Wednesday, November 10, 2010

Mtikila: Viongozi wa dini wanafiki

na Andrew Chale




MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameponda hatua ya ujumbe wa viongozi wa dini nchini kumtaka Dk. Willibrod Slaa, kukubali matokeo ya kushindwa kwenye uchaguzi wa rais uliomalizika hivi karibini na kuwafananisha na Yuda Eskalioti, aliyepewa vipande 30 vya fedha kisha kumsaliti Yesu.

Mtikila aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akiongea na Tanzania Daima, akidai kuwa, kitendo hicho ni cha kinafki, kwani viongozi hao hawakupaswa kumfuata Dk. Slaa na ujumbe wao huo wa kumtaka akubali matokeo ili kulinusuru taifa na machafuko ya kisiasa.

Badala yake aliwataka viongozi hao wangeanza kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na Rais Kikwete ili kuona hatua ya kufuata ili kuzuia mpasuko uliopo sasa nchini.

“Tume imekubali kuwa kulikuwa na makosa mbalimbali kwenye uchaguzi na watayafanyia kazi ili yasitokee tena, vivyo hivyo walitakiwa kumfuata na Rais Kikwete ili kumuona angesemaje juu ya hatua hiyo ya Dk. Slaa, lakini kwa kitendo cha kwenda kwa Dk. Slaa sasa ni cha kinafki na ndio wanaoifanya dini kama mradi wa kuficha maovu,” alisema Mtikila.

Akinukuu vifungu vya Biblia, kikiwamo cha Tito 2:11, Waraka wa pili wa Timotheo 4:2, ambavyo vyote vinalaani na kukemea machafuko na dhuluma kwa wanadamu, Mtikila alisema kuwa viongozi wa dini wameafiki hali ya uchakachuaji uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuiba kura za wananchi na kudhani ni za Dk. Slaa.

“Kilichotakiwa kufanywa na viongozi hawa wa dini kama wanaona kuna machafuko, walitakiwa wagome kwa pamoja hatua ya kuapishwa kwa rais na kudai maridhiano ya pamoja. Lakini wao waliafiki moja kwa moja kwa kukubali kupewa vipande 30 vya fedha kama Yuda na kisha kumsaliti Yesu,” alisema Mtikila.

Aidha, Mtikila alikubaliana na hatua hiyo ya Dk. Slaa kuyakataa matokeo hayo yaliyochakachuliwa, kwani ni kitendo cha dhahiri, anasimamia masilahi ya taifa ambalo lilimchagua ili awakomboe.

“Kura zilizoibwa na CCM ni za wananchi wote wa Tanzania wanaopenda mageuzi ya kweli, waliochoka na manyanyaso na masuala ya ufisadi, ijulikane hawakumuibia Dk. Slaa ambaye kura yake ni moja tu,” alimalizia Mtikila.

Alisema kuwa kama ingekuwa ni wahuni tu wanamfuata Dk. Slaa na kumtaka akubali matokeo, tungesema wameshalewa madawa, lakini viongozi wa dini ambao ni taswira kwenye taifa ni jambo la kushangaza, halitavumiliwa kamwe na lisifumbiwe macho,” alisema Mtikila.

Pia aliweza kutolea mfano juu ya nchi mbalimbali ambazo viongozi wa dini waliamua kupambana waziwazi ili kulinda hali ya amani, ikiwemo kutoa ushawishi mkubwa wa kupatikana haki ya msingi, ambapo ushawishi wao ulisaidia kufanikisha baadhi ya mambo.

Mtikila alizitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na maaskofu wa nchi ya Afrika Kusini, waliokuwa upande wa watu walioonewa wa vyama vya ANC na PNC, kwa Malawi viongozi wa dini 16 waliamua kwa pamoja kumpinga Rais Banda.

Hivyo hivyo ilifanyika katika nchi za Ukraine, Thailand na Kenya, ambao walikuwa na machafuko makubwa.

No comments: