Kuu ya VODACOM za 2006.Katibu Mkuu wa Simba hakutoa ufafanuzi wakati wa Ligi Kuu ya VODACOM jambo ambalo linaonyesha ni jinsi gani TFF inayoongozwa na wasomi inavyolazimisha mambo na kukwepa hoja ya msingi.
6.Hoja iliyo kubwa na yenye kubeba uzito na TFF inapaswa kuizingatia ni ile inayoainishwa na kifungu 44 (1) na (a) na (b) inayobainisha kwamba vyombo vya kisheria vya TFF ni:-
(a) Kamati ya Nidhamu
(b) Kamati ya Rufaa
Kwa mantiki hii haihitaji hata kuwa Profesa wa Chuo Kikuu kuelewa kwamba Kamati ya Mashindano haina uwezo kisheria, kuhoji tuhuma na kutoa adhabu bali ni Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Rufaa, ndivyo vyenye uwezo kisheria kutekeleza jukumu hilo.
Uongozi wa Simba unapenda kumkumbusha Mwakelebela na TFF kwa ujumla kuwa, wajibu wa kuendeleza soka nchini ni wa wadau wote na si wa TFF peke yake, Mkoa, Wilaya, Klabu na mdau mmoja mmoja, hivyo basi zipo njia nyingi na nzuri za kumaliza matatizo ndani ya jumuiya za soka na sio kutumia utashi binafsi.
Tunapenda kumalizia kwa kusema kwamba, uongozi wa Simba unaiheshimu TFF na uko tayari kukaa na TFF na chombo chenye uwezo kisheria na sio Kamati ya Mashindano, ambayo haina mamlaka kwa mujibu wa Katiba ya TFF ya 2.05.2007 (English Version).
Tunatanguliza shukrani,KAMATI YA UTENDAJI.
Imesainiwa na
Hassan Dalali (Mwenyekiti),
Omar Gumbo (Makamu Mwenyekiti),
Mwina Kaduguda (Katibu Mkuu),
Idd Senkondo (Mweka Hazina),
Chano Almas (Mweka Hazina),
Yassini Mwete (Mjumbe)
Sultani Ahmed (Mjumbe).
Nakala:
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo,
Baraza la Michezo la Taifa,
Mwenyekiti Kamati ya Nidhamu TFF,
Mwenyekiti Kamati ya Rufani TFF,
Mwenyekiti Kamati ya Mashindano.

No comments: