Saturday, July 14, 2007

Watanzania wakataa shirikisho

(muheshimiwa raisi akipokea ripoti kutoka kwa Profesa Samuel Wangwe)

ROBO tatu ya Watanzania waliohojiwa kuhusu haja ya kuharakishwa kwa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki, wamepinga mpango huo.
Ukweli huo umebainishwa katika Ripoti ya Kamati ya Kukusanya Maoni kuhusu Kuharakishwa kwa shirikisho hilo ambayo iliwasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam, jana.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Joseph Wangwe, alimweleza Rais Kikwete kuwa, asilimia 75.9 ya Watanzania waliohojiwa wamepinga uamuzi wa kuharakisha uundwaji wa shirikisho hilo, ilihali ni asilimia 20.8 ndio waliounga mkono mpango huo.
Profesa Wangwe amemweleza rais kwamba jumla ya Watanzania 65.000 walipata fursa ya kutoa maoni yao na kwamba kamati yake ilitembelea mikoa yote 26 na wilaya zote pamoja na kukutana na makundi yote muhimu ya kijami, kama ambavyo rais alivyokuwa ameagiza.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 74.5 walipinga kuharakishwa kwa shirikisho hilo, wakati Zanzibar waliopinga walikuwa ni asilimia 79.
Kwa mujibu wa muhtasari wa ripoti hiyo, asilimia 47.1 ya wananchi wengi waliohojiwa kutoka Mkoa wa Kagera, waliunga mkono uharakishwaji wake na hivyo kuufanya kuwa mkoa ambao watu wengi walikubaliana na mpango huo.
Aidha, asilimia 89.9 ya waliohojiwa Morogoro walipinga uharakishwaji wa shirikisho na wakafuatiwa na wananchi wa Kaskazini Pemba ambao ni asilimia 87.5 na hivyo kuifanya mikoa hiyo kwa na idadi kubwa ya watu ambao walikataa kuunga mkono ajenda hiyo.
Ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba, asilimia 76.7 ya wanawake waliohojiwa walipinga kuharakishwa kwa shirikisho hilo wakati wanaume waliokataa kwa nchi nzima walikuwa ni asilimia 73.9.
Wangwe alimueleza Rais Kikwete kuwa, ukusanyaji wa maoni hayo umechukua muda mrefu kutokana na umuhimu wa jambo lenyewe, lakini pamoja na kuzingatia maagizo waliyopewa na rais mwenyewe.
Alisema, njia mbalimbali zilitumika katika ukusanyaji wa maoni hayo zikiwamo za mikutano ya hadhara, madodoso, radio, televisheni na tovuti.
Aidha, Profesa Wangwe alibainisha kwamba, taarifa hiyo ambayo imo katika vitabu viwili pamoja na mkanda wa video, imegawanywa katika maeneo makuu mawili – ambayo ni ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Katika siasa, Profesa Wangwe alieleza kuwa, elimu ya ufahamu kuhusu shirikisho ni jambo ambalo lilisisitizwa na wananchi wakati wakitoa maoni yao.
Takwimu zinaonyesha kwamba, asilimia 80.2 ya wananchi wote waliohojiwa walionyesha kufahamu vyema kuhusu maana ya shirikisho hilo na kwamba asilimia 17.1 walikiri kutofahamu na wengine asilimia 2.6 wakasema walikuwa hawana uhakika.
“Kuhusu demokrasia na utawala bora, wananchi walionyesha wasiwasi wao kama nchi jirani zina demokrasia na utawala bora kiasi cha kuridhisha kuwa na shirikisho.
“Lakini pia suala la kero za muungano lilijitokeza huku wananchi wakishauri kwamba, kero hizo zipatiwe ufumbuzi kabla ya kuingia kwenye shirikisho,” akasema.
Ameeleza kuwa katika sababu hizo za kisiasa, wananchi pia walielezea wasiwasi wao kuhusu tofauti za kiitikadi kwamba bado kuna tofauti ambazo ni lazima zishughulikiwe.
Kwa upande wa uchumi na maendeleo ya kijamii, Profesa Wangwe alisema, Watanzania wengi wamekuwa na wasiwasi katika mambo manne.
Kwanza ni tofauti za kiuchimi kati ya Tanzania na Kenya, pili uwezo wa ushindani wa kibiashara na hasa soko la ajira, tatu ni umuhimu wa kuweka misingi mizuri ya kiuchumi na nne umiliki wa ardhi na maliasili.
“Kwa wale wanaosema tuharakishe uundwaji wa shirikisho, nao walielezea faida mbalimbali kuhusu shirikisho hilo. Lakini pia Mheshimiwa Rais kuna maswali mengine yaliyojitokeza ambayo hayahusiani na mambo ya shirikisho na ni ya kitaifa, nayo pia tumeyaweka kwenye ripoti hiyo,” alieleza Wangwe.
Akihitimisha maelezo yake, Professa Wangwe alimweleza rais kwamba, katika mchakato huo wa kukusanya maoni hayo, wananchi waliihoji kamati kama maoni yao yangefikishwa kwa rais kama yalivyo na kama yatafikishwa, je, yatafanyiwa kazi?
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Kikwete alisema kuwa, baada ya kamati kukamilisha kazi yake, sasa kazi iliyobaki ni ya serikali na akaongeza kuwa, ripoti hiyo itawasilishwa katika Baraza la Mawaziri na Waziri anayeshughulikia Jumuia ya Afrika Mashariki, Profesa Ibrahim Msabaha.
“Baada ya kuwasilisha katika Baraza la Mawaziri, wizara husika watakutana na wenzao na Sekretariati ya Afrika Mashariki.
“Ninawashukuru sana kwa kazi nzuri na kwa ripoti hii nzuri mliyonikabidhii, nawashukuruni kwa uvumilivu maana hata kusikiliza nako kunahitaji uvumilivu, nina imani wako baadhi ya wananchi waliokuwa wakali sana kuhusu mchakato huu na wakawafokea kama vile nyie ndio mlioliamua jambo hili. Mmemaliza kazi yenu, sasa kazi iliyobaki tuachie sisi,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu kama serikali itayazingatia na kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wananchi, Rais Kikwete amewahakikishia wananchi kwamba serikali imeyapokea maoni yao na itayafanyia kazi kwa kuzingatia ushauri wao.
Kamati ya kukusanya maoni kuhusu uharakishwaji uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki ilianza kazi yake Oktoba mwaka jana na ikaikamilisha jana.

No comments: