Wednesday, June 20, 2007

Neema yazidi kuiangukia Taifa Stars

NEEMA imezidi kuwashukia wachezaji wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, baada ya Benki ya National Microfinance (NMB), nayo jana kuwamwagia sh mil. 17.
Huu ni mwendelezo wa neema kwa timu hiyo iliyowasili jijini Mwanza Jumapili usiku ikitokea Burkina Faso na kutua Dar es Salaam juzi jioni.
Kabla ya kutua Dar es Salaam, msafara wa timu hiyo ulipitia bungeni na kufanyiwa harambee na kuchangiwa kiasi cha sh mil. 322.5.
Kiasi hicho cha juzi, ni jumla ya fedha taslimu na ahadi mbalimbali zilizotolewa na wabunge, mawaziri na taasisi za serikali na watu binafsi.
Fedha hizo ni zawadi kwa wachezaji hao kutokana na ushujaa wao wa kuishinda Burkina Faso 1-0, mechi iliyopigwa nchini humo Juni 16.
Siku moja baada ya Stars kuvuna kiasi hicho, NMB nayo imeamua kuungana na wengine katika kuwapongeza wachezaji na viongozi wa timu hiyo.
Ahadi ya NMB, ilitolewa jana katika hafla fupi ya chakula cha mchana, kilichoandaliwa na benki hiyo kwa wachezaji hao katika hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ben Christiaanse, alisema jana kuwa, wao kama wafadhili, wamefurahishwa na kazi kubwa iliyofanywa na Stars.
Alisema, ushindi wa Stars dhidi ya Burkina Faso, umewagusa wengi, hivyo wao kama moja ya taasisi za fedha walio na wajibu wa kuwajengea maisha ya baadaye wateja wao, wameamua kutoa fedha hizo sambamba na kuwafungulia akaunti.
Meneja huyo alisema fedha hizo za wachezaji na viongozi, zitawekwa kwenye akaunti zitakazofunguliwa katika benki hiyo kama mfano wa kujiwekea akiba ya baadaye.
Mtendaji mkuu huyo aliongeza kuwa jumla ya wachezaji na viongozi 34, kila mmoja atapata sh 500,000 ambazo watawekewa katika akaunti mbili tofauti, yaani Personal na Bonus.
Alisema, ni matarajio yao na Watanzania kwa ujumla kuwa, Stars itashinda mechi dhidi ya Msumbiji, inayotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja mpya wa Taifa, Septemba 8 jijini Dar es Salaam.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mkurugenzi wa Utawala na Uanachama, Raymond Wawa, aliipongeza NMB kwa msaada huo, ambao uko nje ya mkataba uliopo.
“Unajua mtu anayekusaidia kitu kwa ajili ya maisha yajayo ni mtu muhimu kwako, hivyo tunawashukuru sana na itakuwa ni changamoto zaidi kwa wachezaji.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wachezaji wa Stars, walioongozwa na nahodha Mecky Maxime, Kocha Mkuu, Marcio Maximo, kocha wa viungo, Itamar Amorin, Kocha Msaidizi Ali Bushir, Kocha wa Vijana, Marcos Tinoco na Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa NMB, Imani Kajura.

No comments: