By Waandishi Wetu, Mwananchi Dar es Salaam. Wadau wawili wa michezo na burudani nchini; Yusuf Manji na Said Fella wameibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha udiwani katika jimbo jipya la Mbagala jijini hapa. Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality Group, alishinda katika udiwani katika Kata ya Mbagala Kuu wakati Fella ambaye ni msimamizi wa kazi za wasanii na muasisi wa Kundi la Mkubwa na Wanawe, alishinda katika Kata ya Kilungure. Fella ni Meneja wa mwanamuziki maarufu nchini, Diamond Platnumz, TMK Family na Yamoto Band. Kaimu Katibu CCM Wilaya ya Temeke, Rutami Masunu alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri katika maeneo mengi isipokuwa changamoto kidogo katika kata moja ambayo itafanya uchaguzi huo leo. Alisema tayari matokeo ya kata 28 kati ya 32 za wilaya yake yamewasilishwa ofisini kwake na baada ya kuyapitia na kukusanya taarifa zinazowahusu madiwani na wabunge na muda wowote leo atatoa taarifa kamili. Vurugu Jangwani, Buguruni Uchaguzi wa kumteua mgombea wa udiwani Kata ya Jangwani wilayani Ilala, umeingia dosari baada ya kikundi cha vijana wanaosadikiwa kutokea Kinondoni kuvuruga upigaji kura na kuvunja hema jambo lililosababisha polisi kuingilia kati. Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Ramadhan Manda alisema jana kuwa kundi hilo linadaiwa kutumwa na watoto wa mmoja wa wagombea kutokana na dalili za wazi za kushindwa uchaguzi huo. Mkazi wa Mtaa wa Mtambani B, Suleiman Maarufu alisema: “Saa nne asubuhi nilisikia vurugu nje, nikatoka na kuona kikundi cha vijana kutoka Tawi la Mkombozi kikivutana na mmoja wa makada ninayemfahamu. Wale vijana wakapiga teke masanduku, wakavunja hema… sasa wakati naingia kuamulia, wakanipa misukosuko na kipigo na baada ya kuamka nikakuta nimeumia unyayoni na kwenye goti.” Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Ernest Chale alisema ni makundi matatu ya wagombea yaliyochangia kuibuka kwa vurugu hizo na kusababisha uchaguzi kutomalizika. “Kutokana na haya yaliyotokea tutakaa vikao vya siasa kujadili, kwa maana hiyo hii kata itaendeshwa kama eneo maalumu. Kinachoonekana hapa mtu anatafuta uongozi kwa nguvu lakini uongozi unatolewa na Mungu, mimi naona ni bora akatulia kama anaona haki haitatendeka ni bora angesubiri akate rufaa.” Mmoja ya wagombea wa udiwani, Abdul Faraji alisema: “Uchaguzi ilibidi ufanyike jana (juzi) na maeneo mengine lakini uliahirishwa kutokana na matatizo ya kwenye matawi… sasa tena unaahirishwa lakini hapa inaonekana bayana ni vigumu haki kutendeka.” Katika Kata ya Buguruni wilayani Ilala, baadhi ya wanaCCM ambao tangu juzi walikesha kwenye ofisi cha chama hicho kulinda kura za wagombea udiwani, wanadaiwa kumshambulia Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Tawi la Madenge, Ramadhani Mfinanga. Tangu juzi saa tano usiku, wanaCCM hao wanaofikia 40 waliweka kambi katika ofisi hizo wakipinga matokeo ya kura za maoni zilizopigwa katika Tawi la Kisiwani. Mfinanga alifika jana katika ofisi hizo na kusema matokeo hayatabadilishwa kauli iliyowakera na kuanza kumshambulia hadi alipojinasua baada ya kujichanganya na wafanyabiashara walioko katika Soko la Buguruni. Mmoja wa wagombea wa udiwani katika Kata ya Buguruni, Barua Mwakatanga alisema walibaini kwamba kura zilizopigwa katika Tawi la Kisiwani zilikuwa 411 wakati idadi ya wapigakura ilikuwa 337. Alisema walimweleza Katibu wa CCM, Kata ya Buguruni ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi, Abdul Kinogozi aliyewata wapeleke masanduku kwenye Ofisi za Kata ya Buguruni kwa ajili ya uhakiki. “Tulipeleka lakini ilipofika saa tano usiku alisema amechoka na uhakiki utafanyika kuanzia saa mbili asubuhi leo (jana),” alisema. WanaCCM hao waliamua kukesha ili kulinda kura hizo zisibadilishwe wakidai kuna njama za ‘kumbeba’ mgombea mmoja. Kinogozi alisema matokeo hayajatangazwa kwa sababu ya malalamiko ya mmoja wa wagombea na kwamba yatatangazwa baada ya uhakiki utakaofanywa na wagombea wote. Wanaowania nafasi za udiwani ni Musolo Pazi, Magina Lufungulo, Barua Mwakilanga, Abdallah Jaza na Mushokeli Mandali. Imeandikwa na Nuzulack Dausen, Julius Mathias na Raymond Kaminyoge
Monday, August 3, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment