Wednesday, June 20, 2007

Wabunge CCM waishangaa bajeti

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Siha, Agrey Mwanri, jana aliungana na wabunge wengine kuponda utekelezaji wa serikali na kudai kuwa uchumi unaojengwa nchini ni wa kikoloni mamboleo.
Akitoa mchango wake bungeni jana jioni, Mwanri alisema kuwa licha ya uchumi wa Tanzania kuwa wa kikoloni mamboleo, bado upo nyuma na si endelevu.
Katika mchango huo, Mwanri alikosoa bajeti iliyowasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, inayoonyesha utegemezi wa wafadhili kwa zaidi ya asilimia 40, na kusema kuwa nchi haiwezi kuendelea kwa kutegemea fedha kutoka nje ya nchi.
Alisema bajeti ya serikali ni tegemezi na iwapo fedha zilizokadiriwa kutumika katika bajeti ya mwaka wa fedha 2007/08 hazitapatikana zote, kunaweza kuwa na nakisi kubwa katika utekelezaji wa bajeti hiyo.
Alibainisha kuwa nchi za nje wanapenda kuendelea kuisaidia Tanzania ili waendelee kuitawala kwani hata sasa haiko huru.
“Mtu hawezi kukupa fedha yake akakuacha tu, lazima akupangie cha kufanya, lakini kama hajakusaidia, hawezi kukupangia, maana unaweza kumuuliza kwani huwa nakula kwako?” alisema Mwanri kwa hisia kali kama ilivyo kawaida yake.
Alisema kama bajeti inapangiwa fedha zote kila jambo bila kuwa na ziada, hiyo si bajeti ya maendeleo kutokana na kukosa ziada.
Alisema bajeti nyingi zimekuwa zikikosa ‘mtekenyo wa ndani’ na kupapasa juu juu, hali inayoweza kukwamisha maendeleo na uchumi wa nchi nzima.
Aliwataka Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Rais Jakaya Kikwete, kusonga mbele ili kuifanya nchi iachane na utegemezi na isimame yenyewe katika kujiletea maendeleo endelevu sanjari na kukuza uchumi.
Mwanri alisema tatizo la Tanzania ni umaskini na ndiyo unaifanya iendelee kuwa na uchumi wa nyuma, duni, tegemezi na wa kiukoloni mamboleo, ambao hauwasaidii Watanzania wengi.
Alisema kupanda kwa mafuta kutasababisha gharama za uzalishaji kuongezeka, hivyo serikali ihakikishe inasimamia kikamilifu bajeti hiyo kwa manufaa ya Watanzania.
“Ongezeni bei ya mafuta lakini msimamie mfumko wa bei kwa kuangalia kiwango… kama kiwango kilichoongezwa kinalingana na bei inayouzwa kwa mafuta yaliyoongezewa kodi,” Mwanri aliiambia serikali kupitia Bunge.
Alisema serikali ibebe jukumu la kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya kibajeti ili kuwapunguzia mzigo wananchi na fedha zilizotengwa katika bajeti zifanye kazi zinazoonekana kwa wananchi.
Hata hivyo, Mwanri aliwasihi wapinzani kuipitisha bajeti hiyo bila kuipinga ili kusubiri utekelezaji wake.
Wabunge wengine waliionya serikali kuwa lengo lake la kukusanya mapato mengi kutoka kwenye mafuta, halitafikiwa kutokana na hujuma inayofanywa na wafanyabiashara wa bidhaa hizo Mkoa wa Pwani.
Akichangia mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2007/08, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alisema kodi mpya iliyopendekezwa kwa dizeli haitapatikana kwa sababu vituo vyote vya Mkoa wa Pwani, vinatumika kubadilisha dizeli na kuweka mafuta ya taa.
Shabiby, ambaye naye anamiliki vituo kadhaa vya kuuzia mafuta, alisema ongezeko la kodi kwenye dizeli ni sh 512 na mafuta ya taa ni sh 56, tofauti yake ni sh 456 na kwamba, watakachofanya wafanyabiashara ni kulipa kodi ya dizeli na kuchanganya mafuta ya taa.
“Kwa mtu yeyote akipitia mkoani Pwani ataona vituo vingi vimejengwa vina maghala ndani, kazi kubwa ni kupakua, kubadilisha dizeli na kupakia mafuta ya taa. Kazi hiyo ni maarufu kama chakachua,” alisema Shabiby na kuongeza:
“Gari lenye ujazo wa lita 35,000 za dizeli linapakua lita 9,000 na kuingiza kiasi hicho hicho cha mafuta ya taa. Hesabu ya haraka linakuwa limekwepa kodi ya sh 4,104,000, hilo ni gari moja.”
Alisema tofauti ya mafuta ya taa na dizeli, isipoangaliwa na kusimamiwa vizuri itanufaisha wafanyabiashara wadanganyifu na kwamba, wakaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hawafanyi kazi zao inavyotakiwa.
Kuhusu kuongeza kodi ya leseni za magari, mbunge huyo alipendekeza kiwango cha 1,500CC ibaki sh 80,000 badala ya sh 230,000 zilizopendekezwa na serikali kwa sababu watu wengi watakwepa kodi.
Mbunge wa Mvomero (CCM), Suleiman Sadiq, alisema tatizo analoliona ni ongezeko la sh 4 kwenye mafuta ya taa na kupendekeza bei kubaki ile ya zamani.
“Naomba chonde chonde serikali ifuatile eneo la Mkoa wa Pwani, kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara wa mafuta, fedha nyingi za serikali zinapotea,” alisema Sadiq.
Akichangia upande wa leseni za magari, Sadiq alisema 1,500CC ni gari dogo, sh 230,000 zilizopendekezwa itakuwa mzigo mkubwa na inahusu watumishi na wananchi wa kada ya chini.
“Sisi wenye VX tuache tuendelee, hatuna matatizo tutalipa. Lakini fedha zinazotokana na leseni za magari tukubaliane ziende moja kwa moja kwenye barabara, maana (Harry) Kitilya (Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA), iko janja sana, ameona eneo hili limechangia sana akaongeza,” alisema.

1 comment:

Anonymous said...

ccm kavu tu,haina faida wala nini inazingua tu