Rehema Matowo, Moshi
WAKUU wa Wilaya za Taveta na Lotokitok, nchini Kenya, wameiomba Serikali ya Tanzania kuruhusu wafanyabiashara wa mazao ya chakula wa nchi hiyo jirani, kuingia nchini kwa lengo la kununua chakula ili kukabiliana na upungufu mkubwa chakula unaoikumba Kenya kwa sasa.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Taveta, Nkaduda Hiribae, alipokuwa akizungumza katika kikao cha ujirani mwema, kilichofanyika mjini Moshi.
Kikao hicho kiliwahusha wakuu wa wilaya hizo za Kenya na wakuu wa wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro, ambao kwa pamoja, walisaini maazimio yanayotokana na kikao cha kudhibiti uhalifu mipakani, kilichofanyika Julai 13 mwaka huu, katika eneo la Holili, wilayani Rombo.
Hiribae alisema Serikali ya Kenya inaunga mkono agizo la Serikali ya Tanzania kuhusu kudhibiti usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi, lakini ni vyema serikali hiyo ikaona umuhimu wa kusaidia majirani pale wanapokabiliwa na baa la njaa.
Alisema kwa sasa Kenya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula uliofikia kiwango cha asilimia 70, hali ambayo ni tishio kwa usalama wa maisha ya wananchi.
Aliiomba Serikali ya Tanzania, kufungua milango kwa wafanyabiashara wa Kenya, kuingia nchini na kununua chakula kwa njia halali, jambo ambalo pia litaipatia mapato serikali.
Akizungumzia ombi lililotolewa na Hiribae ,Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Musa Samizi, alisema wao kama wakuu wa wilaya, hawana mamlaka ya kutoa vibali vya kuruhusu wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania kununua chakula na kukiuza Kenya.
Alisema wanachoweza kukifanya ni kuwasiliana na ofisi ya Waziri Mkuu na kufikisha ombi hilo kwa utekelezaji.
Kuhusu maazimio waliyoyaazimia mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Peter Toima, alisema ni pamoja na pande zote mbili kushirikiana katika kutoa taarifa zitakazosaidia kuzuia uvushaji haramu wa chakula na uhalifu mwingine.
Alisema azimio lingine ni kuangalia namna wakuu wa wilaya hizo watakavyowasiliana na wizara za Chakula katika pande zote mbili, ili kuona ni jinsi Serikali ya Tanzania inavyowaruhusu Wakenya kununua chakula kutika nchini hata kwa muda mfupi ili kutatua tatizo la njaa linalokabili Kenya.
Mwenyekiti huyo alisema maazimio mengine ni kuanzishwa kwa soko la mazao katika maeneo ya karibu na mpaka wa Holili na Himo ili kuwezesha wafanyabiashara kutoka Kenya, kuja kununua mazao kwa kupitia njia halali na kulipa kodi.
Alisema pamoja na kuazimia kuanzishwa kwa soko la mazao pia wameazimia kufuatilia kwa pamoja maghala yote yaliyoko katika maeneo ya mipakani na kuyachunguza kwani mengi yamekuwa yakitumika kuhifadhia magendo na hata wahalifu.
Sunday, July 24, 2011
Kenya yaomba Tz iruhusu usafirishaji wa mahindi
Posted by Mafia Kisiwani at 10:14 AM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment